GGML KUJENGA UWANJA WA SOKA WA KISASA
Na Andrew Charle Dar es Salaam
KAMPUNI ya uchimbaji madini ya Geita Gold Mine Limited (GGML), ya Mkoani Geita inatarajia kuwa na uwanja mkubwa wa kisasa wa soka ambao utaingiza watazamaji zaidi ya 20,000 unaojengwa eneo la Magogo.
Hayo yamebainishwa na Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa GGML, Laurian Pima wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa aliyetembelea banda hilo la madini Julai 6, 2023 kwenye maonesho ya 47 ya biashara kimataifa sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Amemhakikishia Naibu Waziri wa Madini kuwa wanajenga uwanja huo kwa lengo la kusaidia kuibua vijana lakini pia kuiwezesha timu ya soka ya Geita Gold Fc kutumia uwanja huo pamoja na timu zingine zinazofika Geita.
"Uwanja huu unajengwa kwa awamu na unagharimu Bilioni 6. Ukikamilika utakuwa miongoni mwa uwanja mkubwa na kisasa ukiingiza mashabiki 20,000 ambapo utakabidhiwa Halmashauri ya Geita.
"Lakini pia utakuwa na maeneo mengine ya masuala ya michezo na maeneo ya kuegesha magari." Amesema Pima.
Aidha, Pima amesema uwanja huo pia utakuwa msaada mkubwa kwa klabu ya Geita Gold FC ambao wanawadhamini msimun wa pili sasa kwa mafanikio makubwa.
"Tunataka benchi la ufundi lifanye yao nyumbani. Tumeweza kudhamini timu changa ya Geita na inafanya vizuri.
Pia uwanja huu utakuwa ni kichocheo cha uchumi wa Geita.
"Kauli mbiu yetu ni 'Jamii inayotuzunguka inufaike kutokana na uwepo wa shughuli zetu', uwanja huu ni kielelezo muhimu ya Kauli mbiu hii.". Amesem Pima.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Kiruswa amewapongeza GGML kwa uwekezaji wao ikiwemo kurejesha fadhila kwa jamii.
GGML ni miongoni mwa kampuni kubwa ya uchimbaji madini ya dhahabu ambapo wameanza uwekezaji tangu mwaka 2000 na sasa kuwa na zaidi ya miaka 20 ya ufanyaji kazi.
Post a Comment