HEADER AD

HEADER AD

MADIWANI WASEMA HAKUNA VIKAO VILIVYOWAHI KUJADILI KUWA WANANCHI WA BEGI, KIWANDANI NI WAVAMIZI

>>Wasema hoja ya Serikali kudai kuwa wananchi wamevamia shamba la mifugo haikuwahi kujadiliwa katika vikao vya Baraza la Madiwani.

>> Wasema licha ya uthamini unaoendelea Serikali ya Rorya haijaweka wazi aina ya mradi unaotarajiwa kuwekezwa au mwekezaji gani anayetaka kuwekeza.

>>>Diwani Mstaafu Peter Sarungi akazia, asema wananchi wa Vitongoji hivyo hawajavamia shamba la mifugo (Utegi Dairy Farm) ni makazi yao ya asili.

Na Dinna Maningo, Rorya

MADIWANI ambao wameongoza Katika Kata ya Koryo, wilaya ya Rorya mkoani Mara, ambao ni wakazi wa Kata hiyo wamesema wanashangazwa na kauli ya viongozi wa Serikali kudai kuwa wananchi wa Kitongoji cha Begi na Kitongoji cha Kiwandani katika Kijiji cha Majengo walivamia na kuishi katika eneo la shamba la mifugo (Utegi Dairy Farm).

Wamesema wananchi wa Vitongoji hivyo hawajavamia ni maeneo yao ya asili huku wakishangazwa na hatua ya Serikali kuwafanyia uthamini wananchi bila kuwaambia ni mradi gani wanaotarajia kuwekeza au mwekezaji gani atakayewekeza katika shamba hilo ambalo limekaa kwa zaidi ya miaka 20 bila kuendelezwa.

Diwani wa Kata ya Koryo Ores Simba anasema kuwa uthamini wa fidia unaofanyika katika Kitongoji cha Begi na Kitongoji cha Kiwandani umezua taharuki kwa wananchi baada ya wathamini kutofanya uthamini wa ardhi na badala yake wanafanya uthamini wa nyumba na maendelezo katika ardhi.

Diwani wa Kata ya Koryo Ores Simba


"Uthamini huu umechukua sura ya hajabu, Julai, 14, tulikutana ofisi ya Mkurugenzi ukumbi wa halmashauri na aliyetukutanisha ni mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao. Alikuwepo Mbunge, Mwenyekiti na Katibu wa CCM wilaya, Madiwani wa maeneo husika yanayofanyiwa uthamini kutoka Kata ya Koryo na Bukwe.

"Wengine ni Wenyeviti wa Vitongoji ,Watendaji wa Vijiji na Kata wa maeneo husika, wathamini, kamshina wa ardhi wa mkoa, wataalam wa ardhi wa Halmashauri ambao pia wamehusika katika zoesi la uthamini"anasema.

Anasema katika kikao hicho walilalamika juu ya ushirikishwaji. Ni baada ya ujio wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula Mwezi Mei, 2023 akiwa ameongozana na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee wakiwa wameongozana na viongozi wengine wa Serikali aliwaambia wananchi kuwa wamevamia shamba hivyo hawatalipwa isipokuwa kifuta jasho.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula (Picha na Mtandao)


 "Mwezi Mei alikuja mkuu wa mkoa akiwa na Waziri wa Ardhi ilijitokeza sintofahamu baada ya kusema kuwa Vitongoji vilivamia kuwa hawastahili kulipwa fidia watalipwa kifuta jasho tu .

"Wananchi hawakuridhishwa na kauli huyo walilalmika sana wakasema ushirikishwaji haukuwa mzuri. Serikali inachanganya kuna waliovamia ardhi lakini hivi Vitongoji vya Begi na Kiwandani hawajavamia shamba ni maeneo yao ya asili.

Diwani anasema katika kikao tulichoketi Julai, 14 tulikubaliana kuwa neno la kuvamia halipo na kifuta jasho halipo, watu watalipwa fidia ya ardhi na maendelezo.

