WANAKITONGOJI WAMTAKA DIWANI AWAPE MWONGOZO WA MICHANGO NA BOQ
>> Washangaa kuchangishwa fedha za ujenzi wa madarasa ambayo tayari Serikali Kuu imetoa Tsh. Milioni 75 kujenga vyumba vitatu vya madarasa na Tsh. Milioni 6.6 za ujenzi wa choo cha matundu matatu.
Na Dinna Maningo, Butiama
WANANCHI wa Kitongoji cha Wakiriba Kijiji cha Magunga, Kata ya Mirwa wilaya ya Butiama mkoani Mara wamemtaka Diwani wa Kata hiyo, Willy Brouwn kuwapa mwongozo wa Serikali.
Wananchi wanataka mwongozo kuhusu wananchi kuchangia michango ya fedha za ujenzi wa shule pamoja na mchanganuo wa gharama za ujenzi (BOQ) kiasi cha fedha Tsh. Milioni 81.6 zilizotolewa na Serikali Kuu kujenga vyumba vitatu vya madarasa na choo matundu matatu shule ya msingi Kamimange.
Kati ya fedha hizo Tsh. Milioni 75 ni za kujenga vyumba vitatu vya madarasa na Tsh. Milioni 6.6 kujenga choo cha matundu matatu.
Habari zilizotufikia kupitia vyanzo vyetu vya habari zinasema kuwa agizo hilo limetolewa na wananchi wa Kitongoji hicho mbele ya Diwani wao katika mkutano wa Kitongoji cha Wakiriba uliofanyika siku ya Jumanne Mei, 23, 2023.
Wananchi wamemtaka Diwani kuwapatia mwongozo na B.O.Q katika mkutano ujao wa Kitongoji hicho utakaofanyika Jumanne ijayo, Mei, 30,2023.
Ni baada kuwepo sintofahamu ya kiasi kilichotolewa na Serikali kujenga madarasa hayo na choo lakini Mtendaji wa Kata na wa Kijiji kupitia kikao cha wazazi kilichoketi Aprili, 28, 2023, waliagiza wazazi na wananchi kuchangia viashiria Tsh. Milioni 18.6 katika Vitongoji viwili kuliko na shule hiyo ili kununua, mawe, mchanga na kokoto.
Habari zinasema kuwa jumla ya Tsh. Milioni 18.6 zinatakiwa kuchangwa na wananchi katika vitongoji viwili, Kitongoji cha Kitalamanka Tsh. Milioni 9.3 na Kitongoji cha Wakiriba Tsh. Milioni 9.3 huku kila kaya ikitakiwa kulipa kati ya Tsh.20,000 na 15,000.
Changizo hilo limeibua maswali kwa wananchi na wazazi katika Vitongoji hivyo kudai kwanini wachangishwe fedha wakati Serikali yao imeshatoa fedha za ujenzi.
Wananchi wa Kitongoji cha Wakiriba wameomba mwongozo wa Serikali na BOQ ili wajiridhishe kama wanatakiwa kuchangia ujenzi ambao tayari Serikali imegharamia huku Kitongoji cha Kitalamanka baadhi yao wakichanga fedha na wengine wamekataa .
Moja ya Stakabadhi ya malipo ya mchango wa ujenzi wa madarasa aliyopewa mwananchi baada ya kulipa Tsh. 19500.
Diwani wa kata hiyo ya Mirwa aliahidi kuwasilisha mwongozo na BOQ kupitia watendaji katika mkutano ujao wa Kitongoji hicho utakayofanyika Jumanne ya wiki ijayo huku akisisitiza kuwa wananchi kuchangia viashiria ni lazima kwakuwa maeneo mengi hufanya hivyo.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Patricia Kabaka alisema hakuna maagizo kutoka ofisini kwake ya kuwataka wananchi kuchangia ujenzi.
"Hakuna kitu kama hicho, hakuna maagizo yoyote yaliyotoka katika ofisi ya Ded kama hayo" amesema Patricia.
Hadi sasa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na choo haujaanza kutokana na kuwepo mvutano huo wa wananchi kuchangishwa fedha.
Mei, 22, 2023, DIMA Online iliripoti habari yenye kichwa cha habari kisemacho WANANCHI WACHANGISHWA MILIONI 18.6 UJENZI WA MADARASA 3 AMBAYO SERIKALI IMETOA MILIONI 81.6.
Post a Comment