MBUNGE KOKA ACHANGIA MILIONI 4.5 UJENZI OFISI YA CCM KATA
Na Gustafu Haule, Pwani
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ,amezindua harambee kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Msangani kwa kuchangia fedha taslimu Tsh .Milioni 4.
Mbali na kuchangia fedha hizo lakini pia Koka ameendesha harambee hiyo kwa kukata keki ambapo hatahivyo alikata keki hiyo kwa Sh.500,000 na kufanya jumla ya fedha alizochangia katika harambee hiyo kufikia Ts. 4,500,000 huku wanachama wengine wakiahidi kuchangia jumla ya Tsh. 1,150,000
Koka ameendesha harambee hiyo Agosti 17 mwaka huu katika viwanja vya ujenzi wa ofisi hiyo na kuwashirikisha viongozi mbalimbali wa CCM akiwemo mwenyekiti wa Wilaya ya Kibaha Mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka na kamati yake ya siasa.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka amezindua harambee kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Msangani
Viongozi wengine walioshiriki harambee hiyo ni wenyeviti wa CCM Kata,Makatibu Kata na baadhi ya Makatibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi kutoka sehemu mbalimbali akiwemo Ramadhani Mkwere kutoka Kata ya Tangini.
Awali akizungumza kabla ya kuendesha harambee hiyo Koka amesema kuwa yupo katika ziara ya kuimarisha Chama kwa kuhakikisha anazifanyia kazi changamoto zilizopo katika Kata mbalimbali ikiwa pamoja na kuhakikisha ofisi za Chama zinajengwa kila Kata.
Amesema kazi ya ujenzi wa Chama ni jukumu la kila mwanachama na kwakuwa Kata ya Msangani na maeneo mengine wapo tayari kujenga ofisi hizo basi ni vyema wakahakikisha dhamira hiyo inaanza maramoja .
Koka amesema kuwa yeye yupo tayari kushirikiana na wanachama na viongozi wote wa Kata na matawi katika kufikia malengo hayo na kwamba hatowaangusha katika shughuli zote za ujenzi wa Chama na hata zile za kuwaletea maendeleo.
Amesema kuwa Kibaha Mjini kwasasa ipo vizuri kwani ni tofauti na Kibaha ya mwaka 2010 na kwamba kwasasa maendeleo ni makubwa kutoakana na kuwepo miundombinu.
"Nawaahidi sitowaangusha katika shughuli zote ziwe za Chama au Serikali, ndio maana nimefanyakazi nanyi kwa muda mrefu na maendeleo mmeyaona na sasa Kibaha yetu ipo vizuri na Mji wetu unakwenda kuwa Manispaa,"amesema Koka.
Mbunge Koka amewataka wanaccm kuungana na kujipanga kikamilifu kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za mitaa unaokwenda kufanyika mwaka 2024 wanashinda kwa kishindo kwakuwa ushindi huo utakwenda kutoa dira ya uchaguzi Mkuu wa 2025.
Hatahivyo amewashauri viongozi wa CCM Kata ya Msangani kuhakikisha fedha zilizopatikana katika harambee hiyo waanze kukarabati vyumba vichache ili viweze kutumika wakati juhudi za kutafuta fedha nyingine zikiendelea.
Kaimu mwenyekiti wa CCM Kata ya Msangani Frank Msimbe amesema kuwa ujenzi huo ulianza miaka kumi iliyopita kwa michango yao wenyewe ,Diwani na mbunge .
Msimbe amesema kwasasa jengo hilo limefikia hatua ya upauaji na kilichobaki ni hatua za umaliziaji (Finishing) ambapo wanahitaji kuweka milango, madirisha, choo, upakaji rangi na mambo mengine madogomadogo.
Msimbe amemshukuru mbunge huyo kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwani anaamini utakwenda kusaidia katika kukamilisha jengo hilo huku akisema matarajio yao ni kwamba ifikapo Septemba 30 liwe limekamilika.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka, amesema ujenzi wa ofisi za Chama ni endelevu na huo ni mpango maalum wa CCM katika kuhakikisha kila tawi, Kata na Wilaya zinakuwa na ofisi zenye hadhi na za kudumu.
Nyamka amesema kuwa ofisi nyingi za CCM zilizopo hivi sasa ni za kukodi na kwamba tayari kwasasa wameweka mikakati ya kuhakikisha kila eneo la tawi na Kata zinapata ofisi zake na kufanya Chama kuwa imara zaidi.
Nyamka amewaomba wadau kujitokeza katika kuchangia ujenzi wa ofisi hizo kwakuwa milango ipo wazi lakini kinachotakiwa ni kufuata utaratibu wa Chama ambao unatoa fursa kwa mtu anayetaka kuchangia chama.
"CCM haizuii mdau au kiongozi yeyote kuchangia chama wala kutoa msaada ila chama kinakemea watu wanaokuja bila kufuata utaratibu na sisi tunasema Kama kuna mtu anataka kusaidia Chama basi ni vyema waje na wapate utaratibu mzuri ,"amesema Nyamka.
Post a Comment