NAIBU KATIBU MKUU : RUWASA NA MAMLAKA ZA MAJI SHIRIKIANENI
>>>Taasisi zisaidiane kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi
>>>Zibuni vyanzo vipya vya maji
Na Samwel Mwanga, Maswa
WAKALA Wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA)pamoja na Mamlaka za Maji Mijini hapa nchini zimetakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana kwa kuwa lengo lao ni moja la kuhakikisha wanawapatia wananchi huduma ya maji safi na salama.
Hayo yameelezwa Julai, 29, 2023 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Cyprian Luhemeja baada ya kutembelea ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita Milioni mbili linalojengwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa(Mauwasa)katika Kijiji cha Hinduki wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji,Mhandisi Cyprian Luhemeja (mwenye kofia nyeupe) akizungumza mara baada ya kutembelea ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita Milioni mbili katika Kijiji Cha Hinduki wilaya ya Maswa huku Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(mwenye shati la draft)akisikiliza.
Amesema kuwa taasisi hizo zote ni za Serikali na zipo katika Wizara moja ya maji ambayo imepewa dhamana ya kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama katika maeneo ya mjini na vijijini.
Mhandisi Luhemeja amesema kuwa taasisi hizo zisaidiane katika suala la kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi kwa kubuni vyanzo vipya vya maji ili waweze kupata maji ya kutosha kwani bado kuna changamoto za upatikanaji wa maji kwa baadhi ya maeneo.
"Ni vizuri mkashirikiana hizi taasisi ambazo wote mnajukumu la kumpatia mwananchi huduma ya Maji safi na salama katika maeneo yenu yawe ya mjini au vijijini hivyo mkifanya kazi kwa pamoja tutafikia lile lengo la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan la kumtua mama ndoo kichwani,"amesema.
Amesema kuwa Serikali bado inaendelea na jitihada za kuboresha huduma ya maji vijijini na mijini na kiwango cha upatikanaji wa maji kinakua siku hadi siku ambapo hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo hayo inaongezeka.
Tenki la kuhifadhi maji lita Milioni Mbili linalojengwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (Mauwasa)katika Kijiji cha Hinduki wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.
Akizungumza ujenzi wa tenki hilo amesema kuwa ameridhishwa na ujenzi huo na kuhaidi kuwa wizara ya maji itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo ili liweze kukamilika kwa wakati.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa tenki hilo,Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Mhandisi Nandi Mathias anasema ujenzi wa tenki hilo ambalo linatarajia kutumia gharama ya zaidi ya Tsh. Bilioni 2.2 umefikia asilimia 60 na linajengwa kwa kutumia mafundi wa ndani(Force Akaunti) na hadi sasa wameshapokea kiasi cha shilingi Milioni 450.
Mhandisi Nandi amesema kuwa ujenzi huo ambao utakuwa sambamba na usambazaji wa mabomba ya maji utakapokamilika moja ya faida kubwa ni pamoja na kuwapatia maji wananchi wa mji wa Maswa kwa muda wa masaa 24 kwa siku kwani sasa wanapata maji kwa muda wa masaa 18 kwa siku.
"Baada ya ujenzi huu wa tenki kukamilika Moja ya faida kubwa ambayo tutaipata ni kuwapatia huduma ya maji wananchi wa mji wa Maswa kwa muda wa masaa 24 kwani kwa sasa tunatoa Maji kwa muda wa masaa 18,"anasema.
Pia Mhandisi Luhemeja ametembelea mradi wa maji katika kijiji cha Zabazaba wilayani humo unaoendeshwa na RUWASA ambao umekamilika na kuendelea kutoa huduma ya Maji safi na salama kwa wananchi wa Kijiji hicho.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Cyprian Luhemeja(mwenye shati la bluu) akizungumza na wananchi katika Mradi wa Maji wa Zabazaba wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu pia Mkuu wa wilaya hiyo,Aswege Kaminyoge(wa kwanza kulia)naye akisikiliza.
Meneja wa RUWASA wilaya ya Maswa,Mhandisi Lucas Madaha amesema kuwa kwa wale wananchi wanaohitaji kuingiza maji kwenye nyumba zao wafanye hivyo kwa kufuata taratibu watakazopewa na chombo cha watumiaji maji ambao ndiyo wanaendesha mradi huo wa maji.
"Ruwasa tuna msemo wetu kuwa maji bombani hivyo kwa wale watu wote wanaohitaji maji ya bomba kuingiziwa kwenye nyumba zao katika Kijiji Cha Zabazaba unafika kwenye chombo kinachoendesha mradi huu wa maji unapewa utaratibu kisha unapewa maji na wala hatutoi msaada kwenye jambo hili utalipia huduma hiyo ya maji" amesema.
Post a Comment