Home
/
Barabara
/
DARAJA LAWAPUNGUZIA MZUNGUKO, GHARAMA ZA USAFIRI WATUMIA BARABARA SORONETA - NYAKONGA
DARAJA LAWAPUNGUZIA MZUNGUKO, GHARAMA ZA USAFIRI WATUMIA BARABARA SORONETA - NYAKONGA
>>Msimu wa mvua wanakijiji walistisha safari, wengine walilala njaa
>> Mto ulisababisha wanafunzi kutoenda shule, vifo
>>Furaha zatawala baada ya Serikali kusikia kilio cha wanakijiji na kujenga Daraja la Milioni 511
>>Kabla Daraja kujengwa walizunguka umbali mrefu kwa pikipiki nauli Tsh. 8000-15000
>> Baada ya Daraja kujengwa usafiri wa pikipiki ni Tsh.1000- 2000
Na Dinna Maningo, Tarime
NI majira ya saa tatu asubuhi nawasili stend ya Rebu iliyopo Halamashauri ya mji Tarime mkoani Mara.
Naingia ndani ya gari ili kuianza safari, dakika kadhaa zinapita dereva anawasha gari nakuianza safari kuelekea Kijiji cha Kemakorere, Kata ya Nyarero katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime.
Tunasafiri kwa dakika kadhaa kufika senta ya Kemakorere, dereva anasimamisha gari nami nashuka, pembeni ya barabara nawaona waendesha pikipiki wakiwa katika kituo chao cha maegesho.
Nazungumza na dereva mmoja kisha namuomba anipeleke kulikojengwa daraja barabara ya Soroneta- Nyakonga lililojengwa mpakani mwa Kijiji cha Soroneta kata ya Nyarero na Kijiji cha Kebweye Kata ya Nyakonga.
Ananiambia gharama kisha nalipa tunaianza safari kuelekea darajani.
Tunafika salama hadi mtoni kulikojengwa daraja, nashuka na kulitazama daraja kila upande.
Daraja
Nikiwa katika daraja hilo punde si punde anapita mwananchi mmoja akitokea Kijiji cha Soroneta. Namsimamisha kisha tunasalimiana na kujitambulisha kwakwe.
Lengo la kumsimamisha ni kutaka kufahamu je kabla ya daraja kujengwa wananchi walikabiliwa na changamoto gani wakati wa kuvuka mto?.
Je wanasemaje baada ya Serikali kujenga daraja katika mto ambao ulikuwa mateso kwao?.
Wambura Mwita mkazi wa Kijiji cha Kebweye anasema kabla daraja halijajengwa wakati wa msimu wa mvua wananchi walipata shida kuvuka mto kwakuwa ulijaa maji mengi.
" Tulipata shida sana msimu wa mvua, tulishindwa kuvuka ng'ambo ya mto kwenda kulima mashamba yetu, tulishindwa kupeleka mifugo malishoni. Wanafunzi walikaa utoro, maji yalipopungua wazazi walilazimika kuacha shughuli zao na kwenda kukaa mtoni kusubiri kuwavusha watoto.
" Kabla ya daraja kujengwa ili uvuke mto ilikubidi upandishe juu nguo zako ili zisilowane. Tulipata tabu kuvusha mazao, tulijitwisha mahindi vichwani na mazao mengine huku tukivuka maji" anasema Wambura.
Wambura anaongeza kusema" Wakati wa mvua wananchi wa Soroneta walishindwa kuvuka mto kwenda kupata huduma za afya Kijiji jirani katika Zahanati ya Kebweye.
Anasema miaka iliyopita kabla ya kujengwa kituo cha afya Magoma katika Kijiji jirani wananchi walisafiri kwa gari kwenda kupata huduma ya afya Tarime mjini.
Wengine walisafiri kwa pikipiki kwenda kupata huduma ya afya Kituo cha afya Magoto huku gharama za usafiri wakigharamika kati ya Tsh 8,000- 15,000.
Nikiwa darajani namuona mwananchi mmoja akiwa shambani nasogea kisha tunazungumza, anajitambulisha kwa jina la Peter Kitegi mkazi wa Kebweye.
