DIWANI MWANAMKE AMWANGUKIA RAIS SAMIA UTHAMINI WA FIDIA
Na Dinna Maningo, Rorya
DIWANI wa Viti Maalum Tarafa ya Girango wilayani Rorya mkoa wa Mara kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM),Hellena Ezekiel Magige amemuomba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuingilia kati zoezi la uthamini wa fidia linalofanyika Kitongoji cha Begi na Kiwandani Kata ya Koryo.
Diwani huyo amesema wathamini wamegoma kufanya uthamini wa ardhi badala yake wanafanya uthamini wa vitu pekee vilivyoendelezwa juu ya ardhi kwa madai kuwa wananchi walivamia ardhi ya shamba la mifugo (Utegi Dairy Farm) hivyo hawawezi kufanyiwa uthamini wa ardhi.
"Rais Samia wewe ni mwanamke mwenzetu tunakuomba uingilie kati mgogoro wa uthamini Kitongoji cha Begi na Kiwandani ili sisi viongozi wanawake tuendelee kuaminiwa katika uongozi, lisipotatuliwa hili watu wakaondolewa bila kulipwa fidia ya ardhi sisi wanawake tutapuuzwa na wananchi hawatatuamini wanawake katika uongozi" amesema Diwani Hellena.
Amesema ardhi isipofanyiwa uthamini hawatalipwa fidia na watakaoathirika ni wanawake na watoto kwani huwenda wanaume wakakimbia familia zao kwenda mbali kutafuta kazi kutokana na uthamini wa fidia kutofanyika kwa haki utakaopelekea malipo kidogo.
Amesema katika vikao vya Baraza la Madiwani haikuwahi kuibuka hoja yoyote kwamba Kitongoji cha Begi na Kiwandani vipo ndani ya shamba la mifugo.
"Nachofahamu Kitongoji cha Begi na Kiwandani vipo nje ya Farm, na walituambia watachukua vitongoji hivyo, wakasema kwenye vikao watatathmini ardhi ambayo ipo tupu na vitu endelevu.
"Nasikitika baada ya tathmini kuanza wameacha kupima ardhi wanahesabu vitu vilivyo tu juu ya ardhi. Ukiangalia hali ya watu wa Vitongoji hivi shughuli yao kubwa ni kilimo wanaposema hawatafanya uthamini wa ardhi wakati ardhi hiyo ndiyo inayowaingizia kipato wananchi, wanasomesha watoto kutokana na kilimo sasa wataishije?
"Kuna watu wanaishi kule ni wazee, Yatima, Walemavu wa viungo ambao ukiwaondoa bila kuwalipa ardhi utawaingiza katika dimbwi la umasikini na maisha yao yatakuwa ya mateso.
Diwani huyo anasema wapo wananchi walichukua mikopo na dhamana yao ni ardhi ambapo hurejesha mikopo hiyo kutokana na mazao wanayovuna na kuuza na hivyo kupata pesa ya kurejesha mikopo.
Post a Comment