HEADER AD

HEADER AD

MWEKEZAJI AWASHAURI WAKULIMA KUONGEZA UZALISHAJI KILIMO CHA ALIZETI

>>Asema mahitaji ya kiwanda Nyihita Sunflower Cooking oil Production ni tani 24 lakini wanapata asilimia 5 ya mahitaji

Na Boniface Gideon, Mara 

MWEKEZAJI wa Kiwanda chakuchakata zao la Alizeti Nyihita Wilfred amewaomba wakulima wa zao hilo mkoani Mara kuongeza uzarishaji ili kukidhi  mahitaji ya Kiwanda.

Mwekezaji  huyo mzawa anamiliki Kiwanda cha Alizeti kijulikanacho kwa jina la Nyihita Sunflower Cooking oil Production kilichopo katika Kijiji Nyanchabakenye Wilaya ya Rorya.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Nyihita amesema mahitaji ya kiwanda hicho kwa siku ni Tani 24 lakini kwasasa wanapata asilimia 5 tu ya mahitaji ya Kiwanda.

Nyihita Wilfred (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wake wakiwa na mafuta yanayochakatwa Kwenye kiwanda chake

Amesema kuwa aliamua kuanzisha uwekezaji huo kwaajili ya kuchakata zao la alizeti na kuwa mzalishaji mkubwa wa mafuta yatokanayo na alizeti lakini pia ameweza kufungua na kutoa ajira kwa vijana hatua ambayo amesema ni ya kujivunia kwa wakazi wa wlaya hiyo na wilaya jirani.

Nyihita amesema aliigeuza changamoto na kuwa fursa kwake kutokana na wilaya hiyo kutokuwa na kiwanda cha alizeti na hivyo kupata wazo la kuwekeza.

"Nilipata wazo la kuja kufanya uwekezaji wa kilimo cha alizeti wilayani Rorya ikiwa ni eneo ambalo halikuwahi kuwa na historia ya kilimo cha alizeti na niliamini kwamba malighafi zinapatikana kijijini na maendeleo makubwa na mapinduzi ya viwanda yanafanyika  vijijini.

"Nilianza kuwashawishi wakulima wenye mashamba ili waweze kulima na ni kweli wazo hili lilifanikiwa kwa asilimia 100 kwani wakulima walijitokeza na kuanza kulima kilimo cha Alizeti mwaka 2019.

Ameongeza "Ilipofika 2020 wakulima walianza kujiuliza maswali kwamba baada ya kulima mazao tutauza wapi? nikapata wazo kwa kutafuta wazo la soko na kujenga kiwanda. Baada ya kuanza ujenzi huo kiwanda hiki kilizinduliwa rasmi 2021 na  kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa  na ndio kikaanza kufanya kazi mpaka sasa" amesema.

Amesema anajivunia kuwa mwekezaji mzawa na mmoja wa watanzania ambao wanaweza kuzalisha fursa za ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo sambamba na kuwapatia soko la uhakika wakulima hatua ambayo imeleta mwamko wa wakulima wengi kujikita shambani tofauti na ilivyokuwa awali.

"Pamoja na hayo uwepo wa kiwanda hiki kimeweza kutengeneza fursa za ajira  kwa vijana wetu wa kitanzania  lakini pia kuongeza  uchumi wa mtu mmoja mmoja, kwahiyo tumeongeza wigo mpana kwa ndugu zetu wa Mara  kuweza kuongeza pato lao kupitia kiwanda hiki.

"Wakulima kuweza kupata soko la uhakika na kuuza malighafi zao hapa na pia kiwanda hiki kimeweza kuwa faida kwa nchi yetu ya Tanzania kwani tunalipa kodi na  zinasaidia kuleta maendeleo kwenye Taifa letu.

"Ni wito wangu kwa watanzania na wana Mara kujikita kwenye kilimo cha alizeti wakitumie kama fursa  na kuhakikisha tunasaidia kuinua uchumi wa Taifa letu lakini pia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja  ndani ya Tanzania kwa ujumla" amesisitiza.

Nyihita amesema ukubwa wa kiwanda hicho hauendani sawa na mali ghafi inayozalishwa mashambani ambayo imekuwa ni kidogo huku akiwaasa wananchi kuendelea kujikita katika kilimo hicho kwani tayari uhakika wa wapi watauza mazao yao upo hivyo ni suala tu la kuongeza uzalishaji.

"Uwezo wa kiwanda ni mkubwa tofauti na Malighafi inayoweza kupatikana, kwa misingi hiyo basi tunahitaji wakulima wajitokeze kwa wingi kulima  wakijua kwamba fursa ya soko la uhakika ipo ili waweze kusaidia kiwanda kuweza kuzalisha kwa wingi na kupata ukamilifu wa uhitaji wa mali ghafi.

"Sasa hivi wizara ya kilimo imeanzisha kilimo biashara, wazo hili linasaidia vijana wakitanzania na watanzania kwa ujumla kuweza kujikita kwenye kilimo. Kupitia wazo hili la kilimo biashara litasaidia watanzania kujiwekeza.

Ameongeza "Ni matumaini yangu kwamba kupitia kilimo biashara vijana wengi watajitokeza kulima zao hili ambalo litasaidia  kuongeza utoshelevu wa uhitaji wa malighafi"Amesema 

Mariam Hamis ni miongoni mwa wakulima na wanufaika wakubwa wa zao la alizeti, amesema wamekuwa wakijihusisha na uzarishaji wa zao hilo kwa muda mrefu lakini hawakuwahi kupata mafanikio kutokana na kukosa soko, hivyo kwasasa wanashukuru uwepo wa kiwanda hicho.

" Tumekuwa tukijihusisha na kilimo cha kawaida tu katika zao hili ili tupate pesa kwaajili ya kukidhi mahitaji ya familia lakini hata hivyo tumekuwa na changamoto ya muda mrefu wa kupata soko la uhakika kwajili ya kuuza mazao yetu yalikuwa yanaharibika.

"Lakini kwa sasa uwepo wa kiwanda hiki ni furaha kwetu wakulima kwasababu tayari tumepata uhakika wa kutosha kuhusu changamoto ya muda mrefu.

"Tulikuwa hatujui ni wapi tutauza mazao yetu baada ya kuvuna, tunashukuru sana mwekezaji kwa kuona changamoto hii na kuitatua katika wilaya yetu na sasa wakulima wote tumehamasika na tunanufaika vyakutosha na uwepo wa kiwanda hiki"  

Amesema vijana wengi hususani wa vijiji vinavyozunguka eneo la kiwanda hicho wamepata mwamko mkubwa wa kufanya kazi hususani za kilimo kutokana na uhakika wa soko la Alizeti.

"Vijana wengi tunafaidika na kunufaika na uwepo wa kiwanda hiki kutupatia ajira ambapo watu waliosoma na wasiosoma wameweza kuajiriwa kiwanda cha Nyihita Sunflower Cooking oil Production.

Mariam amesema kiwanda kimesaidia kupunguza upungufu wa ajira ambao bado ni tatizo katika nchi hivyo uwepo wa kiwanda hicho kimekuwa na manufaa kwa wananchi  wengi.


No comments