HEADER AD

HEADER AD

TMDA YATAKIWA KUONGEZA NGUVU YA KUDHIBITI DAWA BANDIA ZINAZOINGIA NCHINI


Na WAF, Dodoma

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI Stanslaus Nyongo ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuongeza nguvu ya kudhibiti bidhaa feki za dawa zinazoingia nchini Tanzania. 

Mwenyekiti wa kamati hiyo Nyongo ameyasema hayo Agosti 17, 2023 baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TMDA Adam Fimbo katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI Stanslaus Nyongo

“Tunaona juhudi mnazofanya za kuteketeza dawa feki zinazoingia nchini, hii inaonesha bado kuna mianya mingi ya kuingiza dawa nchini hivyo ni muhimu sana kuongeza nguvu ya kudhibiti uingizwaji wa dawa feki”, amesisitiza Stanslaus.

Ameitaka Mamlaka hiyo kuangalia ufanisi wa dawa zilizopo kwa maana kuna baadhi ya dawa hazina ubora mzuri unaotakiwa kulingana na dawa husika hasa kwenye dawa wa ‘Antibiotic’.

“Kuangalia ufanisi wa dawa iwe kipaumbele cha kwanza hasa kwenye hizi dawa za ‘Antibiotic’, maaana anaweza kuja mgonjwa anasema nikitumia dawa hii inaniponyesha kwa haraka kuliko nikitumia dawa hii, Sasa hii ni changamoto kwenu mkalifanyie kazi”, amesema Stanslaus.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa katika suala la ubora wa dawa linaangaliwa katika mambo Matatu, ambavyo ni ubora, usalama na ufanisi.

     Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza

“Kwanza tunaangalia swala la ubora,  tunaangalia usalama na ufanisi, kwa hiyo hapa TMDA mnatakiwa kuongeza nguvu kwenye ufanisi wa dawa”, amesema Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy ameipongeza TMDA kwa jitihada wanazofanya kwenye TEHAMA kwa kuwa hakuna malalamiko yoyote ya mtu kukwama usajili kwa muda wa miaka Miwili.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Adam Fimbo amesema usajili wa waganga wa tiba asili nchini ulianza mwaka 2010 ambapo hadi Julai Mwaka 2023, idadi ya wataalam wa Tiba Asili/Mbadala waliosajiliwa ilifikia 47,467 na vituo vya kutolea huduma 1,640 vilikuwa vimesajiliwa.

     Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Adam Fimbo.

“Baada ya kufanya usajili huo, matarajio ya Wizara katika kipindi cha mwaka 2023/2024 huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini zitaimarika na kuboreshwa zaidi kwa kuzingatia Sheria na mikakati iliyowekwa na Baraza”, amesema Fimbo.

No comments