HEADER AD

HEADER AD

WAZIRI UMMY: MLIPUKO WA UGONJWA WA MARBURG UMEISHA

Na Alodia Babara, Bukoba

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema Tanzania hususani mkoa wa Kagera ni salama baada ya mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa marburg kuisha kutokana na wataalam kujiridhisha

Ni baada ya kutotokea maambukizi mapya na wagonjwa wapya kwa siku 42 tangu mlipuko wa ugonjwa huo ulipotokea nchini katika mkoa wa Kagera na kusababisha vifo vya watu sita.

Waziri Ummy ameyasema hayo Juni 02, 2023 katika kilele cha mapambano ya mlipuko wa ugonjwa wa Marburg kilichofanyika mjini Bukoba.

    Waziri wa Afya Ummy Mwalimu

"Ushirikiano wa dhati kutoka kwa wananchi, Serikali, watumishi wa idara ya Afya na wadau kutoka ndani na nje ya nchi ndio umechangia kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa huu.

"Kwa sasa tunasherehekea, hivyo natangaza leo ugonjwa huu umeisha Tanzania ni salama ila tusibweteke tuendelee kujikinga na kutoa taarifa pale tunapoona mambo tusiyoyaelewa "amesema Waziri Ummy. 

Amesema mlipuko huo ulitangazwa rasmi na Waziri wa afya kwa mara ya kwanza katika kata za Maruku na Kanyangereko wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Machi 19 mwaka huu kuwa ni ugonjwa wa Marburg ambapo  walipatikana wagonjwa tisa kati yao watatu wamepona na sita walipoteza maisha.

Amesema vifo hivyo alikuwemo mtumishi wa Afya ambaye alikuwa mtaalam wa maabara katika kituo cha Afya Maruku aliyehudumia wagonjwa wa kwanza, mtoto mdogo wa miezi 18 na wengine wanne kutoka familia moja ambapo Serikali inaendelea na uchunguzi ili wajue kiini cha mlipuko huo.

Ameongeza kusema kuwa Serikali  imetoa Tsh. Milioni tano kama kifuta jasho kwa familia ya mtumishi huyo wa idara ya Afya aliyefariki akiwa kazini kwa ajili ya kusaidia katika masuala mbalimbali ya familia hiyo ikiwemo ada za watoto wanne.

Amesema serikali itaendelea kuwahudumia na Dk Nduru ambaye alipata ugonjwa na kupona ataendelea kuhudumiwa na ikiwezekana kumpeleka nchi za nje kwa ajili ya matibabu zaidi.

Aidha amesema Serikali inaendelea kupambana na magonjwa mbalimbali ikiwemo ya mlipuko kwa kuboresha huduma za Afya na kuleta vifaa tiba huku akiwashauri wananchi waendelee kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapoona kumezuka ugonjwa usioeleweka na watu kutozikwa ambao wamefariki kwa vifo ambavyo hawajavielewa.

Amewataka wananchi kutambua kuwa kumalizika kwa mlipuko huu isiwe mwisho wa kuendelea kujikinga na kutoa taarifa sahihi.

Amewaomba viongozi wa dini kuendelea kuiombea Tanzania mwenyezi Mungu haepushe majanga ya milipuko ya maradhi yanayotabiliwa na wataalam wa dunia kwamba inatatokea siku za usoni hapa duniani.

Kwa upande wake Daktari wa ugonjwa wa Marburg ambaye alikuwa mtaalamu wa afya kituo afya Maruku Dk. Mahona Nduru ametoa shukrani kwa madaktari wote waliosaidia kupona kwake na akawatahadharisha wataalamu wenzake wanapokuwa wanatimiza majukumu yao kuchukua tahadhari.

Naye katibu Tawala wa mkoa wa Kagera Toba Nguvila ametoa maombi matatu kwa Serikali kwa kuomba kujengewa kituo maalum cha kuhudumia wagonjwa wa magonjwa ya mlipuko inapojitokeza.

Pia kujengwa vituo vya matibabu mipakani kwasababu mkoa upo mpakani hali inayosababisha kukumbwa na magonjwa mbalimbali ya mlipuko, kuboresha chuo cha Afya cha Kagemu kwa kuwapatia gari na kujenga jengo la utawala.

Hata hivyo mganga mkuu wa Serikali Prof.Tumain Nagu amesema mafanikio hayo yametokana na kupata taarifa mapema na kuchukua hatua mapema.

Amewashukuru wadau mbalimbali walioshirikiana na Serikali katika mapambano hayo ikiwemo shirika la Afya duniani (WHO),UNICEF,US CDC na ,Africa CDC.

No comments