HEADER AD

HEADER AD

DARAJA JIPYA BARABARA YA NYARWANA- MWARA FURAHA KWA WAFUGAJI, WAKULIMA


>>Limejengwa na mkandarasi mwanamke

>>Wafugaji, wakulima waishukuru Serikali

Na Dinna Maningo, Tarime

HATIMAYE hofu imekwisha iliyokuwa imetanda kwa wananchi wakiwemo wafugaji na wakulima waliokuwa wakipita kwenye daraja lililoharibika barabara ya Nyarwana -Mwara, Kata ya Kibasuka wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Ni baada ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga daraja jipya.

         Daraja jipya barabara ya Nyarwana-Mwara

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) ikatoa fedha kwa mkandarasi kiasi cha Tsh. Milioni 184.5 kujenga daraja katika Kitongoji cha Mwara Kijiji cha Nyarwana.

Meneja Wakala wa Barabara Mjini na vijijini Mhandisi Charles Marwa anasema ujenzi wa daraja hilo ulianza Machi, 25/2022 na kukamilika Mei, 29, 2023.

    Meneja Wakala wa Barabara Mjini na vijijini Mhandisi Charles Marwa

Anasema daraja hilo limejengwa na mkandarasi mwanamke UK Contraction and General Supply na kukamilisha kazi yake mapema.

" Mkandarasi amekamilisha kazi mapema kabla ya muda wa mkataba, mkataba wa ujenzi ni Milioni 184.5, umebaki muda wa matazamio wa mwaka mmoja ili kukiwa na changamoto anarudi kurekebisha.

" Ni box Karavati la midomo miwili la mita 11, box Karavati nguzo zake siyo nene kama za daraja ndiyo maana linawekewa nguzo katikati. 

"Usipoweka nguzo katikati kile kitanda chake ni rahisi kushuka kama magari makubwa yatapita pale ndiyo maana inawekwa nguzo ili liwe imara zaidi" anasema Mhandis Charles.

Anasema kwa sasa imebaki hatua ya ujenzi wa mitaro na kwamba ujenzi utaanza hivi karibuni.

Daraja mto Nyarukamu

"Imebaki kazi ya kuinua tuta pande zote mbili, baada ya kuinua tuta ndiyo tutajenga mitaro ya pembeni ya kulinda tuta na kuelekeza maji chini ya daraja.

" Kimsingi tumekwisha omba fedha na tumefanikiwa kupata pesa kwa ajili ya kufanya hiyo kazi kubwa na ujenzi wa kingo za daraja umeanza.
Ujenzi ukiendelea Kwenye kingo za daraja

Anaongeza kusema " Tuliamua wananchi waanze kupita watumie daraja wasihangaike kupita wakati daraja limekamilika " anasema Mhandisi Charles.

Wafugaji, wakulima wazungumza

Garani Chacha mkazi wa Kijiji cha Nyarwana ambaye ni mkulima na mfugaji ameishukuru TARURA kwa kusikia kilio chao cha daraja lililoharibika na ujenga daraja jipya.

                    Garani Chacha

" Tunaishukuru Serikali na TARURA kutujengea daraja jipya sasa hivi hatupati hofu kuvuka daraja, lililokuwepo liliharibika gari na pikipiki zilishindwa kupita lakini baada ya ujenzi zinapita bila wasiwasi" anasema Garani.

Ester Jastine mkazi wa Kitongoji cha Mwara anasema kuwa wakati wa msimu wa mvua wakulima walipata shida kuvusha mazao yao.

                 Ester Jastine

Anasema walishindwa kutumia usafiri wa pikipiki na gari kusafirisha mazao yao kutokana na ubovu wa daraja lililokuwa limeharibika na kusababisha wakulima kuingiwa hofu na kuogopa kupita darajani.

Anasema kuharibika kwa daraja kulisababisha wavuke mto Nyarukamu kwa kutembea kwa miguu ndani ya maji wakiwa  wamejitwisha mazao kwenda kuuza mnada wa Nyarwana kitendo ambacho kilikuwa kero kwao.

            Daraja la zamani lililobomoka

" Tunaishukuru Serikali kutujengea daraja jipya, sasa hivi wakulima tunavusha mazao yetu bila hofu kwakuwa usalama wa daraja upo baada ya kuondolewa daraja bovu na kujengwa jipya.

"Tulilazimika kuvuka mto kwa miguu tukiwa na mazao yetu tumejitwisha  vichwani, mto ulipojaa tulisubiri kwa saa kadhaa maji yapungue ndipo tuvuke "anasema Ester.

