MADIWANI WAJADILI HOJA RIPOTI YA CAG, RC ATIA NENO MIRADI UJENZI WA MASOKO YA SAMAKI
Na Boniface Gideon, Tanga
MKAGUZI Mkuu wa nje wa Hesabu za Serikali mkoa wa Tanga amebaini uwepo wa dosari namna ya uendeshaji wa miradi ya masoko ya samaki huku miradi hiyo ikishindwa kutoa faida licha ya Serikali kuwekeza fedha nyingi kupitia sekta hiyo ya Uvuvi.
Aidha Halmashauri hiyo imeonekana kupunguza kiwango cha hoja zilizoibuliwa na CAG kwa Mwaka wa fedha 2021/2022 kutoka hoja 44 hadi kufikia hoja 41 huku hoja nyingi zikionekana kujirudia kila mwaka hali iliyoonekana kuwakasirisha viongozi wengi wa Halmashauri hiyo hususani Madiwani na Mkuu wa mkoa huo Waziri Kindamba.
Hoja hizo za CAG ziliibuliwa Juni, 19 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi kwamujibu wa Sheria kujadili Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Tanga Waziri Kindamba na kuchambua hoja 41 ambazo CAG amezitolea kwenye Ripoti yake ya mwaka wa fedha 2021/2022 na zinatakiwa zifanyiwe kazi kabla ya mwaka wa fedha kufungwa juni 30 mwaka huu.
Katika hoja za CAG ameonesha kutokuridhishwa na namna Halmashauri hiyo inavyoendesha na kusimamia masoko ya samaki huku mapato yatokanayo na sekta ya uvuvi yakionekana kupotea kutokana na isimamizi mbovu.
Masoko hayo ni Mchukuuni,Tongoni na Deepsea huku soko kuu la samaki Kisosora likinyooshewa vidole na Madiwani kufanyiwa ukarabati ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Katika Ripoti hiyo mkaguzi ameonesha kutokufurahishwa na mazingira mabovu ya kufanyia biashara katika soko la Deepsea huku kwakiwango kikubwa masoko mengine kutokufanya kazi kwa ufanisi.
Akijibu hoja hiyo ya masoko ya Samaki , Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Spora Liana amesema;
‘’Tumetenga Mil.300 kwaajili ya ukarabati na ujenzi wa vizimba vya kuuzia samaki soko la Deepsea, kuhusu masoko mengine ya Tongoni na Mchukuuni yapo kwenye mradi wa Botnar foundation lakini pia wavuvi tuliwanunulia Boti kwaajili ya kuwahamasisha kuanza kufanya kazi ya uvuvi’’ amesisitiza Liana
Hoja hiyo imeonekana kumkasirisisha Mkuu wa Mkoa Tanga Waziri Kindamba na kutoa tamko.
‘’Tanga jiji ndio kioo cha mkoa wa Tanga na mikoa ya Kanda ya Kaskazini Mashariki, sisi tuna ukanda mzuri wa Bahari na ndio mgodi wetu wa madini tunaoutegemea kwenye vitu vingi ikiwamo kitoweo cha Samaki aina mbalimbali ambao hawapatikani katika mikoa ya Bara.
"Mkurugenzi hakikisha unawapeleka Wataalamu wako hata huko Pemba waende wakajifunze uchumi wa bluu ili tuende sawa kwapamoja, tunahitaji uchumi wetu ukue hasa kupitia bahari yetu ambayo wengine wanaililia ‘’ amesema Waziri Kindamba
Miradi mingine ambayo imetiliwa shaka ni kuchelewa ujenzi wa jengo la stendi mabasi kange, mfumo mbovu wa ukusanyaji mapato eneo la mapumziko forodhani.
Pia fremu za maduka ya biashara za stendi ya Pongwe ambayo ina fremu za maduka 88 lakini mfumo wa mapato hauonyeshi kulipiwa ambapo hadi sasa kwa mujibu wa ofisa ya biashara wa Halmashauri hiyo Lusia Malando ni Sh 400,000 kati ya Milioni 3 pekee ndizo zimelipiwa.
Amesema ni kinyume na makubaliano kati ya wanyabiashara na halmashauri kutokana na kuwa fremu hizo hazikujengwa na halmashauri bali Wafanyabiashara kwa makubaliano maalumu.
Post a Comment