WENYEVITI WASEMA SERIKALI YA RORYA IMEKIUKA MAKUBALIANO UTHAMINI WA FIDIA
>>Wasema kikao cha Julai, 14, 2023, kilichoketi ukumbi wa Halmashauri ya Rorya walikubaliana wananchi wafanyiwe uthamini wa ardhi na kila kilichoendelezwa kwenye ardhi.
>>Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa DC Chikoka
>>Washangaa Serikali ilivyowageuka na kukataa kufanya uthamini wa ardhi kwa madai kuwa wananchi walivamia ardhi ya shamba la mifugo ( Utegi Dairy Farm).
Na Dinna Maningo, Rorya
KUFUATIA kuwepo na sintofahamu juu ya zoezi la uthamini wa fidia linaloendelea katika Kitongoji cha Begi na Kitongoji cha kiwandani Kijiji cha Majengo Kata ya Koryo Wilayani Rorya Mkoani Mara, Venyeviti wa Vitongoji, Kijiji wamesema uthamini unaofanyika umekiuka makubaliano ya kikao.
Mwandishi wa DIMA ONLINE akiwa katika Kitongoji cha Begi na Kiwandani alielezwa na viongozi hao kwamba kitendo cha Serikali kukataa kuwafanyia waanchi uthamini wa ardhi ni ukiukwaji wa makubaliano baina yao na viongozi wa Serikali ya wilaya katika kikao kilichoketi Julai, 14, 2023.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Majengo Kata ya Koryo Wilayani humo Samson Daud Ogoya anasema Serikali ya Wilaya ya Rorya imekiuka makubaliano ya kikao kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya kilichoitishwa na mkuu wa wilaya hiyo Juma Chikoka.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Majengo Kata ya Koryo Wilayani humo Samson Daud Ogoya
"Julai, 14, mwaka huu tuliitwa kwa mkuu wa wilaya, tulikaa kikao Halmashauri, kikao hicho alikuwepo DC, DAS, DED, DSO, Mbunge, Mwenyekiti na Katibu wa CCM wilaya, Wenyeviti wa vijiji, Vitongoji ambavyo wananchi wanafanyiwa uthamini, Madiwani wa maeneo husika na Watendaji wa Vijiji na Kata maeneo.
"Kwenye kikao tuliambiwa kuwa wananchi wa Vitongoji vinavyopakana na shamba la mifugo ( Utegi Dairy Farm) wanatakiwa kuhama kwamba ni maelekezo ya Serikali, tukazungumza mwafaka ukawa wananchi wafanyiwe uthamini ardhi ipimwe na vitu vilivyo juu ya ardhi kisha watalipwa na kupisha maeneo kwa ajili ya uendelezaji wa shamba la mifugo.
"Nachojiuliza hivi maelekezo ya Serikali hayanaga utaratibu? kwasababu nilitegemea baada ya kikao hicho sisi wananchi tungepata muda ili tulijadili kwenye mkutano wa wananchi ili nao watoe maoni yao.
Anasema" Nilipotaka kufanya mkutano wa wananchi watu wakiwa wameshafika mkutanoni ili niwaeleze kilichojili kutoka kwa viongozi wa Serikali wilayani, DC akapata taarifa kuwa nafanya mkutano, ile tunataka kuanza kikao Polisi hao nikakamatwa mimi na Diwani tukapelekwa kituoni.
"OCD alikuja mkutanoni akatukamata, mkutano haukufanyika, tukapelekwa kituoni baadae OCD akasema tujidhamini akasema tumefunguliwa jarada la uchunguzi na tunachunguzwa
"Mwisho wa siku niliitwa halmashauri DC akaniambia kuwa hili swala ni agizo kutoka makao makuu, ndo kama hivyo unavyoona linafanyika wanavyotaka wao"anasema Samson.
Samson anasema kuwa Kitongoji cha Begi na Kiwandani ni vya asili sio eneo la shamba la mifugo na kwamba kuna wazee ambao waliishi maeneo hayo tangu wakati wa mkoloni.
"Watu wameishi kwenye maeneo hayo miaka ya 1800 kabla hata Serikali haijaanzisha mfumo wa Vitongoji, watu wakazaana mpaka sasa, mfano Mzee Owenga, Obade na wengine.
"Mwaka 2018 wakati Rais Mstaafu Hayati Magufuli akiwa hai watu wa Serikali walikuja kutambua mipaka ya Farm, afisa ardhi mkoa, wilaya na wataalam wengine na mimi nilikuwa mwenyekiti wa Kijiji, tukazunguka nao kuanzia Kitongoji changu tulipofika Kitongoji cha Begi na Kiwandani kukawa na changamoto.
"Watu wa Jeshini walikuwa wanataka wachukue eneo kwenye hivi vitongoji baada ya kuwepo mvutano kati ya wananchi na mwekezaji, Serikali ikachukua shamba ikawapa Wanajeshi kuwa walinzi wa hilo shamba.
"Tulivutana sana baadae afisa ardhi mkoa aliyekuwepo akasema hati haiwezi kutolewa kwenye eneo la mgogoro akawaambia nendeni TAMISEMI ili ikiwezekana hivyo vitongoji watu wapewe fidia wahamishwe.
