HEADER AD

HEADER AD

DARAJA NKONGORE MATUMAINI MAPYA KWA WATUMIA BARABARA, WANANDOA


>> Wananchi wasema kutokuwepo daraja kulisababisha wakose huduma ya ndoa

>>Kabla ya daraja kujengwa walilazimika kuvua viatu na soksi ili kuvuka mto

>>Watu walivuka daraja la miti kwa sh 500-1000

Na Dinna Maningo, Tarime

TENDO la ndoa ni muhimu katika maisha ya wanandoa, lakini pale linapogubikwa na karaha hugeuka kuwa shubiri na huzuni kwa wanandoa.

Wananchi wakiwemo wanaoishi jirani na mto Mori Kata ya Kitare na Nkende, wilaya ya Tarime mkoani Mara, kwa miaka kadhaa wamekuwa wakikabiliwa na adha msimu wa mvua, kwakuwa mto hufurika maji na kusababisha watumia barabara kushindwa kuvuka mto.

Hali hiyo ikasababisha kero kwa wanandoa wakiwemo wanaoishi kando kando ya mto kwakuwa msimu wa mvua walishindwa kupata haki ya tendo la ndoa baada ya kuwahifadhi wananchi walioshindwa kuvuka mto.

Peter Matiko maarufu kwa jina la madaraja mkazi wa mtaa wa Kumturu kata ya Nkende anayeishi jirani na mto huo, alijitolea kujenga daraja la miti na kuwavusha watu walioshindwa kuvuka huku wengine wakilazimika kulala katika nyumba yake pindi mto ulipofurika maji.

 Peter Matiko maarufu kwa jina la madaraja 

Peter anasimulia namna ukosefu wa daraja ulivyowapa mateso wanandoa na furaha yao baada ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga daraja.

" Tunaishukuru Serikali na TARURA kutujengea daraja sasa hivi ndoa zetu zina raha tunapata huduma bila karaha kwasababu wakati wa msimu wa mvua maji yalikuwa yanajaa watu wanashindwa kuvuka, ilipofika usiku ilibidi tuwape hifadhi kwenye nyumba zetu.

Daraja la Nkongore

"Hali hiyo ilitukosesha sana raha ya ndoa. Unakuta nyumba yako ina vyumba viwili mvua ikinyesha watu wanashindwa kuvuka inabidi uwalaze ndani kwako na wanakuwa ni jinsia mbili tofauti.

"Kwakuwa nyumba yako ni ndogo wewe mwanaume utalala chumba kimoja na wanaume wenzako na mke wako itabidi alale na jinsia yake ya kike, siku hiyo hamtashiriki tendo la ndoa.

Mwananchi huyo anaongeza kusema" Tulitoa msaada lakini tulipata karaha wanandoa tunaoishi jirani na mto hatukuweza kukataa, utawakatalia watu waende wapi na maji yamejaa mtoni.

"Tangu daraja lijengwe sasa hivi wanandoa tunapata raha wakati wowote tunajitimizia haki ya ndoa bila bugudha kwakuwa watu wanapita darajani iwe wakati wa mvua au jua. Ile kero ya kukosa tendo la ndoa wakati wa msimu wa mvua haipo tena" anasema Peter.

Peter anasema kuwa mbali na hilo alishindwa kufanya shughuli zake na badala yake kuwavusha watu na alilazimika kujenga daraja la miti ili watu waweze kuvuka lakini mvua zilipozidi daraja lililosombwa na maji.




"Tunashukuru daraja limejengwa. Pia barabara haikuwepo kulikuwa na njia ya kutembea kwa miguu, sasa babaraba imejengwa. Tulikuwa tunatumia daraja la miti ambalo nililitengeneza mimi.

"Mvua iliponyesha nyingi watu walishindwa kuvuka mto, wanafunzi wanaosoma shule ya msingi Ntaburo na Sekondari Nkongore ambazo zipo Kata ya Kitare waliteseka sana, wengine niliwavusha kwa kuwashika mkono na wengine kuwabeba mgongoni na mabegani.

" Wanafunzi walikaa siku tatu na hata wiki bila kwenda shule, kwasababu hata daraja nililotengeneza mvua iliponyesha lilisombwa na maji.

Anaongeza kuwa mto ulisababisha maafa" Nikiwa sipo iliwabidi wakatishe safari warudi nyumbani hasa msimu wa mvua wa mwezi wa nne na wa 12. Mazao yalisombwa na maji, mifugo ilikufa nakumbuka ng'ombe 6 zilisombwa na maji, watu walikufa wakati wakijaribu kuvuka mto.

