HEADER AD

HEADER AD

VIONGOZI AMCOS WILAYANI MASWA WAKUTWA NA HATIA


Na Samwel Mwanga, Maswa

MAHAKAMA ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imewakuta na hatia Viongozi watatu wa Vyama vya Msingi wa Ushirika(AMCOS)waliokuwa wakikabiliwa na makosa mbalimbali katika mahakama hiyo.

Katika kesi ya Uhujumu Uchumi Na.5 ya mwaka 2022 iliyokuwa inamkabili Ibrahim Mahega ambaye alikuwa Katibu wa Amcos ya Nguliguli baada ya kutiwa hatia  baada ya kukiri kosa na  kutakiwa kurejesha kiasi cha Sh 2,114,000 za Amcos hiyo na kutakiwa kutotenda kosa la jinai kwa kipindi Cha mwaka mmoja.

Awali mshitakiwa alikuwa akishitakiwa kwa makosa mawili ambayo ni Ubadhilifu wa fedha Sh 2,114,000 na kosa la wizi wa Wakala wa  fedha kiasi hicho zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa maghala ya kununulia pamba makosa ambayo anadaiwa kuyatenda Mei 31 mwaka jana.

Katika kesi ya Uhujumu Uchumi Na.6 ya mwaka 2022 iliyokuwa inamkabili tena Ibrahim Mahega ametiwa hatiani baada ya kukiri makosa mawili likiwemo kosa la ubadhilifu wa fedha na wizi wa Wakala kiasi cha Sh 300,000 ambazo alipaswa kulipa ushuru katika chama Kikuu cha Ushirika mkoa wa Simiyu(SIMCU) na amehukumiwa kurejesha kiasi cha hicho cha fedha kwenye Amcos hiyo.

Katika kesi ya Uhujumu Uchumi Na.4 ya mwaka 2022  ilikuwa inawakabili, viongozi wa Amcos ya Sulu ambao ni Stephen Jilingisila ambaye ni Mwenyekiti na Silas Shambota ambaye ni Katibu kwa pamoja walishitakiwa kwa kosa la ubadhirifu wa fedha Sh 3,349,800 na hivyo kila mmoja alihukumiwa kurejesha kiasi cha  Sh 1,116,600  za AMCOS hiyo.


Imeelezwa kuwa washitakiwa wote hao walikuwa wametenda makosa hayo kinyume cha kifungu cha 28 cha Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa Sura 329 marejeo ya mwaka 2019 .

Hukumu zote zimetolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Maswa, Enos Misana huku upande wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa(TAKUKURU)ikiwakilishwa na waendesha Mashitaka wawili ambao ni Bahati Kulwa na Albertina Mwigilwa.

Katika hatua nyingine,TAKUKURU imemfikisha mahakamani,Richard Bundala ambaye ni Katibu wa Amcos ya Kidema wilayani Maswa.

Akisomewa Mashitaka yake mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Maswa,Enos Misana na Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU,Bahati Kulwa ilidaiwa mshitakiwa kufanya ubadhirifu wa kiasi Cha fedha Sh 1,228,000 za ushuru wa SIMCU kinyume na kifungu 28(1)cha Sheria ya Kupambana na Rushwa Sura 329 iliyofanyika marejeo mwaka 2019.


 Pia amesomewa shitaka la pili la wizi wa Wakala kiasi cha Sh 265,273 za AMCOS hiyo kinyume cha kifungu cha sheria 265 na 273(b) cha kanuni ya Adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Mshitakiwa huyo anadaiwa kufanya makosa hayo yote Septemba 15 mwaka jana na alikana mashitaka yote aliyosonewa mahakamani hapo.

No comments