TMDA YATANGAZA KUPOKEA KAZI ZA WAANDISHI WA HABARI KUWANIA TUZO
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetangaza rasmi kupokea kazi za Waandishi wa Habari kuwania tuzo maalumu za msimu wa pili kwa walioripoti taarifa na kuandaa Makala mbalimbali kuhusu kazi na majukumu ya TMDA katika kipindi cha Julai, 2022- Mei, 2023.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo amesema lengo la tuzo hizo ni kutambua mchango wa Waandishi wa habari na kuleta hamasa katika kuelimisha jamii kuhusu masuala ya udhibiti wa dawa, vifaa tiba,vitendanishi na bidhaa za tumbaku kupitia vyombo vya habari ili kulinda afya ya jamii.
"Kazi zinazolengwa ni zile zilizoripotiwa kupitia runinga (TV), Redio, Magazeti na mitandao ya kijamii kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Mei mwaka huu 2023.
Baada ya kupokelewa, zitashindanishwa na hatimaye kuwapata washindi watakaopewa tuzo." Amesema Adam Fimbo katika taarifa yake hiyo.
Aidha, ameongeza kuwa TMDA inawaalika waandishi kuwasilisha kazi zao kabla ya tarehe 15 Julai, 2023.
"Kazi zote Waandishi watume kupitia barua pepe: commpedtmda@gmail.com au kwa njia ya CD, katika ofisi za TMDA zilizopo Dodoma, Dar es salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Mtwara, Tabora na Geita." Amesema Adam Fimbo.
Post a Comment