Mto Mori

"Tunashukuru Mungu daraja limejengwa linatusaidia, sasa hivi tunavaa viatu na soksi, iliponyesha mvua watu walivua viatu na soksi na kuzishikilia ili kuvuka mto, ulikuwa unakunja suruali juu unavuka.

Anasema daraja alilolijenga kwa miti lilidumu kwa muda tu ambalo liliwasaidia waendesha pikipiki na abiria lakini maji yalipokuwa mengi lilisombwa na maji.

" Msimu wa mvua nilikuwa nahamasisha Mwenyekiti wa mtaa wa ng'ambo hii na wa ng'ambo ile wananinunulia misumari miti nilikuwa nayo nilikuwa nalitengeneza mwenyewe kivuko, mwenye kujisikia kulipa alilipa sh. 200, wengine 500 kwakuwa waliona nawasaidia.

Je  kujengwa kwa daraja kumeondoa kipato cha Peter cha kuwavusha watu na daraja la miti ambalo lilimwezesha kupata fedha msimu wa mvua? Peter anasema;

"Mimi sioni kujengwa daraja kumenipunguzia ulaji bali kumeniongezea maarifa, muda ambao nilikuwa natumia kuvusha watu sasa hivi nautumia kufanya shughuli za kilimo hakuna hofu, amani imetawala" anasema Peter.

William Matiko mkazi wa mtaa wa Butirya Kata ya Kitare anasema maji yalipojaa mtoni hawakuweza kupita kuvuka mto na kwamba baadhi ya watu walisombwa na maji na wengine kupoteza maisha. 
William Matiko

"Mwaka 2020 Chacha Girimwa Ndege  alifariki wakati anavuka mto akienda ng'ambo kwenye harusi, James Kitenga mtu mzima naye alikufa akivuka mto wakati anaenda kwenye harusi" 

"Kabla daraja alijajengwa wakulima wenye mashamba ng'ambo ya mto walipata shida, hata sisi wenye mashamba Magena tulipata shida kuvuka mto.

"Mvua ikinyesha unalala ng'ambo au unazungukia romoli unatokezea shule ya msingi Nyamwino mwendo wa masaa manne, yaani unapaona kwenu ni pale lakini huwezi kuvuka inabidi uzunguke mbali" anasema William.

Anasema daraja hilo lilianza kujengwa mwaka jana mwezi wa tatu na ujenzi umekamilika mwezi wa tatu mwaka huu wa 2023.

Rhobi Marwa Msaire mtumiaji wa barabara akiwa shambani akikata vijiti vya mihogo ili kupanda kwenye shamba anasema daraja jipya limekuwa mkombozi kwakuwa limewaondolea adha.

Rhobi Marwa Msaire

Anaishukuru Serikali kwa kuwaondolea kero na sasa wanapita darajani kwa pikipiki bila shida ikilinganishwa na awali pikipiki zilipita kwa shida daraja la miti na kwamba kujengwa daraja kumewezesha magari kupita.

"Msimu wa mvua tulipita kwenye daraja la mabanzi unalipa sh. 500 kwenda na kurudi sh.500 hadi maji yatakapopungua ndio.tunapita ndani ya maji na mvua ikinyesha nyingi linasombwa na maji hupiti unahairisha safari" anasema Rhobi.

Tarame Chacha mkazi wa mtaa wa Kumturu anaongeza kusema" Kabla daraja kujengwa kulikuwa na shida, sehemu ya kuvuka ilikuwa haipo unasubiri masaa manne maji yapungue uvuke.

Tarame Chacha

" Sasa hivi natembea kwa raha hata mvua ikinyesha kiasi gani napita kwa muda wowote kwakuwa daraja lipo.

"Changamoto iliyopo ni hii barabara hapa karibu na daraja ni mbovu tunaomba iwekewe moramu yakutosha, kwingine barabara ni nzuri.  

"Tunaishukuru sana Serikali na TARURA kutuondolea shida ya kivuko na barabara vilivyotutesa kwa miaka mingi " anasema Tarame.

Peter anashauri mitaro ijengwe kwa saruji ili kulinda daraja na barabara na kwamba nyasi zilizooteshwa pembeni ya daraja haziwezi kuzuia mmomonyoko wa udongo, kwakuwa mvua ikinyesha kubwa maji hujaa mtoni hivyo yatasomba nyasi hizo zilizooteshwa kando kando ya mto karibu na daraja.

 Daraja

Mwenyekiti wa mtaa wa Kumturu Juma Kisiri anaishukuru Serikali kuwajengea daraja na kuondoa adha kwa wananchi.

"Wananchi na wanafunzi walipata shida kuvuka mto, wananchi wawili wa mtaa wangu walikufa wakati wakivuka mto,sasa hivi daraja lipo wanapita kwa raha. 

