HEADER AD

HEADER AD

TECLA YATOA MSAADA KWA WATOTO 50 WENYE ULEMAVU

>>DC Sima asisitiza wazazi kuwapeleka watoto shule

>> Asema watoto wenye ulemavu kutoandikishwa shule ni kuvunja sheria

Na Alodia Dominick, Bukoba

SERIKALI wilayani Bukoba mkoani Kagera imesema wazazi wanapaswa kuwapeleka watoto wao kuanza shule ya msingi kwani kutofanya hivyo ni kuvunja sheria na kuwakosesha haki ya msingi ya kupatiwa elimu watoto wao.

Mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima ameyasema hayo Julai 12, 2023 alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya ugawaji wa vifaa mbalimbali vya shule ikiwemo viti mwendo na baiskeli za mataili matatu kwa wanafunzi wenye ulemavu  wapatao 50 kutoka shule sita za wilaya ya Bukoba vilivyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la TECLA linalohudumia watu wenye ulemavu.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Sima akigawa misaada kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, vitu vilivyogawiwa ni pamoja na viatu, sale za shule viti mwendo na baiskeli za mataili matatu

“Kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakikiuka sheria ya kuwapeleka watoto wao kuanza shule ya msingi, kwa mzazi yeyote ambaye atabainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria, Serikali yetu imeweka mipango mizuri kwa ajili ya watoto wetu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa vya kutosha" amesema Erasto.

Mtendaji mkuu wa shirika la TECLA Mugisha Kasaju amesema kuwa, wamegawa viti mwendo na baiskeli zenye mataili matatu zipatazo tano, jozi za viatu 38 na sale za shule 40 vyenye thamani ya Sh17 milioni na kuwa wanafunzi waliopokea msaada huo ni kutoka katika shule za msingi, Mgeza viziwi, Mgeza Mseto, Tumaini, Rubale, Ryamaholo na Buzi.


Mwalimu mkuu shule ya msingi Mgeza Viziwi Benson Rwechungura amesema Wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu wana mwamko mdogo wa kuwapeleka watoto shule jambo ambalo linasababisha watoto hao kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu.

“Tunakumbana na changamoto ya wazazi kutokuwa na mwamko mdogo wa kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu, mfano watoto wanapofunga shule baadhi ya wazazi hawaji kwa wakati kuwatafuta watoto wao kuwapeleka nyumbani.

"Wanapofungua shule baadhi ya wazazi  wanachelewa kuwarudisha shule kwa madai kwamba  wanaanza kuwahudumia vifaa vya shule wale watoto wao ambao si wenye ulemavu” amesema Mwalimu Rwechungula.

Mmoja wa wazazi mwenye mtoto mlemavu Autropia Benedicto amesema, mtoto wake Merry Daudi (11) yupo darasa la awali shule ya msingi Mgeza Mseto ana ulemavu wa miguu kushikana na mikono miwili kupinda.

Amesema awali alikuwa anabebwa kutoka bwenini kwenda darasani lakini msaada huo wa kiti mwendo utamsaidia kupunguza adha ya kubebwa kila wakati.




No comments