TAWIRI KUFANYA KONGAMANO LA KIMATAIFA LITAKALOSHIRIKISHA WATU 500
Na Andrew Charle, Dar es Salaam
TAASISI ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) inatarajiwa kufanya kongamano kubwa la Kimataifa la 14 la Kisayansi litakalokutanisha washiriki zaidi ya 500 kutoka nchi zote Duniani.
Lengo ni kujadili uhifadhi wa wanyamapori nchini, changamoto zake , na kupokea mapendeko ya kupunguza changamoto hizo kwa ajili ya uhifadhi endelevu na kuboresha maendeleo ya Jamii.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dk.Eblate Mjingo katika taarifa yake kwa Umma.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa wa siku Tatu, yaani Desemba 6-8,2023 katika ukumbi wa Kimataifa wa AICC Jijini Arusha, mada kuu: “Mahusiano mema baina ya Binadamu na Wanyamapori kwa ajili ya uhifadhi endelevu wa Bioanuai na maendeleo ya kijamii na kiuchumi”
(Human-Wildlife Coexistence for biodiversity conservation and social-economic development ).
Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa, zoezi la usajili kwa washiriki limeshaanza na linatarajiwa kufikia tamati Julai 30, mwaka huu huku maelezo kamili namna ya kujiandikisha na kushiriki yakipatikana kwenye tovuti ya Taasisi hiyo ya TAWIRI.
"Jiandikishe sasa, mchango wako unahitajika sana ndani ya Kongamano kutakuwa na mambo mbalimbali ikiwemo mikutano mikubwa, mijadala, maonesho ya biashara mbalimbali katika sekta ya Uhifadhi, Utalii, Mazingira na mengine mengi" amesema Mjingo katika taarifa yake hiyo.
Aidha, Mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwemo Mahuasiano baina ya Binadamu na Wanyamapori, Utalii kwa maendeleo ya kijamii na uchumi, Ikolojia ya wanyamapori na mahusiano yao, ufuatiliaji wa mienendo ya wanyamapori nchini na wanyama walioko hatarini kutoweka
Pia mada za Afya ya mifumo Ikolojia na magonjwa ya wanyamapori, rasilimali maji na uhifadhi wa ardhi oevu, Mabadiliko Tabia nchi, Ikolojia ya nyuki, ufugaji bora wa nyuki, na utalii wa nyuki, ikolojia ya mimea, mimea vamizi na hifadhi ya makazi ya wanyamapori.
Katika Kongamano hilo, pia warsha, semina, mikutano ya kirafiki, mazungumzo, mijadala mbalimbali inakaribishwa kwa kuwasiliana na Kamati ya Maandalizi kupitia tovuti ya TAWIRI.
Post a Comment