SERIKALI YAFURAHISHWA MAENDELEO KITUO CHA SAYANSI TANGA 'PROJECT INSPIRE'
Na Boniface Gideon, TANGA
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolph Mkenda ameonesha kufurahishwa na Maendeleo makubwa ya kuinua Sayansi mkoani Tanga baada ya ujio wa Kituo cha Sayansi cha STEM PARK kilicho chini ya usimamizi wa wa mradi wa Insipire.
Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kujenga kituo kikubwa cha Sayansi na Teknolojia mkoani Dodoma ambacho kitatumiwa na viongozi wengine wa Serikali kama mfano utakaosaidia vituo vya aina hiyo kujengwa maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi.
Waziri Mkenda ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea kituo cha Sayansi cha Stem Park kilichopo Jijini Tanga, mpango ambao amesema utasaidia kumaliza tatizo la wanafunzi kutopenda masomo ya sayansi.
"Ujio wa kituo hiki umesaidia sana tatizo la wanafunzi kutokupenda masomo ya Sayansi,tunawapongeza wote waliofanikisha ujenzi wa kituo hiki lakini mpango wa serikali nikuongeza vituo vingi zaidi vya sayansi na katika kufanikisha hili tutashirikiana na Project Inspire kujenga kituo kikubwa mkoani Dodoma" Amesisitiza Waziri Mkenda.
Waziri asema kituo ambacho kitajengwa mjini Dodoma kitakuwa kama kituo cha mfano ambacho wabunge na viongozi wengine wa serikali watakitembelea ili kuona umuhimu wa kuwa na vituo vya aina hiyo kwenye maeneo yao.
"Dodoma ni katikati ya nchi yetu halafu pale wabunge, mawaziri wenzangu na watu mbalimbali wakuu wa mikoa nitapenda watembelee pale waone nini kinaweza kufanyika.
"Vituo hivi vinapaswa kujengwa kila mikoa najua haitafikia wanafunzi wote vitu vyote hivi ni matunda ambayo yanapatikana kirahisi. " amesema Waziri Mkenda.
"Kwahiyo mimi mwenyewe nitasapoti kwanza tutafute eneo jiji la la Dodoma litupe eneo litupe na majengo waje pale na tusiwatoze hata thumni kwasababu wenyewe hawawatozi wanafunzi wanaokuja kufanya mafunzo hapa hawalipishwi chochote," amesema Prof Mkenda.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mradi wa Insipire Lwidiko Edward amesema kituo hicho kinawatengeneza wanafunzi kwenye masomo ya sayansi kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kujifunza kwa Vitendo na kuandaa mazingira yanayotoa hamasa ya kusoma.
"Kituo hiki mpaka sasa hivi kimewanufaisha maelfu ya wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali nchini,bara na visiwani.baadae"Amesema Edward.
Ameongeza kuwa kituo hicho kinafundisha kwa vitendo zaidi kwakutumia mbinu na vifaa vya kisasa zaidi vya sayansi, hivyo wanawaandaa wanasayansi mahiri wa baadae.
Post a Comment