Peter anasema msimu wa mvua wananchi walipata karaha, baadhi ya watu walisombwa na maji wengine waliokolewa na wengine walikufa wakati wakijaribu kuvuka mto.
"Mto ulisababisha majanga watu walisombwa na maji, watu walikufa wakivuka mto, mimi mwenyewe nilimshuhudia mzee Marwa Magige alikufa akivuka mto, tukamfuatilia lakini tulikuta ameshakufa, na watoto wengine wanne walikufa wakivuka mto.
" Mifugo imekufa mingi, mfano kama ya Semse Magweiga ng'ombe wanne walikufa na ng'ombe wawili wa Rhobi Kusula. Maji yalikuwa yanajaa siku mbili au tatu" anasema Peter.
Peter anasema "Baada ya daraja kujengwa sasa hivi hatuhofii usalama wa maisha yetu, tunatembea hata usiku bila shida tukijua kuna uhakika wa kuvuka mto.
Hakika tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kutuona. Tunawapongeza TARURA kutujengea daraja zuri, tunampongeza na mzabuni kwakweli kafanya kazi kubwa" anasema.
Wanawake wampongeza Rais Samia, wasema wanawake wanaweza kuongoza
Baadhi ya jamii huamini kuwa wanawake hawawezi kuongoza hasa nafasi za juu za uongozi wakiamini wanaoweza ni wanaume.
Imani hiyo imepingwa na wanawake wanaoishi jirani na mto kwa kile walichoeleza kuwa katika uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiyo daraja limejengwa wanapita juu ya daraja na sio ndani ya maji.
Natembea hatua chache kutoka kuliko na daraja hadi eneo la mto ambao wananchi wanalitumia kufua nguo, kuoga na kuchota maji. Flora Zakaria mkazi wa Kitongoji cha Nkukuhesahe anaeleza furaha yake baada ya daraja kujengwa.
" Wanaume wajue kuwa sisi wanawake tuna uwezo mkubwa sana tukipata nafasi, sisi ndiyo tunahakikisha mme kala, watoto wamekula, nguo zimefuliwa na kutekeleza majukumu mengine.
" Kwa kuwa wanawake ni nguzo kubwa katika Taifa na katika kuthibitisha hilo kuwa wanawake wanaweza ni huu ujenzi wa daraja kubwa, limejengwa wakati wa uongozi wa Rais Samia licha ya nchi hiyo kuongozwa na Marais wanaume kwa miaka mingi.
Flora anasema kabla ya daraja kujengwa walikuwa wanapata shida kwenda kusaga na kununua mahitaji mengine na wakati mwingine badhi ya wananchi walilala njaa.
"Sisi wananchi wa Kijiji cha Soroneta tunaoishi jirani na mto mahitaji yote tunaenda kununua Kijiji jirani cha Kebweye ambacho kipo ng'ambo ya mto, huko ndiyo kuna maduka na mshine ya kusaga unga.
" Maji yakijaa tunashindwa kupika tunalala njaa maana hutoweza kuvuka kwenda kusaga au kununua kibiriti uwashe moto, kama unavyoona huku ni kijijini nyumba zipo mblimbli. Unamtuma mtoto dukani mvua ikimkuta inabidi aombe hifadhi alale mpaka maji yatakapopungua uende kumvusha.
Flora anazidi kueleza kuwa wanawake walipata shida hususani wajawazito kwani walilazimika kwenda kupata huduma ya afya Tarime mjini badala ya kuipata Zahanati iliyopo Kijiji jirani.
"Zahanati ipo ng'ambo unatembea kwa miguu dakika chache umefika lakini tulishindwa ilibidi mtu aende kliniki Tarime mjini unapanda gari nauli sh.4,000 kwenda na kurudi bado usafiri wa pikipiki 3,000 kwenda nyumbani kwako.
" Tunampongeza sana Rais Samia kwa kazi kubwa ya maendeleo, tunaomba aendelee kulishangaza taifa na kutuheshimisha wanawake watanzania kuwa nao wanaweza, asirudi nyuma achape kazi, asikubali kukatishwa tamaa na sisi tutamuunga mkono kwa nguvu zote " anasema.
