MJUMBE CCM ASEMA MKATABA WA DP WORLD UMELENGA KUBORESHA BANDARI YA DAR ES SALAAM
Na Gustafu Haule, Pwani
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC)Hamoud Jumaa, ameungana na mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka kumtetea Rais wa awamu ya Sita Dkt.Samia Suluhu Hassan juu ya mkataba wa bandari baina Serikali ya Tanzania na Kampuni DP World ya Dubai kwa kusema mkataba huo ni muhimu kwa Taifa na kamwe Rais hasirudi nyuma.
Jumaa na Koka wameungana katika mkutano wa majumuisho ya ziara ya mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka uliofanyika Agosti 19 katika viwanja vya ofisi ya CCM Kibaha Mjini mkutano ambao umehudhuriwa na makatibu tawi,Kata, viongozi wa Wilaya na mkoa.
Jumaa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo amesema kuwa, Rais Samia hawezi kuingia mikataba ya hovyo na wala hawezi kuuza bandari isipokuwa anachokifanya ni kuboresha bandari ili hiweze kufanyakazi kwa ufanisi zaidi.
Amesema kuwa,mkataba wa Serikali na Kampuni ya DP World ya Dubai unalenga kuboresha bandari ya Dar es Salaam kwa kuhakikisha mapato yanaongezeka pamoja na kuondoa changamoto za ucheleweshaji mizigo na mambo mengine mengi.
Ameongeza kuwa Rais Samia ana malengo mazuri ya kuitaka kuifikisha nchi katika hatua ya juu ya maendeleo na anafanyakazi kwa mujibu wa Sheria za nchi hivyo ni vyema wananchi na wanaCCM wakaungana mkono juhudi zake.
"CCM kazi yake ni kutekeleza kupitia ilani yake na ndio wenye majukumu ya kuelimisha wananchi maana Mama Samia amefanya maamuzi ya busara na hawezi kufanyakazi ya hovyo na anafanya hivyo kwa ajili ya kuongeza mapato ya Taifa kwahiyo tumuache afanyekazi yake,"amesema Jumaa.
Jumaa amewaomba wanccm kumuunga mkono Rais Samia kwa kuhakikisha wanalisemea vizuri suala la bandari na kukemea wale ambapo wamekuwa wakitoa taarifa za uzushi juu ya mkataba huo kwani anaamini mkataba huo unafanyika maslahi mapana ya Taifa.
Aidha Jumaa ametumia nafasi hiyo kumpongeza mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka kwa kufanyakazi vizuri huku akimtaka aendelee kuchapakazi kwa ajili ya kutekeleza ilani ya uchaguzi kwakuwa CCM imeingia mkataba na wananchi na lazima isimamiwe vizuri.
Hata hivyo Jumaa amesema kuwa Chama hakiwezi kujengwa na mtu mmoja ndio maana unapotaka kugombea lazima ueleze umekifanyia nini chama lakini cha msingi anayetaka kuchangia lazima afuate utaratibu.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka, amesema kuwa hoja ya bandari inapaswa kuungwa mkono na watu wote kwakuwa kinachofanywa na Rais Samia sio kwa ajili ya maslahi yake bali ni maslahi ya Taifa.
Koka amesema wanaopinga mkataba wa bandari ni wazi kuwa hawana uelewa wa kutosha na wengine wakifuata mkumbo wa watu wachache wanaopinga bila kujua umuhimu wa jambo lenyewe.
Amesema kwakuwa anatambua dhamira njema ya Rais Samia juu ya mkataba huo angependa kuona wanaCCM na wananchi na Taifa kwa ujumla wanaunga mkono jambo hilo ili wampe nafasi Rais ya kuendelea kufanyakazi ya kuleta maendeleo ya Taifa.
Mwenyekiti wa CCM Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka, amesema kuwa Kibaha mjini ipo salama na wamejipanga kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika 2024 CCM inashinda kwa kishindo.
Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka, akizumgumza katika mkutano wa majumuisho ya ziara yake uliofanyika Agosti 19 katika viwanja vya CCM Kibaha Mjini.
Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka, akizumgumza katika mkutano wa majumuisho ya ziara yake uliofanyika Agosti 19 katika viwanja vya CCM Kibaha Mjini.
Nyamka amesema kuwa ziara aliyoifanya katika Kata zote za Kibaha Mjini imeonyesha taswira halisi ya ushindi wa CCM na kwamba ameahidi kushirikiana na viongozi wa matawi na Kata katika kufikia malengo ya chama.
"WanaCCM Kibaha Mjini tunamuunga mkono Rais kwa juhudi zake alizozifanya hapa Kibaha Mjini za kutuletea miradi mingi ya maendeleo na sisi tunatoa tamko rasmi la kumuunga mkono katika suala la mchakato wa uboreshaji bandari ", amesema Nyamka.
Post a Comment