HEADER AD

HEADER AD

WATAKIWA KUTOWAFICHA, KUWATENGA WATOTO WENYE CHANGAMOTO YA AFYA YA AKILI

Na Lubango Mleka, Tabora

KATIKA kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika, wazazi, walezi na wananchi mkoani Tabora wametakiwa kutokuwaficha na kuwatenga watoto wenye changamoto ya afya ya akilia, bali watenge muda wa kuwajumuisha na kuonana na wataalamu ili wapatiwe elimu jinsi ya kuishi na kuwalea watoto hao.

Hayo yamesemwa na mwanzilishi  wa shirika lisilo la kiserikali la Akili Platform Tanzania mkoani Tabora linalojishughulisha na utoaji wa huduma kwa watoto wenye changamoto ya afya ya akili, Roghat Robert katika hafla ya kushiriki siku ya mtoto wa Afrika inavyofanyika kila tarehe 16, ya mwezi Juni kila mwaka iliyoandaliwa na shirika hilo Tabora mjini.

Amesema kumekuwa na wazazi ambao wamekuwa wakiwatenganisha watoto hao na wenzao kutokana na matatizo hayo, hivyo amewaomba wazazi na walezi kuwasiliana na wataalamu wa afya ya akili jinsi ya kuwalea watoto hao.

   Baadhi ya watoto wenye changamoto ya Afya ya akili wakiwa na wazazi wao katika chakula cha pamoja

" Tunawaomba wazazi, walezi, ndugu, jamaa na marafiki watambue kwamba changamoto ya afya ya akili ni suala mtambuka, kila mmoja anatakiwa kuwa barozi wa kulinda, kutetea, kuendeleza na kuimalisha sula la afya ya akili katika familia.

"Wazazi, walezi na ndugu au jamaa wawalete watoto katika kujumuika na watoto wengine ili waweze kuchangamana, kufanya shughuli za pamoja kulingana na hali walizonazo," amesema Robert.

Ameongeza kuwa, wazazi watenge muda wa kuonana na wanasaikolojia kuongea nao kulingana na tabia za watoto wao wanazokuwa wanazifanya  na kuzionesha katika familia zao  itasaidia kwa namna moja ama nyingine, ambapo mzazi atakuwa anatambua lini mtoto anahitaji nini na kwa wakati gani.

Aidha, amesema kuwa, kuna mitazamo mingi katika jamii juu ya watoto hao, ambapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakiona ni laana na mkosi katika familia, hivyo amewataka kuwaona kama watoto wengine wasiyo na changamoto ya afya ya akili.

"Mtoto anyazaliwa na shida ya afya ya  akili, wengine watasema amelogwa, ni laana na vitu kama hivyo, lakini ni kwamba hawana elimu ya kutosha juu ya mtazamo huo, ndiyo maana kwenye saikolojia tunasema ukiona mtu anamcheka mtoto mwenye tatizo la akilia anayefanya matendo yake, huyo anayecheka ndio anatatizo," akisema Robert.

Robert ameendelea kusema kwamba, mtazamo huo upo na ndio maana wanawaunganisha katika siku kubwa kama hiyo na ndio maana wamewaunganisha wazazi na kuona kuwa yeye anamtoto kama huyo lakini kuna mwingine naye aneya kama wake.

Hivyo sio shida yake peke yake, na pia kama ni familia basi wote wanavuta hewa kama binadamu, wanakula chakula, wanakwenda haja ndogo na kubwa utofauto ni matendo tu.

Badhi ya watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete wakiwa na Mkurugenzi wa shirika la Akili Platform Tanzania mkoani Tabora Roghat Robert watano kutoka  kushoto (mwenye tisheti jekundu) wakiwa na maziwa kwa ajili ya kunywa.

Hata hivyo amezitaja changamoto zinazolikabili shirika la Akili Platform, kuwa ni uhaba wa viti mwendo, vifaa vya mawasiliano na wazazi kama vile simu janja zitakazo ungwa na mfumo wa kuonana na wataalamu moja kwa moja kama kuna shida kwa mtoto.

Pia vifaa vya ofisini, vifaa vya michezo kwa watoto hao, hivyo amewaomba wadau wote nchini kusaidia shirika hilo vifaa vitakavyo wezesha watoto hao kushiriki shughuli kama hizo na watoto wengine.

Katibu wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete, Marcela Sila na  Mratibu wa Magonjwa ya Akili Dokta Swaumu wameushukuru uongozi wa Shirika hilo na kuomba kuendelea na moyo wa kujitoa katika kusaidia watu wenye ulemavu wa akili.

