ASHIKILIWA KWA KUMUUA MKE, SHEMEJI
Na Boniface Gideon, TANGA
JESHİ la Polisi mkoa wa Tanga limefanikiwa kumkamata Swalehe Miraji Ally mwenye umri wa miaka 38 kwa kosa la kumuua mke wake pamoja na shemeji yake kwa kuwakata kwa mapanga mara mbili kichwani wakati wakiwa shambani kisha kukimbilia mkoani Tabora.
Akitoa taarifa hiyo kwa Waandishi wa habari Augost 17/2023, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga ACP Almachius Mchunguzi amesema mtuhumiwa huyo ambaye ni fundi ujenzi mkazi wa Mkanyageni wilayani Muheza alimuua mkewe Mwanahawa Hassan (24) na Sauda Sufian (20) kisha kukimbilia Tabora lakini jitihada za Polisi zilifanikiwa na kumkamata mtuhumiwa kwaajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha jeshi hilo wilayani Handeni limefanikiwa kumkamata Rajab Athuman mwenye miaka 32 kwa kosa la kumuua kwa kumkata kichwa Helena Sila ambapo bado upelelezi unaendelea kufuatia tukio hilo.
Katika taarifa nyingine Kamanda Mchunguzi amesema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kuwatia hatiani watu watano kwa makosa mbalimbali ambapo Ally Kilulu amehukumiwa miaka 15 jela kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya aina ya Heroin gram 1, Amos Hamis akihukumiwa miaka 14 jela kwa kosa la kubaka huku Halid Yusufu akihukumiwa miaka mitano jela kwa kosa la wizi wa mifugo.
Wengine ni Bakari Mohammed ambaye amehukumiwa miaka mitano jela kwa kosa la kuvunja duka usiku na kuiba huku Ernest Petro akihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa makosa ya kuzini na Maharimu (ndugu yake) .
Hata hivyo Kamanda Mchunguzi amewataka wananchi mkoani wa Tanga kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama pale wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao ili sheria kali dhidi ya wahalifu na uhalifu ziweze kuchukuliwa.
"Jeshi la Polis linatoa wito kwa wananchi wote mkoani Tanga kuendelea kutoa ushirikiano wa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa jeshi la Polis ili kuzifanyia kazi na kuimarisha hali ya utulivu na amani"
"Wananchi wa mkoa wa Tanga muendelee kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika maendeo yenu na kutumia wakaguzi kata wa jeshi la Polisi waliopo katika kata zote mkoani hapa katika kuzuia viashiria vya uhalifu na wahalifu kabla haujatendeka katika maeneo yenu" amesema kamanda ACP Mchunguzi.
Post a Comment