Anasema baada ya makubaliano hayo viongozi walishirikiana katika utoaji wa elimu kwa wananchi pamoja na wenye shamba ambao ni Serikali.

Anasema zoezi la uthamini lilipoanza zikajitokeza dosari za wananchi kutotathminiwa ardhi zao huku baadhi ya nyumba zikiachwa bila kuhesabiwa.


"Wakasema wao hawawezi kupima ardhi, viongozi na wananchi wakaenda kulalamika CCM wilaya wakidai kwanini fomu iwe moja, Katibu akatoa maelekezo wakasema watatekekeza, lakini maelekezo ya Chama hayakufuatwa, watu wanaendelea kuhesabiwa maeneo yao maana hawawezi kushindana na Serikali, tunaomba Rasi Samia asikilize vilio vya wanyonge.

Anasema suala la uthamini halikuwa wazi lilifichwafichwa hata kwenye vikao vya Baraza la Madiwani halikuwekwa wazi zaidi ya kauli ya Serikali kuwa inataka kuendelea eneo hilo, na Madiwani kulalamikia zoezi la uthamini.

"Nilifuatilia kujua kwanini miradi ya shule ya msingi Utegi haiendelezwi wakasema ni maamuzi ya Serikali kuu hivyo watakuja kueleza baadae. Serikali ilizuia watu kuendeleza maeneo bila hata kutoa tangazo la maandishi la zuio la uendelezaji wa maeneo ambalo lilipaswa kubandikwa kwenye mbao za matangazo ofisi ya Kata au ya Kijiji ili wananchi wajue.

"Kwakuwa hapakuwa na tangazo la kuwazuia watu kuendeleza maeneo yao wakayaendeleza maana ni ardhi ya wananchi na hujawazuia kwa barua rasmi, istoshe wananchi hawajakataa kuhama wanachotaka Serikali itende haki kwa kila mmoja.

Anaiomba Serikali ifate haki ilipe watu ardhi yao na malipo yawe mazuri kwani kwa kufaya hivyo wananchi watakuwa na imani na Serikali yao.

Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Girango mkazi wa Kijiji cha Utegi, Hellena Ezekiel Magige anasema kuwa katika vikao vya Baraza la Madiwani haikuwahi kuibuka hoja yoyote kwamba Kitongoji cha Begi na Kiwandani vipo ndani ya shamba la mifugo.
Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Girango mkazi wa Kijiji cha Utegi, Hellena Ezekiel Magige

Anasema katika vikao walielezwa kuwa Serikali inataka kuendelea na uwekezaji katika shamba la mifugo hivyo wananchi wa Vitongoji hivyo watafanyiwa uthamini wa ardhi, nyumba na mazao na Maendeleo mengine kisha kulipwa fidia ili kuondoka katika maeneo hayo.

"Nachofahamu Kitongoji cha Begi na Kiwandani vipo nje ya Farm, na walituambia watachukua vitongoji hivyo,  wakasema kwenye vikao watatathmini ardhi ambayo ipo tupu na vitu endelevu.

"Nasikitika baada ya tathmini kuanza wameacha kupima ardhi wanahesabu vitu vilivyo kwenye ardhi . Ukiangalia hali ya watu wa Vitongoji hivi shughuli yao kubwa ni kilimo wanaposema hawatafanya uthamini wa ardhi wakati ardhi hiyo ndiyo inayowaingizia kipato , wanasomesha watoto kutokana na kilimo sasa wataishije?

Anasema ni vyema Serikali ikawafanyia na uthamini wa ardhi ili pesa hiyo wakanunue mashamba kwa ajili ya kuendelea na shughuli yao ya kilimo. 

"Kuna watu wanaishi kule ni wazee, Yatima, Walemavu wa viungo ambao ukiwaondoa bila kuwalipa ardhi utawaingiza katika dimbwi la umasikini na maisha yao yatakuwa ya mateso.

