HEADER AD

HEADER AD

RIDHIWANI AWAAGIZA WARATIBU KUFANYA UTAMBUZI ILI WENYE VIGEZO WANUFAIKE NA TASAF

Na Gustafu Haule, Pwani

NAIBU Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Ridhiwani Kikwete,amewataka waratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) kuhakikisha wanaendelea kufanya utambuzi  kwa wazee na hata watu wengine wenye vigezo ili waingizwe katika mfuko huo.

Ridhiwani amesema lengo la kuanzisha mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) ni kutaka kuwainua watu kutoka katika hali duni ya umaskini na kuwainua kiuchumi ili nao waweze kupata mahitaji muhimu kama ambavyo wanapata watu wengine.

      Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Ridhiwani Kikwete.

Ametoa kauli hiyo kwa wakati tofauti alipotembelea miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyoanzishwa na jamii kupitia mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Katika ziara hiyo aliyoifanya Julai 11 -12 Ridhiwani ametembelea mradi wa kilimo cha mbogamboga na matunda katika Kitongoji cha Mwembebaraza Kata ya Janga katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini pamoja na vikundi vingine vilivyopo katika Kijiji cha Kisanga Kata ya Masaki Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe.

Amesema kuwa mradi wa TASAF ulianzishwa na Hayati  Benjamini Mkapa kwa ajili ya kuondoa umaskini lakini umeendelee kusaidia jamii mpaka sasa ukiwa chini ya utawala wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa,Rais Samia anataka kuona TASAF inaendelea kuwa msaada katika kuwakomboa watanzania ndio maana ameelekeza nguvu nyingi katika mfuko huo na anataka kuona matokeo chanya yanapatikana.

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo ni lazima waratibu wa TASAF waendelee kufanya kazi ya kuwatambua wazee na wale wote wenye sifa au vigezo vya kuwa katika mpango huo ili nao waweze kusaidiwa.

"Mimi nawapongeza TASAF kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya maana imewafaidisha wananchi wengi Tanzania lakini Rais Samia anataka kuona kila mwenye sifa ya kuwepo TASAF anaingizwa ili nao waweze kusaidiwa na mpango huu,"amesema Kikwete

Naibu Waziri amesema kuwa ni vyema watendaji wa Halmashauri wakaangalia namna ya kushirikiana na TASAF kwa kuhakikisha zile fedha za asilimia 10 nazo zinaelekezwa katika kuwasaidia watu waliopo katika mpango huo kwakuwa wanaweza kulipa mikopo yao.

"Mifuko mingine isaidiane na TASAF ili kuendelea kuwakwamua kiuchumi watu wenye hali duni maana kuna watu wanakopeshwa fedha mpaka milioni 10 huko halmashauri lakini kurudisha hawawezi, sasa bora hivi vikundi vya TASAF vipewe fedha hizo kwakuwa wanaweza kurejesha."amesema Ridhiwani.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibaha Vijijini Josephine Gunda,amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mkombozi wa jamii ya watu maskini waliopo katika Halmashauri yake kwani amewasaidia kubadilika maisha yao.


Gunda amesema vipo vikundi vingi vya ujasiriamali pamoja na vile vya kuweka akiba vimefanikiwa kupitia fedha za TASAF na sasa wengi wao wanasomesha watoto pamoja na kuwa na uhakika wa kupata chakula .

Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia inapaswa kuungwa mkono kupitia juhudi zake kwakuwa bila kuweka msukumo katika TASAF ni wazi kuwa baadhi ya wanajamii wangekuwa katika hali mbaya ya kimaisha.

"Lazima tumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza mfuko huu wa TASAF kwani inawezekana alipoingia madarakani angeweza kuvunja lakini kwa maono yake amesema ngoja azidi kuimarisha TASAF kwa faida ya wananchi ,hakika katika hilo anapaswa pongezi,"amesema Gunda.

Hata hivyo mmoja wa wanufaika wa TASAF kutoka Kitongoji cha Mwembebaraza Dawia Hassan , ameishukuru  Serikali kwa kuwapelekea mpango huo kwa kaya masikini kwani umemsaidia kusomesha mtoto wake Hassan Kolola mpaka kufikia chuo Kikuu.



No comments