MTOTO WA DARASA LA TATU AFANYIWA VITENDO VYA UKATILI
Na Samwel Mwanga, Simiyu
MWANAFUNZI wa kike wa darasa la tatu mwenye umri wa miaka 12 wa shule ya msingi Migato katika wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu amefanyiwa vitendo vya kikatili kwa kubakwa akiwa anavuna karanga katika shamba lililoko jirani na nyumbani kwao.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP)Edith Swebe kwa waandishi wa habari imeeleza kuwa tukio hilo limetokea Juni 4 mwaka huu majira ya saa 5:00 asubuhi katika kitongoji cha Bukingwaminzi kilichopo katika Kijiji cha Migato wilayani humo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtoto huyo alifanyiwa kitendo cha kikatili na mtu asiyemfahamu kwa sura.
Kamanda Swebe ameeleza kuwa mtoto huyo akiwa peke yake kwenye shamba la nyumbani kwao umbali wa mita 140 akivuna karanga ndipo alivamiwa na mtu huyo na kufanyia vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.
Amesema kuwa kwa sasa mtoto huyo anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Simiyu na hali yake inazidi kuimarika.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na tayari watu wawili wameshakamatwa wakihojiwa kuhusiana na tukio na atakayebainika au watakaobainika watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika na kubainika kufanya kitendo hicho.
Aida Jeshi la Polisi mkoa wa Simiyu linatoa onyo kali kwa wananchi wanaoendelea kutenda makosa ya ukatili dhidi ya watoto vilevile linawaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa fiche za mtu au watu wote wanaojihusisha na matukio ya vitendo vya uhalifu ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Post a Comment