WORLD VISION WATOA MSAADA WA VYAKULA KWA KAYA 229
Na Boniface Gideon, Tanga
JUMLA ya Kaya 229 kutoka Vijiji mbalimbali wilayani Mkinga Mkoani Tanga zimepatiwa msaada wa chakula kupitia Shirika la World Vision ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na uhaba wa Chakula kwenye baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na ukame kwa miaka miwili mfululizo.
Baadhi ya kaya wilayani humo zinakabiliwa na upungufu wa chakula kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo hali inayopelekea kupata lishe duni kutokana na watoto wao kula mlo mmoja kwa siku badala ya milo mitatu
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa msaada huo wa chakula Wananchi wa Vijiji zaidi ya 8 wilayani humo wamesema jambo hilo linalopelekea afya zao kudumaa na hatimaye watoto kushindwa kufanya vizuri pindi wawapo mashuleni.
"Watoto wetu wanatakiwa wale kutwa mara tatu lakini wanakula mara moja tuu, hii ni changamoto kubwa sana inayotukabili sisi wazazi, "amesema mmoja wa wananchi hao.
Baadhi ya wananchi wengine wamesema wanasumbuliwa na upatikanaji wa pembejeo za kilimo katika Vijiji vyao ambapo wameliomba Shirika la World Vision kuviwezesha vikundi vya ulemavu ili waweze kupatiwa msaada wa pembejeo.
"Tunaishukuru World Vision kwa hiki walichotuletea leo, tunaomba watutembelee pindi wanapokwenda kwenye miradi yao sisi walemavu tuna vikundi vyetu vya walemavu waje wavione waone nini kinatukwamisha hususani kwenye pembejeo za kilimo maana walemavu sisi hatuoni wengine wamekatwa miguu lakini watoto tulionao ndio wanatusaidia, "amesema mmoja wa walemavu hao.
Kwa Upande wake Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Duga Maforoni wilayani Mkinga Albertina Makungu amesema katika mwaka wa 2021 na mwaka 2022 walipatwa na changamoto ya ukame katika maeneo ya wilaya ya Mkinga, ambapo amelishukuru shirika hilo kwa kutoa msaada kwa watu wenye uhitataji wa chakula.
"Kweli tuna janga la njaa tunakula kwa shida tunashukuru zaidi kwa msaada huu tumekuwa na janga la njaa kwa muda mrefu, kaya na familia zimepata shida ya chakula kwa miaka miwili mfululizo, "amesema Makungu.
Meneja wa Mradi wa World Vision katika Wilaya ya Mkinga Evodia chija amesema shirika hilo kupitia viongozi wao limeamua kuwagusa waathirika wa Janga la njaa kutokana na ukame katika baadhi ya maeneo, ambapo wameweza kuwachangia maharage na mahindi kilo 2000.
Amesema lengo la kutoa msaada kwa makundi ya wenye ulemavu na watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu ni ili na wao waishi kwa furaha kwa kupata tumaini kwenye maeneo yao kama watu wengine.
"Wafanyakazi wa World vision kwa ushirikiano wao na upendo wao tuliweza kukusanya kiasi cha Tsh. Milioni 7.5 ambazo kwa furaha kubwa viongozi wetu wakazielekeza zile fedha zilizopatikana zije kusaidia watoto wenye uhitaji katika eneo la mradi wa Mkinga, "amesisitiza chija.
"Tumetoa msaada wa Maharage, unga kilo 2000 wenye virutubishi kwenye kaya hizi lakini kati ya kaya hizo kaya 30 ni za watu wenye ulemavu, watoto ambao ni wasajiliwa kwenye miradi ya World Vision wako kaya 136,"amesema Chija.
Post a Comment