HEADER AD

HEADER AD

HOSPITALI YA WILAYA YA MASWA YAANZA KUTOA MATIBABU KWA WATOTO NJITI

>>Ni baada ya Serikali, Wadau kutoa vifaa tiba vya kisasa

>>Watoto Njiti walipoteza maisha kwa kukosa huduma

>>Sasa hali ni shwari waanza kupata huduma

Na Samwel Mwanga, Maswa

HOSPITALI  ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imeanza kutoa matibabu kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati “Watoto Njiti” baada ya kupata vifaa tiba vya kisasa viliyotolewa na Serikali na Wadau mbalimbali wa Afya ikiwemo Taasisi ya Dorris Mollel Foundation.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya hiyo, Dk. James Bwire, ameyasema hayo Julai, 13, 2023 mbele ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalim aliyetembelea Hospitali hiyo na kufika wodi ya kulaza watoto hao ili kujionea jinsi huduma zinazotolewa kwenye wodi hiyo.

Waziri wa Afya,Ummy Mwalim(mwenye kilemba kichwani)akifurahia jambo na baadhi ya Viongozi wa wilaya ya Maswa wakati alipote mbelea Hospitali ya wilaya hiyo.

Amesema baada ya kupata vifaa hivyo waliviweka kwenye wodi maalum ambayo inawahudumia watoto hao ili waishi kama wengine.

Amesema kuwa changamoto ilikuwa kubwa kwa sababu wengi wa watoto hao walikuwa wanapoteza maisha kutokana na ukosefu wa vifaa tiba katika hospitali hiyo ila kwa sasa hali ni shwari na wameweza kuokoa maisha ya watoto hao wanaofikishwa katika hospitali hiyo.

“Moja ya changamoto tuliyokuwa tunaipata kutokana na vifo vya watoto katika hospitali ya wilaya yetu ni hawa watoto njiti na hii ilitokana na kutokuwa na vifaa tiba kwa ajili yao, hivyo wengi wao tulikuwa tunawapatia rufaa kwenda hospitali ya Bugando jijini Mwanza.

“Kuzaliwa njiti si mkosi kama baadhi ya watu wanavyodhani kwenye jamii sasa matibabu yanapatikana hapa na tangu tumeanza huduma hii tumekuwa tukipata watoto wa namna hii kutoka hospitali nyingine za wilaya katika mkoa wa Simiyu kama vile wilaya za Meatu,Itilima na wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga,”amesema Dk. Bwire.

Amesema  watoto wanaozaliwa kabla ya wakati hasa wale wanaozaliwa na uzito mdogo zaidi chini ya gramu 500 wanahitaji vifaa maalum ili waweze kuishi wakiwa hospitalini.

     Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Maswa,Dk James Bwire(kulia)akitoa maelezo kwa Waziri wa Afya,Ummy Mwalim(kushoto)juu ya matibabu ya Watoto Njiti huku Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda(aliye kati)akisikiliza.

Naye Waziri Ummy ameipongeza wilaya ya Maswa kwa kuweza kutoa huduma hiyo ya matibabu kwa watoto Njiti kwa kuokoa maisha yao.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu imejipanga kuhakikisha inaboresha huduma ya Afya ya Mama na mtoto kwa lengo la kukomesha vifo vinavyotokana na masuala ya uzazi.

     Waziri wa Afya, Ummy Mwalim(mwenye kilemba kichwani)akizungumza na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI mara baada ya kuitembelea hospitali ya wilaya ya Maswa.

Amesema kwa sasa bajeti ya dawa katika hospitali hiyo imeongezeka kutoka kiasi cha Tsh.Milioni 240 hadi Tsh Bilioni Moja.

"Hizi huduma za watoto njiti zilikuwa zinapatikana katika hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyoko Jijini Mwanza sasa mambo yote ni hapa Maswa,nimekuta katoto kachanga amezaliwa na uzito wa gram 700 lakini ndani ya siku tatu madaktari wetu wamepambana na sasa anauzito wa gram 1,100,"

"Lengo la serikali yetu ni kuhakikisha Mama mjamzito atoke salama na kachanga kake maana kila mzazi anataka kufurahia uzazi wake.

"Uzazi ni baraka,uzazi ni furaha na neema kwa familia na jamii, tutaendelea kulifanyia kazi kama tulivyoleta vifaa tiba vya kisasa katika hospitali hii pamoja na jitihada za mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki ,Stanslaus Nyongo"amesema.

Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki,Stanslaus Nyongo amesema kuwa ataendelea kupambana katika serikali kwa kujenga hoja ili kuhakikisha sekta ya afya katika wilaya hiyo inaboreshwa kwa kupatikana kwa huduma vifaa tiba vya kisasa pamoja na madawa ili wananchi waweze kupata matibabu.

Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki,Stanslaus Nyongo(aliyenyoosha mkono)akiteta jambo na Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu (aliyekati mstari wa mbele)wakati wakitoka kwenye Wodi ya Watoto Njiti katika Hospitali ya wilaya ya Maswa.

Judith Madaha ambaye amejifungua watoto wawili njiti na anaendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo amesema kuwa watoto wa namna hiyo huhitaji maziwa ambayo ni ghali mno.

Aidha, ameiomba serikali kuelimisha jamii kuanzia wanafunzi hadi kushirikiana na wizara ya Afya ili kuanzisha mtaala wa kusaidia elimu ya watoto njiti kwenye mtaala wa Tanzania ili tupate wananchi wenye uelewa wa jinsi ya kujikinga ama kujisaidia ili wasipate mtoto njiti.

“Na hii itasaidia na hata akija mtu kupata mtoto njiti asione kuwa si riziki au mtoto huyu hatoishi na watoto njiti wanaishi tukiwapatia maisha bora,” amesema.

Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka duniani watoto milioni 15 wanazaliwa njiti, yaani ujauzito ukiwa haujatimiza wiki 37 wakiwa na uzito mdogo na uwezo mdogo wa kumudu maisha yao.
  
Waziri wa Afya,Ummy Mwalim(mwenye kilemba kichwani)akifurahia jambo na baadhi ya Viongozi wa wilaya ya Maswa wakati alipote mbelea Hospitali ya wilaya hiyo.

No comments