HEADER AD

HEADER AD

WANAWAKE WANUFAIKA WA TASAF WAJITOKEZA KULIMA BARABARA WANAUME WAKACHA


Na Ragina Mwera, Tarime

IMEBAINIKA kutokuwepo kwa usawa katika shughuli ya ulimaji wa barabara za mitaa na Vijiji zinazotekelezwa na kaya masikini zinazonufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Wanawake wameonekana kuwa na ushirikiano na kujitokeza kwa wingi kulima barabara huku idadi ya wanaume ikiwa ndogo licha ya fedha zinazotolewa kuwanufaisha wanafamilia wote wanaonufaika na Mpango wa kunusuru kaya masikini.

Julai, 7, 2023, Mwandishi wa DIMA Online ameshuhudia kuona wanawake wengi kuliko wanaume wakiwa wamejitokeza kulima barabara katika mtaa wa Biambwi Kata ya Bomani wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Wanawake wamesema kuwa hujitokeza kwa wingi kulima barabara kuliko wanaume kwakuwa barabara ni muhimu kwao wanapokuwa wakipita kwenda kutekeleza majukumu mbalimbali.

Mjumbe wa Serikali ya mtaa wa Biambwi ambaye pia ni msimamizi wa wanufaika wa kaya masikini Isabela Jackson amesema  wanawake ndiyo wanaowajibika katika shughuli nyingi za kimaendeleo.


"Nasimamia mradi wa kulima barabara unaotekelezwa na kaya masikini wanaonufaika na fedha za TASAF.

"Wanawake ndiyo wanaowajibika na familia, niwatunzaji wa familia na ndiyo maana unakuta misaada mingi inapotoka wamama ndiyo wanakuwa wengi kujitokeza wao ndio walinda miji"amesema Isabela.

Wema Gosori ameongeza kusema " Katika zoezi hili la urekebishaji wa barabara za mitaa, akina mama hawana usumbufu kujitokeza kufanya maendeleo kwasababu wao ndiyo wachakalikaji na ndiyo wanahangaika kutengeneza hizi barabara.

"Wanawake ni waelewa wanaojitokeza kuja kuungana pamoja kufanya maendeleo. Wanaume wanaojitokeza ni wachache sana ukilinganisha na wanawake, tunaendelea kuwahamsisha wanaume wajitokeze kwa wingi kulima barabara wasiwaache tu wanawake ndiyo wawajibike" amesema Wema.

Baadhi ya wanaume wamesema kuwa wanawake wamekuwa wakibebeshwa mzigo wa maendeleo licha ya fedha kuwanufaisha wanaume lakini inapofika kwenye shughuli za uzalishaji wanawake ndiyo wanahamasika kuliko wanaume.

Benedicto Simfukwe maarufu Ninja amesema " Mimi ni fundi wa upimaji wa hizi barabara. Tunamshukuru Rais Samia kwa kuendeza huu mradi wa TASAF ambao unawanufaisha kaya masikini.

"TASAF imesaidia sana hasa akina mama kwasababu ukiangalia tabia za wanaume wengi wa mkoa wa Mara wakishaoa wanawake ndiyo watafutaji watafute mboga, hata hapa kwenye hii kazi ya kulima barabara wanawake ndiyo wanajitokeza kwa wingi kuliko wanaume.

Benedicto ameongeza kuwa baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwanyanyasa wanawake kwani fedha zinapotolewa wanaume huchukua na kwenda kunywa pombe na hivyo familia kubaki kwenye tabu.


No comments