Mgesi Chacha anasema daraja la zamani lilisababisha kero kwa wachungaji wa mifugo kwakuwa walishindwa kuvuka mto msimu wa mvua kupeleka mifugo malishoni na mnadani.

               Mgesi Chacha

"Sasa hivi iwe mvua au jua mifugo inavuka bila shida, wachungaji wa mifugo tunapita bila wasiwasi kwasababu daraja limejengwa jipya na zuri, ule usumbufu tuliopata kuvuka daraja la zamani umeisha" anasema Mgesi.

Neema Marwa anasema kabla ya daraja jipya kujengwa wananchi na wanafunzi walipata shida kuvuka mto.

                     Neema Marwa

" Tulipata shida sana kuvuka mto hasa wanafunzi maji yalipokuwa mengi walishindwa kwenda shule, wazazi walilazimika kuwavusha wanafunzi ili waende shule.

"Tunashukuru kujengwa kwa hili daraja wanafunzi wanapita bila shida wala hofu. Changamoto iliyobaki ni barabara inayopita hapa karibu na daraja ni bovu iliharibiwa na mvua, wakati wa mvua tope zinakuwa nyingi tunapata tabu kupita " anasema Neema.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwara Masero Marwa Mnanka anasema TARURA wamejitahidi kujenga daraja zuri kuliko lililokuwepo awali.

     Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwara Masero Marwa Mnanka

" Tunaishukuru Serikali kutuondolea adha na kutujengea daraja jipya, tunaomba ijenge mitaro ya kukusanya maji kwenda mtoni ili barabara isiharibike, " anasema Mwenyekiti.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyarwana Naftari Mgesi anasema kabla ya daraja hilo kujengwa wananchi wake wakiwemo wafugaji walipata shida kuvuka mto.

   Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyarwana Naftari Mgesi

"Daraja la zamani lilileta hofu kwakuwa walikuwa wanalitumia huku likiwa limezeeka na kuharibika, gari na pikipiki hazikuweza kupita, wakati wa mvua watu walipata shida kuvuka walilazimika kupita majini, maji yalipokuwa mengi hawakuweza kuvuka.

Anaongeza" Tunaomba Serikali itujengee daraja lingine mto Tigite unaotenganisha Kata yetu na Kata ya Matongo- Nyamongo, wananchi wanateseka wanapokwenda Nyamongo kuuza mazao na mifugo.

" Daraja likijengwa mto Tigite litasaidia sana watu wanavuka mto kwa miguu kupeleka mifugo ba bidhaa zingine kuuza mnadani Nyamongo, maji yakiwa mengi huvuka kwenye daraja la miti lililojengwana mwananchi kwa gharama Tsh. 1000 na watoto Tsh. 500" anasema Mwenyekiti.

Bajeti ya fedha Tarime DC

Meneja huyo wa TARURA anasema katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha ikaidhinisha Bajeti ya Matengenezo ya Barabara kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) kiasi cha fedha Tsh.Bilioni 2.209 kutengeneza barabara zilizopo  Halmashauri ya wilaya ya Tarime.

        Daraja lililopo barabaraya Nyarwana- Mwara

Mhandisi Charles Marwa anasema vyanzo vya fedha ni tozo ya mafuta ambayo ni ongezeko la bajeti  Sh. 100 kwa kila lita ya Dizeli na Petroli kiasi cha Tsh Bilioni moja.

Fedha ya Jimbo la uchaguzi Tsh. Milioni 500 na fedha kutoka mfuko wa barabara Tsh. Bilioni 1.27. Hadi kufikia mwezi Machi, 2023 TARURA imepokea Tsh.Bilioni 1.265 sawa na asilimia 50 zilizotekeleza miradi mbalimbali ambapo matengenezo yamefikia asilimia 80.

Mhandisi Charles anasema kuwa baadhi ya barabara zilikuwa ni chagamoto kwa wananchi kutokana na kutokuwa na vivuko na hivyo kuwa kero kwa wananchi wakati wapitapo kwenda katika shughuli zao.

Anasema  kupitia bajeti hiyo ya 2022/2023, TARURA imewaondolea adha wananchi kwani imefanikiwa kujenga Vivuko 42 kwa baadhi ya Vijiji katika halmashauri hiyo na pesa zikipatikana yatajengwa madaraja na makaravati mengine kwani lengo la Serikali ni kuimarisha miundombinu ya barabara ili kuondoa adha kwa wananchi.

         Wanafunzi wa darasa la awali wakipita darajani




                  Mto Nyarukamu




No comments