WATOTO LAKI NNE KUPATA VYETI VYA KUZALIWA
Na Alodia Babara ,Bukoba
ZAIDI ya watoto 400,000 wanatarajiwa kusajiliwa mkoani Kagera kwa ajili ya kupata vyeti vya kuzaliwa kutoka kwa wakala wa usajili ufilisi na udhamini (RITA) baada ya kuzinduliwa kwa mpango huo mkoani hapa.
Kabidhi wasii mkuu wa Wakala wa usajili ufilisi na udhamini (RITA) Frenk Kanyusi akitoa taarifa julai 4, 2023 katika uzinduzi wa mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano uliofanyika uwanja wa mashujaa Mayunga manispaa ya Bukoba.
Frank amesema kuwa lengo la mpango huo ni kusajili na kuwapa vyeti vya kuzaliwa watoto zaidi ya 400,000 mkoani Kagera hadi kufikia mwaka 2025.
“Tuko hapa kuzindua mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano lengo ni kuhakikisha kila mtoto wa umri huo anasajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa na mpango huo utahakikisha kwamba kila mtoto atakayezaliwa kuanzia siku ya mpango huo kuanza anasajiliwa muda mfupi baada ya tukio la uzazi” Amesema Kanyusi.
Amesema mpango huo utasaidia kusogeza huduma karibu ,utaondoa ada ya cheti kwa watoto watakaosajiliwa kupitia mpango huo, kuleta huduma za za usajili karibu na makazi ya watu ambapo zitatolewa katika vituo vya kutolea huduma ya mama na mtoto na ofisi za watendaji kata bila malipo.
Aidha amesema mpango huo umeishatekelezwa katika mikoa 23 ya Tanzania Bara na zaidi ya watoto Milioni 8.2 wameishasajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa, baada ya Kagera mpango utaendelea katika mikoa ya Kigoma na Dar es salaam na kwa Kagera.
Amesema mpango huo utafanyika kwa awamu mbili awamu ya kwanza iliyoanza itafanyika kwa wiki mbili na baada ya hapo mpango utaendelea kwa kusimikwa katika ofisi za watendaji wa kata na vituo vya kutolea huduma ya mama na mtoto.
Meneja wa kampuni ya mtandao wa Tigo ambao ni moja wa wadau wa mpango huo Joseph Mutalemwa amesema wametoa simu janja zipatazo 600 kwa ajili ya kusaidia program za Tehama nchini ili kufanikisha mpango huo na wataboresha mtandao huo katika kata 32 za mkoa wa Kagera.
Kwa upande wake mgeni rasmi ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul akizungumza kwa niamba ya Waziri wa wizara hiyo amesema kuwa, wazazi watakapokuwa wanasajili majina ya watoto wao wahakikishe yanaendana na majina yaliyopo kwenye vitambulisho vyao vingine ili kuondoa changamoto ya majina kutofanana.
Naibu Waziri wa Katiba na sheria Pauline Gekul akitoa cheti Cha kuzaliwa kwa mtoto, katika uzinduzi wa mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano, mpango uliozinduliwa uwanja wa mashujaa Mayunga Manispaa ya Bukoba. Picha na Alodia Babara
Amewataka viongozi wa dini kuwataarifu waumini wao kujitokeza kusajili watoto wao kwa ajili ya kupata vyeti vya kuzaliwa na kuwa wale ambao wamezidi umri wa miaka mitano waombe kupitia mfumo wa ERITA.
Mmoja wa wananchi Didas Selemani mkazi wa Kashai amesema kipindi cha nyuma walikuwa wanatumia muda mrefu kupata vyeti vya kuzaliwa lakini kuja kwa mpango huu kutasaidia kurahisisha upatikanaji wa vyeti hivyo.
Post a Comment