HEADER AD

HEADER AD

TCRA : WAANDISHI WA HABARI MARA ACHENI FITINA, KUBAGUANA PENDANENI


Na Dinna Maningo, Mara

MENEJA wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo amewataka Waandishi wa Habari mkoa wa Mara kuacha chokochoko,majungu, ugomvi, uongo na fitina na badala yake wafanye kazi kwa umoja na kupendana.

Mihayo ameyasema hayo Juni, 13, 2023 wakati akitoa mafunzo kuhusu maadili ya uandishi wa habari na sheria ya huduma za habari kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Mara wanaowakilisha vyombo mbalimbali vya habari katika wilaya zilizopo mkoani humo.

Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandishi  Francis Mihayo akizungumza na Waandishi wa habari

Meneja huyo wa TCRA amesema kuwa Waandishi wa habari wa mkoa huo hawapendani na kwamba wasipopendana hawawezi kufika mbali huku akisisitiza kuwa hatosita kuwaambia ukweli.

"Waandishi wa habari wa Mara acheni chokochoko, acheni ugomvi, fitina, msipopendana hamtafika mbali. Mara Press klabu wanaongoza kwa majungu na kutopendana wakifatiwa na Kagera, hata Shinyanga niliwaambia ukweli sasa hivi wapo vizuri.

"Mimi kama Meneja nitasema ukweli inanitia huzuni mnapotengeneza utaratibu wa kuangalia sura za watu kujiunga kwenye klabu yenu, kwanini hamtaki kuwaingiza kwenye chama Waandishi wa habari wenzenu?.

"Ukienda Redio Mazingira fm wafanyakazi hawapendani na Bunda fm nao hawapendani na sijamaanisha Mara press tu ni waandishi wa habari wote mkoa wa Mara hampendani.

"Nawafahamu sana kwa jinsi msivyofikilia, nimekuja mkoa wa Mara kwa mara ya kwanza acheni majungu hamtafika mbali " amesema Mhandisi Mihayo.

Mihayo amesema kuwa waandishi wa habari watakaomchukia kisa kuwaambia ukweli yeye hatojali kwakuwa ana haki ya kuwashauri.


Amesema Waandishi wa habri na TCRA ni watoto wa baba mmoja wote wapo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hivyo hatoogopa kusema ukweli.

"Anayewaambia ukweli ni mtu mwema zaidi, mkinichukia kuwa nimekuja kuwashambulia ni juu yenu, sisi ni watoto wa baba mmoja tupo Wizara ya Habari, sitaki kuhukumiwa kisa eti nimeogopa kuwaambia ukweli " amesema Mhandisi Mihayo.

Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Mara, Pendo Mwakembe amemwomba Meneja huyo kutenga muda mwingine kujadili suala hilo kwani mjadala huo sio mahala pake na kile waandishi walichoitwa kujadili na kujifunza.


"Umeizungumzia Mara press klabu na hapa tupo mchanganyiko, Mara press klabu ina taratibu zake, katika vitu unavyozungumzia mimi kama kiongozi wa press nashauri unaweza kuwa na nia njema ya kutusaidia lakini ikaleta madhara mara mbili ukaondoka ukiwa umetugawa.

"Tupo majukwaa mawili tofauti waliopo kwenye chama na wasio wanachama, mimi nashauri tuje tukae kama Mara press tuzungumze haya.Nikitazama chombo chako kina dili na maudhui yetu ya habari na una uwezo wa kutushauru.

" Lakini hapa naona kama upo upande fulani. Utaratibu wa kujiunga kwenye chama awali ilikuwa unatuma maombi baada ya miezi mitatu unapitishwa sasa hivi ni mwezi mmoja na unapitishwa kupitia vikao vyetu, kila chama kina katiba yake" amesema Pendo.

Mwenyekiti wa Mara Press Klabu Raphael Okelo amemshukuru Meneja wa TCRA kuwaeleza ukweli na kusema kuwa chama kitaufanyia kazi ushauri wake huku akiwaomba Waandishi wa habari kujiunga na Mara Press klabu.