"Kwanza kabisa natoa shukrani kwa niaba ya Hospitali ya Rufaa mkoa wa Tabora Kitete kwa kutuona na kuja kujumuika nasi kwa hiki kidogo mlichotupatia katika siku hii ya mtoto wa Afrika, sisi tuko tayari kuendelea kuimalisha ushirikiano ili kuona namna ya kuisaidia jamii katika eneo la Afya ya akili,"  amesema Sila.

Naye Mratibu wa afya ya akili mkoa wa Tabora Dokta Swaumu Kimaro anaeleza kuwa anaendeleza ushirikiano na mshikamano katika kuhakikisha elimu ya afya ya akili inafika kila mtaa kwa mkoa mzima wa Tabora kupitia wadau na kitengo chake ambapo aliwaomba wadau waweze kuwezesha shirika la Akili Platform Tanzania kwani linafanya kazi kubwa ya kizalendo kwa kujitolea.

Steavin Leonard, Selina Laurent, Felista Masele na Shabani Ramadhani ni wazazi waishio manispaa ya Tabora wanaoishi na watoto wenye changamoto ya afya ya akili, wameeleza baadhi ya changamoto zinazowakabil katika kuwalea watoto hawa, ikiwemo changamoto ya usafiri unaowezesha kufika shuleni, unyanywasaji kutoka kwa walimu na jamii na kukosekana kwa viti mwendo.

"Changamoto tunazozipata ni nyingi, hasa suala zima la unyanyapaa, watoto wetu wananyanyapaliwa  sana hata shuleni wanasema mimi sewezi kumfundisha mtoto huyu amenishinda tafuta shule nyingine, unyanyapaa mwingine ni unakuta mtu hajuu huyu mtoto yupo vipi akikosa anampiga badala ya kumuelekeza," amesema Selina.

Felista ameeleza " Mazingira ninayoishi siyo rafiki mimi nina mtoto wa kike mwenye tatizo la afya ya akili, jamii kubwa inayomzunguka ni vijana wa kiume, sasa nina kuwa na wasiwasi mkubwa sana juu ya mtoto wangu," amesema Felista.

Wametoa ushauri kwa wazazi kutowaficha watoto hawa, kwani kufanya hivyo ni kuwanyima kufikia ndoto zao na kuonyesha vipaji vyao kwa jamii.

     Baadhi ya watoto wenye changamoto ya afya ya akili wakicheza

Shirika hilo katika mkoa wa Tabora linaadhimisha siku hii ya mtoto wa Afrika, ambayo kwa mwaka huu inakauli mbiu isemayo ' ZINGATIA USALAMA WA MTOTO KATIKA ULIMWENGU WA KIDIGITALI', kwa kufanya shughuli mbalimbali.

Shughuli hizo ni pamoja na utoaji wa maziwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tabora Kitete katika kitengo cha watoto wenye matatizo ya afya ya akili, kufanya michezo mablimbali kwa watoto hao, pamoja na mjadala unaolenga namna ya kusaidia wazazi na watoto wanaopelekewa na changamoto kama hizi.

>>>Kila Mwaka Dunia huadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika (Day of the African Child) ni siku inayosherehekewa ifikapo Juni 16 ya kila mwaka tangu mwaka 1991 ilipoteuliwa na Umoja wa Afrika.

Umoja wa Mataifa uliteua siku hiyo kama kuenzi michango ya watoto walioshiriki katika maandamano kwenye mji wa Soweto, Afrika Kusini mwaka 1976 ikiwa ni pamoja na kujengea jamii uelewa juu ya umuhimu wa elimu bora na malezi kwa watoto.

Itakumbukwa  kuwa, Juni 16, 1976, maelfu ya watoto katika nchi ya Afrika Kusini walikusanyika katika mji wa Soweto kwa ajili ya maandamano yenye malengo ya kudai elimu bora, mamia ya watoto walipigwa risasi na kuuliwa na watoto zaidi ya elfu moja walijeruhiwa.

Ifikapo tarehe 16 ya kila mwaka, mataifa, jumuia mbalimbali na jumuia za kimataifa pamoja na wadau mbalimbali hukusanyika pamoja kwa ajili ya kujadili fursa na changamoto zinazowakumba watoto katika bara la Afrika.

1 comment:

  1. Hongera sana kwa shughuli nzuri sisi wadau wa Afya ya Akili 0626 551 859 WhatsApp tunawashukuru sana

    ReplyDelete