HEADER AD

HEADER AD

MILIONI 12 ZACHANGWA HARAMBEE UJENZI OFISI YA SERIKALI YA MTAA


Na Gustafu Haule, Pwani

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka (CCM)amewaongoza wananchi katika harambee ya kupata Sh .Milioni 12 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mailimoja "A" Halmashauri ya Mji wa Kibaha.

Katika harambee hiyo Koka ,amechangia kiasi cha sh .Milioni tatu ikiwa sehemu ya kuhamasisha wananchi na wadau wengine kujitokeza katika kuchangia ujenzi wa ofisi hiyo.


Harambee hiyo imefanyika Julai 05 kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na wananchi wanaoishi mtaa huo akiwemo Diwani wa Kata hiyo Ramadhani Lutambi.

Jengo la ofisi hiyo linahitaji zaidi ya Milioni 12 mpaka kukamilika lakini katika harambee hiyo mbunge alifanikiwa kukusanya zaidi ya  Sh.Milioni 4.2 na wananchi kuchangia fedha hivyo kufikisha Milioni 12 ambazo zitasaidia katika hatua ya kwanza ya upauaji.

Mbunge Koka ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau wengine katika kuhakikisha jengo hilo linakamilika huku akiagiza kuwafuatilia wananchi na wafanyabiashara waliopo karibu na eneo hilo.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha kwa harambee Koka amesema kuwa Serikali inadhamira kubwa ya kusogeza huduma karibu na jamii hasa kupitia ofisi za Serikali ya Mtaa.


Amesema kuwa,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa ya kuijenga nchi na yeye anashuhudia jinsi anavyohangaika kutafuta fedha huku na kule.

Ameongeza kuwa utafutaji wa fedha unaofanywa na Rais unalenga kujenga na kukamilisha miradi mikubwa nchi nzima lengo ni kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma kwa wakati na zenye ubora.

"Rais wetu Mama Samia anafanya kazi kubwa na anadhamira ya dhati kwa Taifa la Tanzania ndio maana tumeona bajeti imefikia zaidi ya Trillioni 41 tofauti na awali ilivyokuwa chini ya Trillioni 40,"amesema Koka

Amesema kama Rais anafanya mambo makubwa kiasi hicho ni vyema sasa wananchi, viongozi wa vyama vya siasa, wabunge na kada nyingine wakajitoa katika kumsaidia Rais katika kutatua changamoto za wananchi katika Mitaa husika.

Hata hivyo Koka amewaomba wananchi hao kuendelea kumuamini kama ambavyo walimchagua kwa ajili ya kuwatumikia huku akiomba ushirikiano ambao utasaidia kuleta maendeleo ya Mji wa Kibaha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mailimoja Yassin Mudhihir amesema kuwa kwasasa wanafanyakazi katika nyumba ya kupanga jambo ambalo limekuwa ni gharama kubwa katika kuendesha ofisi hiyo.


Mudhihir amesema kuwa kutokana na changamoto wanazopata Januari 2021, wananchi walishirikiana na ofisi yao ya Serikali ya Mtaa na hivyo kupata eneo kupitia George Semwaiko na Abdallah Kihoko.

Amesema baada ya kupata eneo hilo wakalazimika kuanza ujenzi Oktoba 2022  kwa gharama ya Sh .Milioni tatu huku fedha ya mbunge kutoka mfuko wa Jimbo ni Sh .500,000.

Diwani wa Kata ya Mailimoja A Ramadhani Lutambi amesema malengo yao ni kukamilisha ujenzi huo mwishoni mwaka huu ili kusudi wananchi wapate huduma katika mazingira bora.




No comments