Winfrida anayeishi jirani na mto anasema ujenzi wa daraja umepunguza gharama za nauli lakini pia kupata muda wa kuwajibika katika shughuli zao.
",ili uende Magoto ulilazimika kutembea mwendo mrefu kwenda Soroneta senta unapanda pikipiki unapita Rosana hadi Kemakorere unalipa sh. 10,000 unalipa nauli nyingine Tsh 5,000 kwenda Kituo cha afya Magoto.
" Daraja limetusaidia tumeokoa pesa nyingi kutoka nauli ya Tsh15,000 kwenda Magoto sasa tunalipa nauli sh 4,000 kwenda na kurudi tumeokoa Tsh. 11,000. Tunaishukuru Serikali wajawazito walipata shida kujifungua mpaka upite Kemakorere sasa hivi unakatisha hapa darajani unafika haraka" anasema Winifrida.
Nazipiga hatua kadhaa kuelekea Senta ya Kebweye nauona mji nje kukiwa na watu huku mama mmoja akichochea kuni jikoni. Nasogea na kuzungumza nae.
Selina Waitara mwanakijiji cha Kebweye anasema kwa sasa wanawake hawahangaiki kwenda shambani kwakuwa daraja limejengwa wanavuka salama.
Selina Waitara
" Wakati wa masika wakulima tulipata shida kwenda kwenye mashamba yaliyopo ng'ambo ya mto Kijiji cha Soroneta, tulikaa siku tatu bila kwenda shambani" anasema Selina.
Wanafunzi waipongeza Serikali kujenga daraja
Pendo Joseph mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Kebweye anasema walishindwa kwenda shule baada ya mto kujaa maji.
Kulia ni Pendo Joseph na Janeth Mwita
" Mvua iliponyesha kubwa hatukwenda shule tulikaa utoro, tulikosa vipindi darasani, tulikaa siku tatu hata wiki msimu wa mvua kwasababu ya maji mengi kujaa mtoni tukashindwa kuvuka" anasema.
Janeth Mwita mwanafunzi wa darasa la nne katika shule hiyo anasema" Kipindi cha mitihani wazazi walituvusha, naishukuru Serikali kutujengea daraja, sasa hivi hatukai utoro kwa sababu ya mto tunavuka bila tatizo" anasema Janeth.
Zakaria Mwita mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Kebweye anasema wanafunzi wanaotoka ng'ambo ya mto hawakuweza kupita hivyo kiwango cha taaluma kilishuka kwa baadhi ya wanafunzi kutokana na kutohudhuria vipindi darasani.
Zakaria Mwita
Anasema kwa sasa utoro umepungua shuleni kwakuwa hakuna adha tena na kwamba akilitizama kwa macho daraja anaona limejengwa vizuri na lina vutia.
Paulina Nchama Mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Magoto anasema" Namshukuru Rais Samia kwa ujenzi wa daraja, pale mto ulipojaa maji nilishindwa kwenda kumsalimia shangazi yangu Kijiji cha Magoma.
Paulina Nchama
Agnes Chacha mkazi wa Kebweye anaishukuru Serikali na Rais Samia" Tunaishukuru Serikali kwasababu mvua iliponyesha tuliteseka sana, tunampongeza Rais Samia Mungu ampe nguvu, hakika wanawake tunaweza" anasema Agnes.
Agnes Chacha
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakonga John Magogo anasema mto ulipojaa maji wananchi wake waliokuwa wanasafiri kwenda kiiji cha Soroneta walilazimika kusubiri kwa saa kadhaa ili maji yapungue wavuke mto.
Anasema wengine walihairisha safari huku wenye haraka wakizugukia Kemakorere hadi Soroneta kwa gharama ya tsh.8,000-15,000 kwa usafiri wa pikipiki.
Anasema bada ya daraja kujengwa watu wanapita karibu wanatumia nauli sh. 2,000 kwa pikipiki huku wasio na nauli wakitembea kwa miguu muda wa dakika 35 kufika Soroneta.