"Majuzi tena tukasikia wamerudi tuliitwa Wilayani ila kabla alikuwa amekuja Waziri wa ardgi akasema tulivamia tukasema hatujavamia na hatukushirikishwa, akasema kama hamjashirikishwa kwa sasa mtashirikishwa lakini imekuwa tofauti"anasema Mwenyekiti wa Kijiji.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Begi katika Kijiji cha Majengo, Christian Odudo Othiong'o anasema "Tarehe 13, Julai, 2023 nilipigiwa simu na Mtendaji wa Kijiji akaniambia natakiwa kuhudhulia kikao tarehe 14, ofisi ya mkuu wa wilaya.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Begi katika Kijiji cha Majengo, Christian Odudo Othiong'o
"Nilienda Wilayani tukafanya kikao kule Halmashauri, Mwenyekiti wa kikao alikuwa DC, tuliuliza kuhusu uthamini utakavyokuwa, maana watu wa ardhi walisema ardhi haitalipwa, Mbunge akasema kweli inabidi watu wa ardhi waseme ardhi itafidiwaje.
"Wajumbe tukaambiwa tutoke nje wajadili, akabaki mbunge na viongozi wa wilaya kujadili swala hilo, baadae wakatuita wakasema tumekubaliana ardhi italipwa na mali zilizopo juu ya ardhi tukatoka pale vizuri tukiwa tumekubaliana.
Mwenyekiti huyo anaongeza " Ilipofika tarehe 16 mwezi huo timu kutoka Wilayani wakiwemo watu wa ardhi walikuja wakasema tuitishe mkutano vitongoji viwili Begi na Kiwandani ili watoe elimu kuhusu uthamini, tukaitisha watu walihudhulia wengi mpaka na watu wa Ikulu walikuwepo.
"Walisema wao wenyewe kuwa ardhi itapimwa pamoja na vitu vingine vilivyo juu ya ardhi. Ilipofika jumanne tarehe 25, zoezi likaanza la kuhesabu na kupima nyumba, wakahesabu mji wa 1-3, nikawauliza watu wa msafara mbona ardhi hampimi? wakasema ardhi tupu haipimwi mpaka iwe na vitu.
"Wakasema hata kama ardhi yako ni ekali moja na mwingine ana ekali kumi malipo kiwango ni kimoja kitakacholipwa kama fidia ya maendelezo" anasema Christian.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiwandani Onunda Agongo Kimwele anasema kitendo cha wananchi kutofanyiwa uthamini wa ardhi yao kimewapa hofu na na kukosekana kwa amani kwakuwa wananchi wanawatuhumu kuwa wamewauza.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiwandani Onunda Agongo
" Zoezi hili jinsi linavyoendelea kwenye Kitongoji changu sina amani na wananchi kwasababu wanasema sisi kama Serikali tunajua na tumewauza, wanaweza kututoa roho Tunaishi mashakani kutokana na utaratibu uliotolewa na mkuu wa wilaya na hawa wathamini wamekiuka utaratibu.
Onunda anazidi kueleza" Tulianza nao vizuri tukazunguka nao tukawapa ushirikiano lakini kadri tulivyoenda mbele kukaibuka changamoto ya kutopima ardhi baada ya kukataa kupima ardhi ya mwananchi mmoja Kethi Mjee, wakasema wao hawahusiki na kupima ardhi na ardhi ambayo haina kitu haitalipwa isipokuwa vilivyopo juu ya ardhi.
"Waliendelea na msimamo huohuo kukatokea mtafaruku, na sisi viongozi tukaona utaratibu unaofanyika sio ni tofauti na kilichokubaliwa kwenye kikao ofisi ya DC tarehe 14 na kwenye mkutano wa wananchi tarehe 16, Julai, 2023.
"Sisi kama Serikali Wenyeviti wa Vitongoji husika tukasema kama zoezi linaenda hivi bora tustishe zoezi, tukastisha tukaenda kulalamika ofisi ya CCM wilaya,tukakutana na viongozi wote kuanzia ngazi ya Kata, Madiwani wawili, Mwenyekiti wa Kijiji, wa Vitongoji husika na hao wathamini wakaja tukakaa kwenye kikao tukazungumza.
" Tukaridhiana, Katibu wa CCM wilaya akatoa maelekezo akawaambia waende wapime kila kitu cha mtu iwe ardhi ambayo haina kitu wapime wala wasiache kitu chochote, tukaridhiana tukaondoka.
Onunda anasema "Wathamini walivyofika kuendelea na zoezi walikataa tena wakasema wao hawapimi ardhi, nikawaambia mbona Katibu wa CCM wilaya ametoa maelekezo na akampigia simu Mbunge mkiwepo nae akasema iwe hivyo mpime na ardhi kwanini sasa mnakataa mnatengua maamuzi?
"Tukawaambia kama mnatumia mabavu na utaratibu wenu bora wenyeviti tusihusike kwasababu wananchi wanaona sisi tumehusika kwa namna moja au nyingine. Wakaendelea na zoezi wao wenyewe wakiwa na mtendaji wa Kata bila kuwa na mwenyekiti wa Kijiji wala Wenyeviti wa Vitongoji.
Anasema kuwa, kutokana na kutokuwepo kwa maelewano katika uthamini huo alitegemea zoezi lingestishwa kwa muda ili kujadili na kutafuta suluhu lakini Serikali ya Rorya haikujali wala kusikiliza malalamiko ya wananchi badala yake wameendelea na zoezi bila kujali watu wapo majumbani au hawapo.
Rejea
>>> Julai, 27, 2023, wananchi wa Kitongoji cha Begi na Kitongoji cha Kiwandani katika Kijiji cha Majengo, Kata ya Koryo, wilaya ya Rorya mkoani Mara, wanaoishi jirani na shamba la mifugo (Utegi Dairy Farm) waliandamana ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya.
Post a Comment