UMMY : KUPITIA BAHARI WANANCHI WATANUFAIKA NA FURSA YA UCHUMI WA BLUU
Na Boniface Gideon, Tanga
MBUNGE wa Jimbo la Tanga (CCM) Ummy Mwalimu amesema kuwa kupitia bahari wananchi Jijini Tanga watanufaika na fursa ya uchumi wa bluu kwa kujiongezea kipato katika ufugaji na kilimo.
Ummy ambaye pia ni Waziri wa Afya ameyasema hayo Julai, 17,2023 wakati alipotembelea miradi inayotekelezwa na Taasisi ya Tanga Yetu kupitia ufadhili wa Shirika la Botnar Foundation katika Jiji la Tanga huku akiwashukuru kwa kukubali ombi lake kutekelezwa miradi hiyo ambayo itasaidia kukuza uchumi wa bluu.
Waziri wa Afya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu (Kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa mkandarasi anayetekereza ujenzi wa Bustani za kapumziko Jijini Tanga.
Aidha Botnar foundation pia wamefadhili miradi ya Afya, Elimu na kujenga Forodhani ya Tanga.
Katika miradi hiyo jumla ya fedha zilizotumika hadi sasa ni kiasi cha T.sh Bilioni 5.65 zimetumika na kwamba zimewasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
Amesema kutokana na umuhimu wa uchumi wa bluu katika kukuza uchumi wa wananachi, Jiji hilo limejipanga kuwa kinara katika uzalishaji wa majongo bahari, unenepeshaji wa kaa pamoja na kilimo cha mwani kwa kutumia fursa ya bahari iliyopo kwenye Ukanda wa Pwani.
"Kwasababu mkoa wa Tanga una eneo kubwa la bahari na tayari mafanikio tumekwisha kuyaona hivyo tujipange kuongeza uzalishaji Ili tuweze kuwa vinara wa kutumia fursa za uchumi wa buluu kwa maendeleo ya watu wetu sambamba na nchi kupata mapato yake”amesema Waziri Ummy.
Amesema kutokana na uwepo wa fursa wanapaswa kulikumbatia zao la mwani kwa sababu ni zao ambalo kilimo chake sio kigumu zaidi na faida yake ni kubwa.
“Mimi kama Mbunge wa Jimbo la Tanga nitashirikiana na wadau Botnar Foundation kuendeleza kilimo cha mwani kikubwa tuwape elimu na ujuzi wananchi hususani wanawake ikiwemo kuwapa vitendea kazi ambayo vitasaidiaa kufanya vizuri katika kilimo cha Mwani na kutafuta masoko”Amesema Waziri Ummy.
Aidha amesema kwamba amejipa kazi maalumu ya kutangaza mazao makubwa matatu Tanga mjini kutokana na kwamba wanataka mwambao wa Tanga uwe maarufu kwa kuzalisha mazao ya Mwani,Majongoo Bahari na kunenepesha kaa.
Amesema kwamba hayo mazao matatu amevutiwa nayo na kama watawekeza kwenye uchumi wa bluu utasaidia watu wengi sana kupata kipato na hivyo kuweza kujikwamua kiuchumi.
“Lakini niwahaidi kwamba nitafatuta kiwanda cha mwani ili wakiweke kwenye Jiji la Tanga hivyo niwahamasishe watu wengi walime mwani na nimewaomba botnar watusaidie hivyo wananchi tusikate tamaa mapema mwani utalipa hivyo tujitume kulima” amesema Waziri Ummy
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mwakilishi wa Botnar Tanzania Dkt. Hassan Mshinda amemuhakikishia Mbunge Ummy kuwa Botnar itaendelea kushirikiana nae na halmashauri ya Jiji la Tanga katika kutatua kero za maendeleo kwa wakazi wa Tanga mjini hususan vijana na watoto.
Post a Comment