Diwani huyo anasema wapo wananchi walichukua mikopo na dhamana yao ni ardhi ambapo hurejesha mikopo hiyo kutokana na mazo wanayovuna na kuuza na hivyo kupata pesa ya kurejesha mikopo.

" Watu waliweka ardhi yao kama dhamana wakachukua mikopo leo unataka kuwahamisha bila kuwalipa fidia ya ardhi waende wapi na watarejesha vipi mikopo?. Nililalamikia hili kwenye vikao vya halmashauri na tukaelezwa na wataalam kuwa watu watalipwa fidia ya ardhi na mali zilizopo juu ya ardhi lakini imekuwa tofauti." anasema Diwani.

Diwani Hellena anamuomba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro huo kwani waathirika wakubwa ni wanawake na watoto na kwamba endapo kusipokuwepo na fidia ya ardhi wababa watazikimbia familia zao kwenda mbali kutafuta kazi.

"Wababa watakuja kukimbia kwenda mbali maana watakuwa hawajapata malipo stahiki wataondoka kwenda kutafuta kazi sehemu za mbali, wanawake ndiyo watabaki na majukumu.

"Rais Samia wewe ni mwanamke mwenzetu tunakuomba uingilie kati mgogoro wa uthamini Kitongoji cha Begi na Kiwandani ili sisi viongozi wanawake tuendelee kuaminiwa katika uongozi.

Anaongeza" lisipotatuliwa hili jambo watu wakaondolewa bila kulipwa fidia ya ardhi sisi wanawake tutapuuzwa na wananchi hawaatuamini wanawake katika uongozi" anasema Diwani Hellena.

Diwani mstaafu Kata ya Koryo, Peter Sarungi anasema wananchi wa Vitongoji hivyo hawajavamia shamba la mifugo bali shamba ndilo liliwakuta wananchi na wananchi ndiyo walitoa maeneo yao kwa ajili ya uwekezaji wa shamba la mkonge ambalo kwa sasa ni shamba la mifugo( Utegi Dairy Farm).
     Diwani mstaafu Kata ya Koryo, Peter Sarungi

"Badhi ya wananchi wanaoishi kwenye vitongoji hivyo walikuwa wanaishi mlima Koryo Serikali ikawahamisha 1972 walipoamua kufaya uwekezaji na haikuwahi kuwalipa fidia.

"Wakati huo watu waliishi kwenye maeneo kutokana na taratibu zilizokuwepo za uongozi wa machifu, unaomba ardhi unapewa kwa taratibu unaishi, ilikuwa kabla ya Serikali kuchukua maeneo hayo ya mlima mwaka 1972 ambapo wananchi wa Kitongoji cha Begi waliwakaribisha na kuwapa makazi.

"Zamani kulikuwa na Kitongoji kimoja cha Begi baadae viligawanywa kuwa vitongoji viwili kikazaliwa Kitongoji cha Kiwandani.

"Hii kauli ya kwamba wananchi wa vitongoji hivyo wamevamia ardhi ya Farm mimi sikuwahi kuisikia ikizungumzwa kwenye vikao vya Madiwani kwamba wananchi hao wamevamia wanatakiwa kuondoka, nimeyasikia sasa baada ya kutaka kufanyika uthamini"anasema Peter.

      Baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Begi na Kiwandani wakiwa wameandamana ofisi ya CCM wilaya ya Rorya kuwalalamikia wathamini kutofanya uthamini wa ardhi.

Peter anaiomba Serikali kuwatendea haki wananchi wa Vitongoji hivyo na kwamba isitumie umasikini wao na uelewa wao mdogo wa sheria kutowatendea haki kwa mujibu wa Sheria ya ardhi na taratibu za uthamini wa fidia ili wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

Mbunge wa Jimbo la Rorya Jafari Chege anasema Nini kuhusu uthamini wa fidia? je anasemaje kuhusu kikao kilichofanyika Julai, 14, na kwanini wananchi hawafanyiwi uthamini wa ardhi?

.........Endelea kufuatilia DIMA Online itakujuza

No comments