HEADER AD

HEADER AD

SAKATA LA TUHUMA ZA ZCO MAFWELE LATUA KWA WAZIRI MASAUNI

>> Ni kuhusu utata Jalada kituo cha Polisi Stakishari 

 Baraka Shile, Dar es Salaam

SAKATA la Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam (ZCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Faustine Mafwele kudaiwa kuzuia askari polisi wa kituo cha Stakishari kukamata watuhumiwa wanaohusika katika jalada namba  STK/IR/11978/2022, limetua mezani kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Waziri Masauni amesema amepokea malalamiko hayo ya askari wake huyo kutuhumiwa kukwamisha askari wenzake kufanya upelelezi wa jalada lililokuwa mezani kwao katika kituo hicho.

Kitendo hicho kinachodaiwa kuwa ni maslahi binafsi kwa kushirikiana na mtuhumiwa anayetajwa kuwa ni 'Bilionea' Wilson Kiguha Chacha, hivyo ameahidi kulifanyia kazi suala hilo haraka iwezekanavyo ili haki itendeke.

“Nimepokea malalamiko ya askari wangu akilalamikiwa kushirikiana na mtuhumiwa kukwamisha upelelezi kwa lengo la kuhakikisha jalada hilo pamoja na watuhumiwa hawafikishwi Mahakamani, ikibainika tuhuma hizo ni za kweli hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya askari huyo mara moja.

“Tuhuma hizi ni nzito kwa askari wangu hivyo nipeni muda nilifatilie jambo hili kwa kina, ni kweli kuna baadhi ya askari wetu wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya utendaji wa jeshi la polisi na wengine hata kushirikiana na wahalifu” amesema Waziri Masauni.

Waziri Masauni amewataka wananchi kutoa taarifa pale wanapoona kunaviashiria vya kuminywa kwa haki zao na askari polisi ili hatua kali zichukuliwe kwa lengo la kukomesha vitendo hivyo.

“Maeneo ambayo tumedhamiria kuyaboresha ni la upelelezi, ubambikizaji wa kesi, utoaji wa dhamana na hayo yamekua maeneo ambayo tumekua tukipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.” Amesema Masauni.

Hata hivyo Waziri Masauni amewataka askari wote kufanya kazi kwa weledi kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

ZCO Mafwele anatuhumiwa kunyakua jalada na kutokomea nalo lenye kesi ya uvunjaji na wizi wa mali katika bar ya Big Mountain, hivyo kukwamisha upelelezi ambapo hivi sasa ni zaidi ya miezi sita (6).


Jalada hilo namba STK/IR/11978/2022 linalowahusu wafanyakazi wa Kampuni ya Wikicha Estate Development Agency inayomilikiwa na Bilionea Wilson Kiguha Chacha inayo miliki na kusimamia shughuli zote zinazofanywa kwenye kiwanja namba 48766 kilichopo Ukonga Banana jijini Dar  es Salaam.

Taarifa kutoka ndani ya kituo cha Polisi Stakishari zinaeleza kuwa ZCO Mafwele kwa kutumia mamlaka yake amewapiga marufuku askari wote wa kituo hicho kukamata muhusika yeyote aliyehusika kwenye tukio la uvunjaji wa bar hiyo na hivyo askari yeyote atakayekaidi amri hiyo atakiona cha moto.

Habari zaidi zinaeleza kuwa taratibu za jalada kuhama kutoka kituo kimoja kwenda kingine zinajulikana lakini ZCO Mafwele hakufuata taratibu hizo hali ambayo hata wapelelezi wa kesi hiyo hawajui kinachoendelea.

Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo ZCO Faustine Mafwele hakukubali wala kukataa na badala yake amesema kuwa yeye si msemaji hivyo atafutwe kiongozi wake.

Alipoulizwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) Jumanne Muliro kuhusiana na tuhuma hizo amesema ZCO anamamlaka ya kuchukua jarada lolote katika mkoa wake kwa ajili ya kulipitia na kutolea maelekezo pale inapobidi, ndiyo maana analo ofisini kwake.

“Ndugu mwandishi wewe sio wakwanza kuulizia jarada hilo, kwa vile malalamiko yamekuwa mengi nakuahidi nitafatilia  kinachoendelea ili tujue nini kinakwamisha”. Amesema Kamanda Muliro.   

Habari za uhakika kutoka ndani ya kituo hicho zinadai kuwa kiongozi mwingine anayeratibu zoezi la kukwamisha  upelelezi ni Kamisha Mstaafu wa jeshi hilo Linus Vicent Sinzumwa ambaye  pia ni mpangaji anayendesha shughuli zake za kibiashara kwenye moja ya maduka yaliopo kwenye eneo hilo.

