JICHO LA TANZANIA LAHIMIZA UHIFADHI VYAKULA KWA NJIA ZA ASILI
>> Imeelezwa kuwa uhifadhi wa vyakula ni muhimu kwa matumizi ya baadae
Na Dinna Maningo, Mara
MWENYEKITI wa Jicho la Tanzania Organization Taifa amewashauri wananchi kutumia njia za asili katika kusindika na kuhifadhi mazao hasa mazao ya msimu kama nyanya,viazi, ndizi na matunda mbali mbali kwani njia hiyo itawapunguzia gharama na hivyo kujiinua kiuchumi.
Akizungumza na DIMA Online Mwenyekiti huyo Sospeter S. Ndabagoye amesema usindikaji na uhifadhi wa vyakula una faida kubwa hasa katika msimu wa vyakula ambapo bei hushuka na hivyo mkulima kujikuta akiuza mazao kwa bei ya hasara. Hali hiyo kumfanya mkulima kuendelea kuwa na maisha duni.
"Mazao mengi yanaharibika kwasababu hayajatengenezewa thamani, mfano msimu wa ndizi huwa zinashuka bei, ndizi nyingine mpaka unawapa mifugo kama vile mbuzi, nguruwe, ng'ombe na kondoo wanakula hadi zinawakinai, zinabakia kuoza tu.
"Ndizi hizo una uwezo wa kuzisindika na kuzihifadhi kwa matumizi ya baadaye. Changamoto kubwa kizazi chetu tumesahau asili zetu; tunadharau vitu vyetu vya asili vya zamani, kuna vyakula vilikuwa vinahifadhiwa kwa njia za asili ambapo watu walikuwa wana uwezo wa kuhifadhi chakula hata kwa miaka miwili au mitatu kwa njia ya moshi tu" amesema Sospeter.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa Shirika la Jicho la Tanzania litawakumbusha watanzania kwa kutoa elimu ya mbinu za kusindika na kuhifadhi vyakula kwa njia za asili ambazo ni salama kwakuwa hakuna kemikali yoyote inayohusika kwenye uhifadhi wa chakula hicho.
"Sisi kama Jicho la Tanzania pamoja na mbinu zingine za kisasa tunaenda kuwakumbusha watu mbinu za asili zilizotumika kuhifadhi vyakula vyetu ili kupunguza gharama za usindikaji wa vyakula ili mwenye kipato cha juu aweze kusindika na mwenye kipato cha chini aweze kusindika pia.
" Lengo ni kuhakikisha chakula hakiharibiki kwasababu ya kushindwa kuhifadhi, lakini pia ni kukiongezea thamani na ubora.
"Mathalani, ukisindika unga wa ndizi, unauweza kuuza unga wa ndizi kilo moja hadi Tsh. 50,000/= hii ni kwasababu licha ya kuwa ni chakula, bali pia unga wa ndizi pamoja na kwamba ni chakula ni dawa, mtu akitumia ule unga anaenda kuondoa maradhi mbali mbali mwilini" amesema Sospeter.
Amesisitiza kuwa zipo mbinu mbalimbali za kuhifadhi vyakula kwa njia ya asili pasipo kuviwekea dawa zozote na vikawa salama bila kuharibika.
"Mfano mahindi mtu anaweza kuyahifadhi pasipo kuweka dawa zozote zinazotoka kiwandani na mahindi yakabaki salama bila kubunguliwa na ubora wa mahindi usiharibiwe na yakabaki na radha ya asili na hivyo kumfikia mlaji. Hata mboga za majani zinakaushwa kwa njia za asili kama vile (Nsansa) mboga ya asili kwa wenyeji wa mkoa wa Tabora.
"Mipango ya kutoa elimu hiyo ipo mingi ,tutatoa elimu kwa njia ya semina, warsha, makongamano,maonesho na mikutano. Kwa sasa tumeanza kutoa elimu kupitia vyombo vya habari na muziki.
"Tuna mpango mkubwa ambao utakuwa wa kufundisha watoto wadogo huko mashuleni, pia kwenye vikundi vya usindikaji. Tunafahamu kwamba nchi yetu ina wajasiriamali wengi" amesema Sospeter
Mwenyekiti amesema kupitia vikundi vya ujasiriamali halmashauri mbalimbali, Jicho la Tanzania Organization litatoa elimu ya usindikaji na uhifadhi wa chakula kwa njia za asili ili kuweza kuboresha au kuwa na uhakika wa chakula katika Taifa la Tanzania.
Post a Comment