       Mwenyekiti wa Mara Press Klabu Raphael Okelo

"Tumepokea ushauri wako tutaufanyia kazi, niwaombe waandishi wa habari ambao hawapo kwenye kilabu wajiunge wasisikilize maneno wakiwa nje.

" Moja ya majukumu ya klabu ni kusimamia maadili ya uandishi wa habari, klabu haiwezi kuongoza watu ambao wanaweza kuharibu klabu. Juzi kati tuliweka fomu kwenye Magrupu wapo walioomba kujiunga na asilimia 80 walipitishwa.

Mwandishi wa habari mkongwe kwenye taaluma ya uandishi wa habari , Maximilian Ngesi  amesema TCRA ni mlezi wa Waandishi wa habari na Vyombo vya habari na kwamba kuwakosoa waandishi ni kuwasaidia kuwarekebisha ili kwenda vizuri.

"TCRA ana nafasi ya kutusaidia kutushauri na kutuelekeza, haya mambo yapo sio ya uongo lazima tukosolewe tusisubiri mpaka tukae kwenye vyama wote ni waandishi wa habari" amesema MacMillan.

Mwandishi wa Habari na mmiliki wa Musoma TV, Emmanuel Chibasa amesema kinachosababisha waandishi wa habari hawapendani ni ubinafsi na makundi.

     Mwandishi wa Habari na mmiliki wa Musoma TV, Emmanuel Chibasa

" Waandishi wengi wa habari tumekuwa na ubinafsi na tumekuwa hatupendi kuona maendeleo ya wenzetu lakini vile vile kuna makundi yanayoendeshwa na waandishi wa habari yanayopelekea taasisi za Serikali nazo kuwa na makundi na kubagua waandishi wa habari kufanya kazi za Serikali.

" Hali hiyo imesababisha waandishi wa habari kujiona ni bora kuliko wengine. Kuna waandishi wa habari wamejigeuza kuwa maafisa habari wa Serikali wameacha kufanya kazi za kijamii wamekuwa ni waandishi wa mialiko.

Emmanuel ameongeza kusema " Uandishi wa mialiko umekuwa ukileta migogoro, mwandishi asipopata mwaliko anamchukia mwandishi wa hilo kundi lingine lililopata mwaliko huko kwenye ziara za Serikali.

Amesema Waandishi wa habari wakiondoa ubinafsi na kuacha chuki zisizo na msingi na kutojiona bora kuliko wengine au kutojiona bora kwakuwa yupo kwenye chombo cha habari cha Serikali watafika mbali.

Ameongeza kuwa anayefanya kazi kwenye vyombo vya habari vya Serikali ni sawa na wengine wanaofanya kazi kwenye vyombo binafsi, hivyo waandishi wa habari wasibaguane kutokana na vyombo vyao vya habari hata kama ni vidogo.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mwanza Edwin Soko aliyetoa mafunzo kuhusu sheria mbalimbali ikiwemo ya huduma ya habari amesisitiza upendo.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mwanza Edwin Soko

" Waandishi wa habari ni watu tunaoishi kwenye madhira mengi silaha yetu ni moja kama tunapendana itatusaidia kufanya kazi zetu tukiwa salama lakini kama sisi tutashindwa kupendana basi inaleta hathari kubwa kwenye ufanyaji kazi.

Edwin amewashauri waandishi wa habari mkoa wa Mara kupendana hata kama kuna changamoto nyingi wakutane kuzijadili na kuzitatua ili kuzimaliza pamoja na kukiweka chama mbele kiwe ni sehemu ya kuwaunganisha wanachama ikiwa ni pamoja na kubuni mambo ambayo yanaweza kuwasaidia na chama kikasonga mbele.
 
Meneja wa TCRA mwenye mkoti wa bluu akiwa kwenye picha ya pamoja na Waandishi wa habari mkoa wa Mara 





No comments