HEADER AD

HEADER AD

JAMII YATAKIWA KUTOJENGA MAKAZI KARIBU NA HIFADHI ZA WANYAMAPORI


Na Jovina Massano, Musoma

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeitahadharisha jamii kuacha tabia ya kujenga makazi yao karibu na hifadhi za wanyamapori zikiwemo shughuli za kibinadamu ili kujiepusha na hatari za wanyama wakali.

Tahadhali hiyo imetolewa na Mhifadhi mkuu anaesimamia kitengo cha dawati la ujirani mwema kutoka TAWA PC Twaha Twaibu wakati akizungumza na DIMAONLINE ikiwa ni moja ya uelimishaji kwa jamii hasa inayoishi pembezoni mwa mbuga hizo.

    Mhifadhi mkuu anaesimamia kitengo cha dawati la ujirani mwema kutoka TAWA PC Twaha Twaibu

Aidha PC Twaha ameitaka jamii kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa Wanyamapori ili kuepuka athari zitokanazo na wanyama wakali na waharibifu kama Tembo,Nyati,Mamba,Kiboko na wengineo.

Amesema baadhi ya maeneo hapa nchini yalikuwa ni mapitio ya Wanyamapori kipindi cha nyuma na wanyama hao huwa na tabia ya kurejea katika maeneo hayo haswa Tembo hivyo jamii inatakiwa kuwa makini kwa kutowakaribia.

"Kuna wakati wanyama wanafika hadi kwenye makazi ya watu, ukiona mnyamapori kwenye mazingira unayoishi toa taarifa kwa haraka kwa viongozi wa maeneo unayoishi ili hatua za kiusalama ziweze kuchukuliwa na wataalam wa Wanyamapori ambao ni TANAPA na TAWA.

"Tumesomea namna ya kuwadhibiti pia kuna tabia ya baadhi ya wananchi kutaka kupiga picha nao kitendo hicho kinahatarisha maisha yao", amesema Twaha.
 
Amewashauri wananchi wenye umri mkubwa na waliotumia vilevi kutokufukuza wanyama hao na kutofanya shughuli za kibinadamu katika mapitio ya Wanyamapori.

Sanjari na hayo Mhifadhi Twaha kwa niaba ya Kamishna  wa Uhifadhi TAWA amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika Utalii,Uhifadhi na ndie aliezindua Jeshi la Uhifadhi (USU)wakati alipokuwa Makamu wa Rais.

TAWA kupitia kitengo chake cha uelimishaji imefanikiwa kutoa elimu kwa wananchi wapatao laki Saba na sita elfu na mia tatu  kupitia mikutano 1925 katika maeneo mbalimbali.

Nae Afisa Wanyamapori kutoka TAWA Joseph Mnyai ameelezea faida zinazotokana na Uhifadhi kupitia uwindaji wa kutalii na utalii wa picha kuwa ni upatikanaji wa fedha za kigeni.

Fedha hizo hupelekwa kuchangia shughuli za maendeleo katika jamii zilizopo kandokando mwa mbuga hizo yakiwemo mapori ya akiba tengefu na maeneo ya ardhi oevu kwa kuzingatia utaratibu wa mamlaka.




              

No comments