MAUWASA YAPOKEA PAMPU MPYA ZA KUSUKUMA MAJI
Na Samwel Mwanga, Maswa
MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (Mauwasa) iliyoko katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imepokea pampu mpya tatu za kusukuma maji kutoka Wizara ya Maji.
Pampu hizo zitafungwa kwenye mitambo ya kusambaza Maji iliyoko katika bwawa la New Sola(Bwawa la Zanzui)ambacho ndicho chanzo kikuu cha maji cha Mamlaka hiyo.
Pampu hizo ambazo zimenunuliwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mauwasa ni sehemu ya pampu 16 ambazo zinapaswa kununulia ili kuboresha hali ya upatikanaji wa Maji katika mji wa Maswa na Vijiji vipatavyo 12.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Raphael Mwita akizungumza leo ofisini kwake mjini Maswa mara baada ya kupokea pampu hizo amesema kuwa ni sehemu ya uboreshaji wa huduma ya Maji inayotolewa na Mamlaka hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Raphael Mwita akizungumzia mapokezi ya pampu mpya tatu za kusukuma maji walizopokea kutoka Wizara ya Maji.Amesema kuwa pampu zilizopo za kusukuma maji ambazo ni 16 ni za muda mrefu na kwa sasa zimechakaa na ufanisi wake wa utendaji wa kazi umeshuka hadi kufikia asilimia 40.
"Tunazo pampu 16 katika mitambo yetu ya kusukuma maji kutoka bwawani kwenda kwa wananchi lakini pampu hizo ni za muda mrefu tangu zifungwe mwaka 1990 sasa ni miaka 33 zimechakaa na hata utendaji kazi wake yaani ufanisi umepunguza kutoka asilimia 100 hadi asilimia 40,"amesema.
Mwita amesema kutokana na hali hiyo hata gharama za matengenezo zimekuwa kubwa pamoja na pampu hizo kutumia kiasi kikubwa cha umeme na kuongeza gharama za uendeshaji kuwa kubwa kwa Mamlaka hiyo sambamba na maeneo mengine kutopata huduma ya Maji.
Maboksi yakiwa na pampu tatu zilizonunuliwa kwa ajili ya Mauwasa ili kuboresha huduma ya Maji mjini Maswa na Vijiji 12"Pampu zikiwa chakavu ni tatizo zinatuingiza gharama kubwa ya matengenezo ya mara kwa mara na hata umeme unaotumika kuziendesha ni mwingi na hivyo Mamlaka kubeba mzigo mkubwa wa uendeshaji na Kuna baadhi ya maeneo Maji hayafiki kutokana na pampu kutokuwa na nguvu ya kutosha ya kusukuma maji,"amesema.
Ameendelea kueleza kuwa kupatikana kwa pampu hizo kutapunguza baadhi ya changamoto hizo hasa yale maeneo ambayo yalikuwa hayapati maji kabisa hasa ya vijijini kutokana na uchakavu wa pampu hizo.
Aidha ametumia fursa hiyo kuishukuru Wizara ya Maji na kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutolewa kwa fedha kwa ajili ya ununuzi wa pampu hizo na kuomba pampu zilizobaki ambazo ni 13 nazo zinunuliwe ili waweze kutoa huduma bora ya maji safi na salama kwa wananchi wanaowahudumia.
Naye Diwani wa Kata ya Zanzui,Jeremiah Shigalla(Makondeko)ameiomba Mauwasa kuhakikisha inazifunga pampu hizo haraka ili Wananchi wa kijiji Cha Zanzui waweze kupata huduma ya maji kwa muda wote pindi maji yanaposukumwa.
"Tumefurahi kwa jinsi serikali kupitia Mauwasa inavyowajali wananchi wa wilaya ya Maswa ili waweze kupata huduma ya Maji safi na salama kwa kutuletea pampu hizo mpya.
" Ninaamini na nyingine zitakuja hivyo hizi zilizokuja zifungwe zianze kazi ili sisi tulioko maeneo ya vijijini tupate Maji muda wote kama wanavyopata wa mjini tusiwe na siku za mgao kama ilivyo Sasa,"amesema.
Moja ya mota ya pampu ya kusukuma maji ikiwa ni sehemu ya pampu mpya tatu walizokabidhiwa Mauwasa.Ofisi ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa(Mauwasa)iliyoko mjini Maswa mkoani Simiyu.
Post a Comment