Barabara ya Soroneta-Nyakonga
Mwenyekiti wa Kijiji cha Soroneta Weroma Robart anaipongeza serikali kuboresha miundombinu ya barabara na ujenzi wa Daraja.
" Kabla ya barabara na daraja kujengwa ili uende Magoto mpaka uvuke mto kwa miguu, usafiri wa pikipiki ilikuwa Tsh. 3000, ila baada ya daraja kujengwa kwenda Magoto ni sh. 1000-1500.
Awali kabla ya barabara na daraja kujengwa maji yakijaa ili ufike Magoto ulikuwa unazunguka unapita Rosana- Kemakorere hadi Magoto unaenda kwa sh. 8000 hadi 15,000 ila baada ya barabara ya Kemakorere kutengenezwa kwenda Magoto ni sh.4,000.
Mwenyekiti huyo anaongeza" Naishukuru TARURA kwakweli wanafanya kazi kubwa, baada ya kuboresha miundombinu ya barabara wananchi wanaenda kupata huduma ya afya Kijiji jirani cha Magoma mwendo wa nusu saa au nauli sh. 500 hawasumbuki hawaendi Kituo cha Afya Magoto, barabara ni mseleleko.
" Sasa hivi kuna daraja kubwa linajengwa Soroneta- Pemba likikamilika magari ya kutoka Nyamongo, Serengeti, yatakuwa yanapita Rosana -Soroneta yanaenda Pemba hadi Sirari tofauti na sasa mpaka yaende Nyamwigura - Magoma kwenda Sirari.
Peter Kitegi anasema changamoto iliyopo ni mitaro katika barabara ya Soroneta- Kebweye hivyo anaiomba Serikali kujenga mitaro ya kukusanya maji ili miundombinu ya barabara isiharibike.
Katika kuondoa kero za madaraja, barabara, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais mwanamke Dkt. Samia Suluhu imerejesha furaha kwa wanakijiji kwa kujenga daraja lililogharimu Tsh. Milioni 511 lililokamilika na linatumika.
Meneja TARURA aeleza
Meneja Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini wilaya ya Tarime, Mhandisi Charles Marwa anasema ujenzi wa daraja hilo umegharimu Tsh. Milioni 511.
Meneja Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini wilaya ya Tarime, Mhandisi Charles Marwa.
" Daraja lilianza kujengwa Januari 2022 na kukamilika Oktoba 2022. Mitaro ya maji ya mvua ilichimbwa mingi ila ya kujenga ndo haikufanyika kipindi hicho, tumejipanga katika bajeti zijazo" anasema Mhandisi Marwa.
Anasema katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha ikaidhinisha Bajeti ya Matengenezo ya Barabara kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime, Tsh.Bilioni 2.209 kutengeneza barabara zilizopo Halmashauri ya wilaya ya Tarime.
Mhandisi Charles Marwa anasema vyanzo hivyo ni tozo ya mafuta ambayo ni ongezeko la bajeti Sh. 100 kwa kila lita ya Dizeli na Petroli kiasi cha Tsh Bilioni moja.
Fedha ya Jimbo la uchaguzi Tsh. Milioni 500 na fedha kutoka mfuko wa barabara Tsh. Bilioni 1.27. Hadi kufikia mwezi Machi, 2023 TARURA imepokea Tsh.Bilioni 1.265 sawa na asilimia 50 zilizotekeleza miradi mbalimbali ambapo matengenezo yamefikia asilimia 80.
Mhandisi Charles anasema kuwa baadhi ya barabara zilikuwa ni chagamoto kwa wananchi kutokana na kutokuwa na vivuko na hivyo kuwa kero kwa wananchi wakati wapitapo kwenda katika shughuli zao.
Anasema kupitia bajeti hiyo ya 2022/2023, TARURA imewaondolea adha wananchi kwani imefanikiwa kujenga Vivuko 42 kwa baadhi ya Vijiji katika Halmashauri hiyo na pesa zikipatikana yatajengwa madaraja na makaravati kwani lengo la Serikali ni kuimarisha miundombinu ya barabara ili kuondoa adha kwa wananchi.
Post a Comment