HEADER AD

HEADER AD

DC BURA AWATAKA WAZAZI KUACHA UKATILI KWA WATOTO

>>Awasisitiza kuchangia chakula shuleni

Na Samwel Mwanga,Uyui

WAZAZI na Walezi wametakiwa kutimiza majukumu yao katika kulea watoto wao na kuacha kuwafanyia ukatili kwa mikono yao wenyewe.

Pia amewasisitiza kuchangia chakula cha mchana shuleni kwa ajili ya watoto kwani kutofanya hivyo kunawafanya baadhi ya wanafunzi wajiingize katika vishawishi.

Hayo yameelezwa Juni 16 mwaka huu na Mkuu wa wilaya ya Tabora, Louis Bura katika Kijiji cha Misole kilichopo Kata ya Lutende wilaya ya Uyui katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika kimkoa katika kijiji hicho.

     Mkuu wa wilaya ya Tabora, Louis Bura akihutubia siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika kimkoa katika Kijiji cha Misole ,Kata ya Lutende wilaya ya Uyui.

Amesema kuwa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali wamekuwa mstari wa mbele kutetea haki za watoto na kupambana na ukatili dhidi ya watoto lakini bado baadhi ya wazazi wamekuwa kikwazo kwenye harakati hizo.

Amesema kuna wazazi wameshindwa kwa makusudi kuwalipia chakula cha mchana wawapo shuleni, kwa madai kuwa elimu ni bure, jambo ambalo linakwamisha juhudi za serikali pamoja na kudhorotesha kiwango cha ufaulu kwa watoto.

     Mkuu wa wilaya ya Tabora, Louis Bura(aliyebeba mtoto)akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wanaohudumiwa na Shirika la World Vision kupitia Mradi wa Maendeleo ya Jamii Lutende ulioko wilaya ya Uyui.

"Tusaidie ustawi wa watoto wetu kwa kusaidiana na serikali ambayo kwa sasa inatoa elimu bure kwa shule za msingi hadi sekondari, nasi tubebe jukumu la kuhakikisha tunachangia chakula shuleni hasa kwa shule za msingi tayari baadhi ya wadau wa maendeleo kama Shirika la World Vision limeonyesha njia katika Kata ya Lutende katika suala la chakula shuleni,".

"Kwa tabia ya kutokumpa mtoto chakula cha mchana huo ni ukatili, haiwezekani mtoto kushinda na njaa, kuanzia asubuhi mpaka jioni akiwa shuleni, halafu useme unampenda mtoto wako, huo ni ukatili na unapaswa kuachwa mara moja" amesema.

Amewasihi wazazi kuwaonea huruma watoto wao,  na kutambua kuwa Sera ya elimu bila malipo, inaweka wazi majukumu ya serikali na majukumu ya mzazi kwa mtoto, ikiainisha jukumu la mzazi ni pamoja na kumpatia mtoto chakula cha mchana kwa shule za kutwa, kumpatia vifaa vya shule na mahitaji yake yote ya msingi.

 Baadhi ya watoto na watu wazima wakiwa kwenye Sherehe ya Siku ya Mtoto wa Afrika katika mkoa wa Tabora kwenye kijiji Cha Misole wilaya ya Uyui.

Aidha amewataka watoto nao kuacha mara moja matumizi ya simu za mkononi hasa simu janja na runinga bila uangalizi wa watu wazima sambamba na kwenda kwenye maeneo hatarishi kama yale ya starehe kwani katika mazingira hayo wanaweza kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

Naye Meneja wa Shirika la World Vision, Kanda ya Ziwa, Jacqueline Kaihura amesema kuwa shirika linajihusisha na kupambana na ukatili dhidi ya watoto kwa kuwalea na  kupambana na mimba za utotoni kwa kutoa elimu na kuwasaidia watoto katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya jamii.

      Meneja wa World Vision,Kanda ya Ziwa, Jacqueline Kaihura akisisitiza jambo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika katika mkoa wa Tabora katika Kijiji cha Misole wilaya ya Uyui.

Amesema kuwa baadhi ya Wazazi na walezi wamewageuza watoto wa kike kama mtaji kwa kuwaozesha kwa wanaume ili waweze kupata ng'ombe na kuwaachisha masomo na hivyo kufanya ndoto za maisha ya mtoto huyo kutotimia.

 "Tuache tabia ya ukatili kwa kuwafanya watoto wetu hasa wa kike kuwa mtaji kwa kuwaozesha ili tupate ng'ombe na tukifanya hivyo tunapoteza ndiyo za watoto wetu za baadaye ni vizuri tuwaache wamalize masomo yao na kuolewa kupo tu tena atampata mwanamme ambaye anampenda,"alisema.

Mratibu wa Mpango wa Maendeleo ya Jamii Lutende(Lutende AP)uliopo chini ya Shirika la World Vision, Ngasa Michael amesema kwa kutambua umuhimu wa ulinzi wa mtoto wameweza kusambaza mbegu za viazi lishe na mahindi lishe kwa shule zote za msingi katika Kata hiyo ili kuwasaidia wanafunzi waweze kupata chakula cha mchana wanapokuwepo shuleni.

  Wanafunzi wakiwa na bango wakipita mbele ya Mgeni Rasmi mkuu wa wilaya ya Tabora, Louis Bura wakati wa Sherehe ya Siku ya Mtoto wa Afrika katika mkoa wa Tabora iliyofanyika kimkoa kwenye Kijiji cha Misole wilaya ya Uyui.

Baadhi ya Wazazi walisema kuwa moja ya changamotoi nayowakabili ni kuweka viapumbele kwenye masuala yasiyo ya muhimu ambayo hugharimu pesa nyingi na kushindwa kukidhi mahitaji ya watoto.

Wamefafanua kuwa, wazazi wako radhi kuchangia fedha nyingi kwenye harusi na Sherehe mbalimbali zikiwemo za 'kumsalimia mtoto aliyezaliwa', na kushindwa kuchangia chakula cha mchana cha mtoto wake, jambo ambalo wamethibitisha ni ukatili unaofanywa wazi na wazazi.

"Ni rahisi kabisa, kutoa shilingi laki moja mpaka tano kuchangia harusi au Sherehe za kuzaliwa na kutelekeza kulipia chakula cha mtoto cha shilingi laki moja kwa mwaka mzima" amesema Hollo Jimoga.

Pia wameitaka jamii sasa kubadilika na kuanza kuwekeza fedha nyingi kwenye elimu na sio kwenye masuala ya kijamii, ambayo kimsingi ni ya muda mfupi na hayana tija kwa taifa letu la Tanzania.


No comments