DC MASWA ASHAURI WANANCHI WASHIRIKISHWE UUNDWAJI KAMATI UJENZI VETA MASWA
Na Samwel Mwanga, Maswa
MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu, Aswege Kaminyoge ameongoza wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kutambua eneo ambalo litatumika kujenga Chuo Cha Ufundi Stadi na huduma (VETA)katika wilaya hiyo eneo la Sola mjini Maswa.
Mkuu huyo wa wilaya amemshukuru Rais wa awamu ya Sita, Dkt Samia Suluhu kwa kuwapatia mradi huo utakaojengwa katika wilaya hiyo huku akisisitiza wananchi kuuona mradi huo kama wao na kwamba ni vizuri wakawa walinzi wa vifaa vyote vya ujenzi katika eneo hilo.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge (mwenye kaunda suti ya kijivu) akizungumza na wananchi wa eneo la Sola pamapojengwa Chuo Cha Veta wilaya ya Maswa.
Amesema kuwa katika kuunda kamati za ujenzi wa chuo hicho ni vizuri katika kila kamati walau awepo mwananchi mmoja au wawili wa eneo hilo na kuwataka wajumbe wa kamati hizo kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya Sita Iko kazini katika kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo kwa lengo la kuwainua kiuchumi wananchi hivyo ni vizuri kwa wananchi na Viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya chini kutangaza mambo yote mazurk yanayofanywa na serikali.
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Malampaka wilayani humo,Marco Mahundi amewaeleza wajumbe hao kuwa chuo hicho ndicho kimepewa jukumu la usimamizi wa ujenzi kwa kushirikiana na Mshauri Mwelekezi wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia ambaye ni chuo cha ufundi Arusha.
Ujenzi wa chuo Cha Veta Maswa katika eneo la Sola mjini Maswa umeanza
Amesema kuwa chuo hicho kitajengwa kwenye eneo la Sola lenye ukubwa wa Hekari 20 kwa gharama ya Tsh.1,483,532,660.45 hivyo wameona ni busara kutambulisha mradi huo mkubwa kwa uongozi wa wilaya hiyo pamoja na wananchi wa eneo wa eneo hilo.
"Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Malampaka ndiyo tumepewa jukumu la kusimamia mradi wa ujenzi wa chuo cha Veta wilaya ya Maswa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia hivyo tumefika leo kutambulisha mradi huu kwa viongozi wa wilaya pamoja na wananchi wa eneo la Sola ambapo chuo kinajengwa,"
"Huu mradi tutausimamia ili ukamilike kwa wakati na tumekwisha kuanza kazi tunategemea vijana 120 watapata ajira ya muda na kwa sasa tayari tumepokea kiasi cha Tsh. Milioni 200.2 kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya kuanza ujenzi huo,"amesema.
Amesema kuwa ujenzi huo ni wa kipindi cha miezi nane na umeanza rasmi Mei 17 mwaka huu hivyo kipindi walichopewa ni kirefu kwani wanategemea kukamilisha ujenzi huo mwezi Desemba mwaka huu badala ya mwezi Januari mwakani iwapo fedha zitapatikana kwa wakati.
Naye Mhandisi David Minji kutoka Chuo cha Ufundi Arusha ambaye ndiye Mshauri Mwelekezi amesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa chuo cha VETA utakuwa na majengo tisa ambayo ni;
Jengo moja la utawala, jengo moja la darasa, kibanda kimoja cha mlinzi, nyumba moja ya mkuu wa chuo, jengo la karakana tatu(3), jengo moja la choo na jengo moja la umeme.
Amesema kuwa ujenzi huo utafanyika kwa mfumo wa Force akaunti ambapo watakaofanya kazi ni mafundi wazawa na watoa kipaumbele kwa mafundi wa wilaya hiyo na mkoa wa Simiyu.
Naye Diwani wa Kata ya Sola,Masanja Mpiga amesema kuwa mradi huo unakwenda kutekelezwa ndani katika Kata hiyo hivyo watatoa ushirikiano kuhakikisha wanalinda vifaa vyote vya ujenzi vitakavyotumika kwenye ujenzi huo.
Chuo hicho ni miongoni mwa Vyuo 63 vitakavyojengwa nchini katika halmashauri za wilaya.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge (mwenye kaunda suti ya kijivu) akizungumza na wananchi wa eneo la Sola pamapojengwa Chuo Cha Veta
Post a Comment