WANAFUNZI 60 BARA, VISIWANI WASHIRIKI KONGAMANO LA SAYANSI TANGA STEM PARK
Na Boniface Gideon, Tanga
ZAIDI ya wanafunzi 60 wa shule Sekondari kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wameshiriki Kongamano la saba la Sayansi na Teknolojia lililoandaliwa na Kituo cha Sayansi Tanga STEM PARK chini ya usimamizi wa mradi WA uhamasishaji.
Wanafunzi hao wamefuzu na kuonyesha umahiri katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya Nchi kupitia sayansi na uhandisi na Hisabati.
Mratibu wa Kambi hiyo Dkt. Isaya Ipyana amesema wanafunzi waliweka kambi kwa zaidi ya siku 5 katika kituo cha Sayansi Stem Park ambapo wamepata masomo kwa nadharia na vitendo.
Amesema wanafunzi hao wamepata Elimu juu ya mabadiliko ya tabia Nchi namna ya kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia Nchi.
"Wamepata Elimu hii na tunaamini itawasaidia wawapo shuleni na hata baada ya kumaliza Elimu yao ambapo wataweza kutumia sayansi, teknolojia uhandisi na mahesabu ambayo walifundishwa kwa nadharia darasani na hivyo kufanya kwa vitendo hatua ambayo watafanikiwa kwa kiasi kikubwa"
Amesema kambi hiyo ililenga kufundisha mabadiliko ya Tabia Nchi "Kongamano la mwaka huu tulikuwa tumelenga hasa kwenye changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi jinsi gani ambavyo watatumia sayansi uhandisi na mahesabu kutatua changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
"Kwahiyo kuanzia tarehe 26 mpaka 30 June wanafunzi kutoka Mikoa 10 ya Bara na Visiwani walikutana pamoja kukaa chini na kutafuta njia mbadala ambazo wanaweza kuzitumia " amesema Dkt . Isaya.
" Wapo ambao waliweza kutengeneza ndege nyuki ( drones), wapo ambao waliweza kutengeneza mitambo kwaajili ya gesi, nia kubwa ni kuhakikisha yale ambayo waliweza kujifunza Darasani kwa nadharia wajifunze kwa vitendo hapa na tunashukuru kwamba wamefanikiwa" alisema Ipyana.
Amesema lengo lao kuu hasa ni kuwaandaa watoto na vijana ambao watakuwa wabunifu na kuweza kutatua changamoto mbalimbali kwa kupitia yale amabayo walishayasoma darasani ikiwemo Yale ambayo yanawazunguka katika mazingira wanayoishi.
"Dhima kubwa ni kuhakikisha tunatengeneza vijana ambao ni wabunifu na kuweza kutatua changamoto mbalimbali kwa kupitia yale ambayo wanayasoma darasani.
"Lengo ni kupata vijana wabunifu wenye uwezo wa kufikiria zaidi ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo tabia nchi na zile ambazo zinawazunguka kwenye jamii yao" aliongeza Dk. Ipyana.
Akizungumza kwaniaba ya Botnar Foundation ambao ndio wafadhili wakuu wa Kituo hicho , Mratibu wa Shirika Hilo mkoa wa Tanga Mbogolo Philoteus amesema shirika hilo linaamini kumuandaa kijana katika karne ya sasa na ijayo kwaajili ya kuingia kwenye soko la kiushindani.
Amesema hatua hiyo inasaidia kujiepusha kujiingiza katika mmomonyoko wa maadili na makundi maovu ambayo yanaweza kumfanya mwanafunzi kutokutimiza ndoto zake kielimu, kijamii kisiasa na nyanja mbalimbali.
"Sisi kama shirika tunaamini kijana bora huandaliwa akiwa mdogo ndio maana tumewekeza zaidi katika kumjengea uwezo kijana ili aweze kukabiliana na Karne ya 21 ambayo ni ya sayansi na teknolojia na tutaendelea kutoa ufadhili zaidi ya hapa mpaka malengo yatimie ya kuwasaidia vijana wainuke kiuchumi"Amesema Mbogolo
Post a Comment