HEADER AD

HEADER AD

MBUNGE KOKA : MNAONYEMELEA JIMBO MNIACHE NIFANYE KAZI

Na Gustafu Haule, Pwani

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka (CCM) ameeleza kusikitishwa na tabia ya baadhi ya wanasiasa wanaoanza kujipitisha katika Jimbo lake huku akisema kama wanataka ubunge basi wasubiri muda wake umalizike.

Koka amesema kwasasa wamuache afanyekazi yake ya kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Kibaha Mjini sambamba na kukijenga chama na kama kuna mtu anafikiria kuhusu uchaguzi wa mwaka 2025 basi huyo atakuwa anakwenda kinyume na utaratibu.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka kushoto akipokea pesa taslimu Sh.Milioni tano kutoka kwa Mjumbe wa kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani Musa Mansour ikiwa ni sehemu ya mchango wa ujenzi wa ofisi ya CCM Kata ya Tangini.

Amesema kinachotakiwa kwa sasa ni kuhakikisha viongozi wa CCM ngazi zote wanashirikiana na wanachama wao kuhakikisha wanaelekeza nguvu zao katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika 2024.

Koka ametoa kauli hiyo Julai 02 wakati akiendesha harambee ya ujenzi wa ofisi ya CCM Kata ya Tangini iliyofanyika kwa kuwajumuisha viongozi mbalimbali wa CCM kutoka Kata ya Tangini ,Wilaya na Mkoa.

Amesema ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya viongozi na wanachama kuwaza uchaguzi wa mwaka 2025 jambo ambalo halina afya kwasasa na kwamba kufanya hivyo ni kukivuruga chama.

" Nafahamu kuna watu wameanza harakati za ubunge wa mwaka 2025 na watu wanapelekwa Mjini(Wajumbe) kwa ajili ya kuongea na wagombea lakini nawaambia tuache kuwaza 2025 bali tupeleke mawazo yetu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024,"amesema Koka

Koka ameongeza kuwa, ushindi wa uchaguzi wa  Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 ndio dira ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na kwamba lazima kwa pamoja tushirikiane kwa ajili ya kukivusha chama katika uchaguzi huo.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka,akikagua ramani ya ujenzi wa ofisi ya CCM Kata ya Tangini Kibaha Mjini kabla ya kufanya harambee ya kuchangia ujenzi huo jana.

Amesema kuwa suala la kugombea ni demokrasia na endapo muda ukifika kila mmoja anafursa ya kugombea na kwamba wamepewa chama kikiwa salama na lazima wakiache kikiwa salama na endapo wakianza chokochoko hizo ni wazi kuwa wataumiza chama.

Aidha,katika harambee hiyo Koka alifanikiwa kukusanya zaidi ya Sh .Milioni 15 ambapo kati ya hizo yeye alichangia mifuko 200 ya Saruji yenye thamani ya Sh.milioni tatu huku akiahidi kuendelea kuchangia mpaka ofisi hiyo ikamilike.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Kata ya Tangini Anthony Milao amemshukuru mbunge huyo kwa hatua kubwa ya kuendesha harambee hiyo kwani imekuwa na mafanikio makubwa.

Milao amesema jengo hilo mpaka kukamilisha kwake linahitaji kiasi cha Sh Milioni 60 lakini kwa nguvu za mbunge huyo kwa kushirikiana na wadau wengine anaimani litakamilika ndani ya muda mfupi ujao.

Hata hivyo , Mwenyekiti wa CC Wilaya ya Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka, akiwa katika harambee hiyo amewaomba wanaCCM wa Kata ya Tangini kuhakikisha wanajipanga kwa kuweka wagombea wazuri watakaokwenda kusimama katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa hapo mwakani.



No comments