MAKAMU MWENYEKITI : VIJANA WA HAMASA CCM MSITUMIKE VIBAYA
Na Gustafu Haule, Pwani
MAKAMU Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambaye pia ni Mhariri wa gezeti la Uhuru Selina Wilson, amewataka vijana wa hamasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM)Kibaha Mjini kuacha kutumika vibaya na wanasiasa wanaolenga maslahi yao binafsi.
Selina ametoa wito huo Julai 18 mwaka huu wakati akizungumza na vijana hao katika viwanja vya CCM Kata ya Tangini mahali ambapo vijana hao walikuwa wakijitolea kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Kata hiyo.
Amesema wapo wanasiasa ambao wamekuwa wakiwatumia vijana kuwa madalali wao kwakufanya shughuli za kisiasa na baada ya kufanikiwa wanawatupilia mbali.
Selina ameongeza kuwa vijana wanatakiwa kujitambua kwakujua hata wao wanahitaji kupata mafanikio lakini ili waweze kufikia mafanikio hayo lazima waweke msimamo wa kutotumika hovyo na wanasiasa wanaotanguliza maslahi yao.
"Mimi niwaombe vijana kuacha kutumika na hawa wanasiasa maana wengine wanawatumikisha tu halafu wakishinda katika hizo nafasi wanawaacha solemba na matokeo yake kila mwaka mnabaki palepale,"amesema Selina
Selina , amesema kuwa kama kuna mwanasiasa anahitaji kuwatumia katika shughuli zake ni vyema wakaungana kwa kuweka misimamo thabiti ambayo mwisho wa siku itawaletea manufaa katika maisha yao na hata katika maendeleo ya Jimbo lao.
Aidha ,Selina ametumia nafasi hiyo kukabidhi matofali 300 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo ambayo aliahidi katika harambee iliyofanyika Julai 02 chini ya Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka.
"Katika kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi ( CCM) na mimi leo nakabidhi matofali yangu 300 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa ofisi yetu lakini nitatoa Sh.100,000 kwa ajili ya kuwapa hawa vijana kununua maji wakati wakiwa wanafanya hii kazi ya kuchimba msingi wa ofisi yetu,"amesema Selina
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Tangini Anthony Milao, amemshukuru Selina kwa mchango wake mkubwa huku akisema wanaimani matofali hayo yatakuwa sehemu ya kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo.
Milao,ametumia nafasi hiyo kuwaomba wadau na viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitokeza kwaajili ya kusaidia kukamilisha ujenzi huo kwa haraka kwakuwa bila kuwepo kwa ofisi utekelezaji wa majukumu unakuwa mgumu.
Hatahivyo, kiongozi wa vijana wa hamasa wa CCM Kibaha Mjini Ally Gombati , amewashukuru viongozi wa CCM Kata ya Tangini pamoja na Selina kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa kwao.
Gombati, amesema vijana wa hamasa ni wazalendo na wapo tayari kwa ajili ya kujitolea kufanyakazi za CCM wakati wowote na sehemu yoyote hivyo amewaondoa shaka viongozi hao kuwa wanapokuwa na kazi yenye kuwahitaji ni vyema wakatoa taarifa kwa wakati.
Post a Comment