Kamisha huyo mstaafu anamiliki duka linaloitwa Leila Store ambalo limesheheni vinywaji laini na vikali inadaiwa kuwa amekuwa akishinikiza kwa kuwapa maagizo mazito polisi wanaofanya upelelezi juu ya sakata hilo.

Baada ya kupigiwa simu na mwandishi wa habari hizi juu ya tuhuma hizo amekanusha vikari kwamba yeye hajawahi kufanya hivyo na kama wameshindwa kufanya upelelezi ni uzembe wao.

“Mimi siwezi kuwazuia polisi kufanya kazi yao, kama wameshindwa kufanya upelelezi wa jambo hilo hao ni wazembe wanastahili kuwajibishwa” amesema (CP) Mstaafu Sinzumwa.

Mmoja wa wanafamilia zinadai kuwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo mzee Wilson Kiguha Chacha sasa ana haha huku na kule kuhakikisha jinai hiyo haifikishwi Mahakamani kwa lengo la kuficha uovu huo.

Mwanafamilia huyo ambaye jina linahifadhiwa amesema kuwa hivi sasa Mzee Chacha amekuwa akifanya mawasiliano na viongozi mbalimbali na wakati mwingine viongozi hao hufika nyumbani kwa ajili ya mazungumzo akiwataka wamsaidie jambo hilo lisifikishwe Mahakamani.

“Hapa nyumbani magari ya viongozi mbalimbali yanapishana kila uchao na maongezi ni jinsi gani ya kuhakikisha suala la uvunjaji na kuiba mali za bar ya Big Mountain kinyume cha sheria halifikishwi Mahakamani na kwamba liishe kinyemela ili vijana wake waliohusika kufanya tukio hilo wawe huru” amesema mwanafamilia huyo.

“Unajua suala hili linashughulikiwa katika kituo cha polisi Stakishari na ndugu zangu hawa walikamatwa kwa RB namba STK/RB/12887/2022 kimsingi wenzangu walihusika, hivyo Mzee kila mara anazungumza na viongozi wakubwa ili kupindisha ukweli wa jambo hili ili waonekane hawakuhusika” amesema mwanafamilia huyo.

Amesema " Ukitaka kuamini kuwa walihusika mtafuteni mwenyekiti wa serikali ya mtaa ambaye kabla ya uhalifu huo mjukuu wa Mzee huyo  Godfrey  Chacha alimpelekea barua ya kusudio la kuvunja bar hiyo, ambapo mwenyekiti huyo naye ametoa maelezo Polisi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mzee Wilson Kiguha Chacha amesema kuwa hajakutana wala kuzungumza na kiongozi yeyote mkubwa wajeshi la Polisi wala taasisi yoyote ya Serikali na kwamba alimtaka mwandishi wa habari hizi amtaje mwanafamilia huyo ili amshughulikie haraka iwezekanavyo.

“Naomba unitajie huyo mwanafamilia anayetoa siri hizi kuwa mimi naongea na viongozi wakuu wa jeshi la Polisi kuhakikisha napindisha ukweli wa jambo hili ili nimshughulikie maana ni muongo hakuna ukweli wowote wa hayo aliyokuambia” amesema Mzee Chacha huku akifoka kwa hasira.

Hata hivyo wapangaji wake katika kiwanja hicho huko Banana wameiomba Serikali kuchunguza kwa umakini namna Mzee huyo alivyojimilikisha eneo hilo kwani inadaiwa lilikuwa ni mali ya Wizara ya Kilimo na Uvuvi.

Alipotafutwa mmiliki wa bar ya Big Mountain alielekeza atafutwe wakili wake, na alipotafutwa wakili wake Frank Chundu amesema wao wanasubili maamuzi ya jeshi la polisi kupeleka kesi Mahakamani.

Waliokamatwa na kuhojiwa na Polisi hadi sasa ni Godfrey Chacha ,Joseph Nyagare, Michael Julius Chacha, Amosi Chacha, Elizabeth Kiguha, Ramadhani Salehe (Sheta), Amiri Kaswe(White) na Josephat Mlaki ambao ndio wanamiliki wa mtambo uliotumika kuvunja.

Wengine ni  Ally Mbulu na Jafari Mbulu ambao ni wamiliki wa kampuni ya udalali inayoitwa Mak Auctioneers Company  LTD waliopewa kandarasi ya kuvunja bar hiyo na wakili wa Mzee huyo Juvenalis Motete. 

No comments