ZAID YA WATALII MILIONI 1.2 WATEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII MWAKA 2022
>>Bodi ya Utalii Tanzania yampongeza Rais Samia Filamu ya Royal Tour
Na Boniface Gideon, Tanga
ZAIDI ya Watalii Million 1.2 kutoka Mataifa mbalimbali wametembelea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini Tanzania kwa kipindi cha mwaka 2022 ikiwa ni idadi kubwa licha ya kutokea janga la ugojwa wa COVID – 19.
Hayo yameelezwa na Afisa Utalii kutoka Bodi ya Utalii Tanzania William Halule wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya biashara na utalii yanayoendelea kufanyika mkoani Tanga.
Maonesho hayo yanajumuisha makampuni, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali kwa lengo la kutangaza biashara na huduma wanazozitoa kwa jamii.
Amesema kuwa licha ya mlipuko wa janga la COVID -19 na hata baada ya ugonjwa huo bado watalii walimiminika kutoka mataifa mbalimbali kuja kujionea vivutio vilivyopo katika hifadhi mbalimbali zulizopo nchini.
Amesema kuwa ongezeko hilo la Watalii limechangiwa na uzinduzi wa filamu ya Royal tour iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa nchini Marekani.
“Muitikio ni mkubwa sana baada ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan kufanya Royal tour kweli wazungu wameongezeka sana kama mwaka jana tumepata watalii Million 1.2 kulikuwa na janga la ugonjwa wa COVID -19 lakini bado tukapata watalii wengi, hii ilitokana na ziara ile ya Rais kutangaza Roayal tour “amesema
Kwa upande wake Afisa Utalii kutoka Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Athumani Mbaye amesema hifadhi zote zinazosimamiwa na TANAPA zimekuwa zikipata watalii wengi wa ndani na nje hii ikisadifu matokeo na hamasa kubwa iliyopatikana kupitia filamu ya Royal tour iliyochezwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni jitihada za serikali ya awamu ya 6 kuzitangaza Tanzania kimataifa kupitia sekta ya utalii.
"Kwa kweli utalii unakuwa siku hadi siku na hii inayokana na juhudi kubwa ambazo zinafanywa na shirika la hifadhi za Tanzania "TANAPA".
"Pia kupitia Royal tour ambayo aliizindua Rais Samia Suluhu Hassan amefanya juhudi kubwa kuzitangaza hizi hifadhi tangu ametoa hiyo filamu utalii umekua na tumejulikana sana kimataifa.
" Tunapata wageni wengi kutoka nje lakini pia na watalii wa ndani watanzania wenyewe wamekuwa na muamko kwa kuona kwamba Rais wetu anaweka juhudi kubwa katika sekta ya utalii" amesema Athuman.
Amesema licha ya ongezeko la watalii wa ndani na nje kumekuwa na changamoto ya miundombinu mibovu hasa kipindi cha mvua barabara zimekuwa hazipitiki kiurahisi.
"Hata hivyo Serikali iliona hilo hivyo na kutoa fedha kwaajili ya ukarabatI wa barabara zote ili kuhakikisha zinapitika kiurahisi.
" Changamoto kama miundombinu wakati wa masika linakuwa na shida, ufikaji wa maeneo ya hifadhi kidogo barabara zinaleta shida lakini Serikali inaleta fedha nyingi za kurekebisha hizo barabara kwa sasa hivi barabara zote zinapitika kwa muda wote" amesema.
Ameongeza kusema kuwa, kupitia maonyesho ya biashara na utalii yanayofanyika kila mwaka mkoani Tanga yamekuwa na tija kwa upande wa TANAPA.
Amesema wanayatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuvijua vivutio vilivyopo sehemu mbalimbali hapa nchini na faida ya kuvitembelea.
"Ni fursa ya kipekee kupitia maonyesho haya kuzitangaza hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa wakazi wa Tanga lakini pia kwa watanzania wote kuvijua vivutio mbalimbali vilivyopo ili kuzielewa hizi mbuga ziko wapi , vivuyio vilivyopo , shughuli zinazofanyika" amesema Athuman.
Shirika la Hifadhi ya Tanzania (TANAPA) linalosimamia hifadhi takribani 22 hapa nchini zikiwemo Mkomazi, Mikumi , Saadan, hifadhi ya Nyerere, linaendelea kuwakaribisha watanzania wakiwemo watalii wa ndani kwenda kutembelea na kujifunza pamoja na kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana ambapo kiingilio ni Tsh.elfu tano mia nne(5,400) kwa kila mmoja.
Post a Comment