MKAGUZI AVUTIWA NA UBUNIFU WA VYANZO VYA MAPATO BIHARAMULO
>>Asema vyanzo vingi vya mapato vinaisaidia Halmashauri kutekeleza miradi
>>Aipongeza Biharamulo kupata hati safi
>>Awasisitiza Madiwani kuwasimamia Watendaji
Daniel Limbe, Biharamulo
MKAGUZI Mkuu wa nje wa Hesabu za Serikali mkoani Kagera, Godwin Ibrahim (CEA), ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani humo kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo akilinganisha na hali iliyokuwepo awali kwenye wilaya hiyo.
Mbali na pongezi hizo,ameonyesha kulidhishwa na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato kwenye halmashauri hiyo lengo likiwa ni kuhakikisha inatimiza azma ya Serikali ya kila halmashauri nchini kujitegemea kwa aslimia 25 kupitia makusanyo ya vyanzo vya ndani.
Mkaguzi mkuu wa nje wa hesabu za serikali mkoani Kagera,Godwin Ibrahim,akitoa ushauri kwa madiwani na wakuu wa idara za halmashauri ya wilaya ya Biharamulo
Imeelezwa kuwa kujitegemea kwa vyanzo vya ndani vya mapato, itasaidia halmashauri kutekeleza miradi mingi ya maendeleo badala ya kungoja fedha kutoka Serikali kuu.
Akitoa salaamu za mkuu wa mkoa wa Kagera,kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani wa Biharamulo kilichoketi kujadili hoja za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali nchini (GAG) za mwaka 2021/22, Katibu tawala wa mkoa huo,Toba Nguvila,amesema ili kufikia malengo yanayokusudiwa na Serikali, Madiwani wa halmashauri hiyo hawana budi kuwa wakali.
Katibu tawala mkoa wa Kagera,Toba Nguvila,akitoa salaam kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa kagera
"Madiwani mnalo jukumu kubwa sana la kuwasimamia watendaji wenu na iwapo mtawabaini hawatende haki chukueni hatua ilimradi msimwonee mtu, kuweni wakali pale mnapobaini mambo hayaendi, hii itawasaidia sana kwenye uchaguzi ujao maana itakuwa kama mnamsukuma mlevi kwenye mtelemko" amesema Nguvila.
Amesema zipo taarifa za baadhi ya watumishi waliotafuna fedha za michango ya wananchi na bado hatua za kisheria hazijachukuliwa.
Ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) kufanya uchunguzi wa haraka ili itakapo thibitika wahusika wachukuliwe hatua za haraka.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu ameahidi kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo kati ya madiwani na watumishi kwa lengo la kuhakikisha wilaya hiyo inaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo ikiwa ni pamoja na kusimamia vyema fedha za umma.
Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Innocent Mukandala, amesema atayafanyia kazi maoni na ushauri wote uliotolewa na ofisi ya mkuu wa mkoa, mkaguzi mkuu wa nje pamoja na baraza la madiwani, huku akiahidi ufanisi mkubwa wa kazi kwa watumishi wa halmashauri hiyo.
Post a Comment