"Changamoto iliyopo ni barabara ukishavuka daraja kwa mbele kidogo barabara ni mbovu, moramu waliyoweka sio ya kiwango, magari yanayosomba mchanga yakipita kunakuwa na mashimo.

Barabara 

"Tunaomba TARURA itukumbuke kwenye barabara za mtaa, mtaa wangu ni mkubwa lakini hauna barabara za mtaa zaidi ya barabara kuu, tukipata barabara za mtaa itapendeza sana" anasema Mwenyekiti wa mtaa.

Mwenyekiti wa mtaa wa Butirya Jastine Maendeleo anaipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Samia kwani wananchi wake walipata shida katika shughuli zao za biashara na wengine kushindwa kupata haki ya ndoa.




"Tunamshukuru sana Rais Samia kutoa fedha kujenga daraja, wananchi waliokuwa wanapeleka biashara zao mjini walishindwa kuvuka mto wakati wa masika, maji yalipojaa watu walilala ng'ambo wakashindwa kwenda kuhudumia ndoa zao, wababa walishindwa kupikiwa chakula.

" Mto ulisababisha wazazi kushindwa kwenda kulala kwenye familia zao walishindwa kuvuka mto. Wakati mwingine unaondoka nyumbani hakuna mvua huna taarifa unarudi maji yamejaa kutokana na mvua kunyesha maeneo mengine" anasema Mwenyekiti.

Anaongeza " Changamoto iliyopo ni barabara kutokea ramini hadi darajani ni nyembamba inaleta usumbufu kwa watembea kwa miguu, gari na pikipiki.

Barabara

"Hata moramu iliyowekwa haina ubora ni udongo inatusumbua lakini huku kwingine barabara ni nzuri, japo imeleta unafuu maana watu wanapita wanapeleka biashara zao na vyombo vya moto vinapita, tunaomba tu iboreshwe " anasema Jastine.

Meneja TARURA

Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa anasema ujenzi wa daraja barabara ya Nkongore- Kumturu umegharimu Tsh. 684,257,112, ulianza tarehe 25,03, 2022 na kukamilika awamu ya kwanza tarehe 05, 03, 2023.

        Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa

"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuendelea kuipatia TARURA fedha kujenga miundombinu ya barabara, sasa wananchi wa Nkongore wanapita bila shida. Kilichobaki ni kujenga mitaro katika mwaka wa fedha 2023/2024 na kwamba barabara bado ipo Kwenye hatua ya matengenezo" anasema Mhandisi Charles.

Anasema katika uongozi wa Rais Samia miundombinu mbinu ya barabara inazidi kuboreshaa na kwamba Halmashauri ya Mji Tarime katika mwaka wa fedha 2022/2023 ilitengewa bajeti ya matengenezo ya barabara Tsh. Bilioni 2.209.

Anasema bajeti hiyo ni ongezeko la zaidi ya mara tatu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha Tsh. Milioni 729  hali ambayo imesaidia kuwapunguzia wananchi kero za barabara.

Daraja Nkongore

" Utaona bajeti hiyo ni zaidi ya mara tatu ya Tsh Milioni 729 ya mwaka wa fedha 2020/2021. Dhamira ya Rais Dkt Samia ni kuhakikisha kero za barabara zinatatuliwa lakini pia kuhakikisha kila mwananchi anaweza kutoka nyumbani kwakwe na kwenda sehemu za uzalishaji mali na huduma za jamii bila shida" anasema Meneja TARURA.

Anasema bajeti hiyo ya matengeneze ya barabara ni kutoka katika vyanzo vitatu ambavyo ni fedha ya tozo ya mafuta ambayo ni ongezeko la bajeti ambayo ni makato ya Tsh. 100 kwa kila lita ya Dizeli na Petroli kiasi cha Tsh. Bilioni moja.

Fedha ya Jimbo la uchaguzi Tsh. Milioni 500 na fedha kutoka mfuko wa barabara kiasi cha zaidi ya Milioni 700 na kwamba hadi kufikia Machi, 2023 TARURA imepokea fedha Bilioni 1.295 sawa na asilimia 58.6.

Anasema Vivuko/Karavati 24 vimejengwa pamoja na Mitaro ya maji ya mvua yenye jumla ya urefu wa mita 1,900 sawa na km 1.9 pamoja na ukarabati wa barabara za udongo jumla km 145.02 Kata mbalimbali katika Halmashauri hiyo.




Barabara ya Nkongore iliyoboreshwa hivi karibuni kuwekwa moramu na mawe kwa ajili ya kujenga kingo.





No comments