WAKAMATWA KWA KUKUTWA NA NYARA ZA SERIKALI
Na Samwel Mwanga, Simiyu
JESHI la Polisi mkoa wa Simiyu limefanikiwa kukamata watu watatu kwa tuhuma ya kukutwa na Nyara za serikali za wanyamapori aina ya Swala wapatao 28 aina ya Thomson wakiwa wameuawa.
Watuhumwa waliokamatwa ni Masunga Madede(58),Musa Masinga(28) na Yunis Makwaya(45) wote wakazi wa Kijiji cha Mwasilimbi wilaya ya Bariadi mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Kamishina Msaidizi wa Polisi(ACP)Edith Swebe akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Bariadi amesema kuwa Agosti 17 mwaka huu katika Kijiji hicho walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa na Swala pamoja na pikipiki aina ya KingLion yenye namba za usajili T.874 CUA ndani ya nyumba ya Musa Masunga.
Kamanda Swebe amesema kuwa Jeshi hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Uhifadhi walifanya operesheni ya pamoja katika Kijiji hicho na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.
"Watuhumiwa hao walikutwa na Nyara za Serikali ambazo ni wanyamapori Swala 28 aina ya Thomson wakiwa wameuawa pamoja na pikipiki aina ya KingLion ndani ya nyumba ya Musa Masinga,"amesema.
Kamanda Swebe amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo ya nyara za serikali ambapo uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na askari wanyama Pori ili kubaini mtandao wao.
Ameendelea kueleza kuwa watuhumiwa hao pamoja na vielelezo walivyokamatwa navyo watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.
Aidha Jeshi la Polisi mkoa wa Simiyu linatoa wito kwa Wananchi kuacha tabia ya kuwinda wanyamapori bila kufuata Sheria,Kanuni na taratibu zilizowekwa na pia wamewaomba wananchi kutoa taarifa za majangili ili tuweze kulinda raslimali zetu kwa manufaa ya kizazi cha kesho.
Naye Afisa Mhifadhi wa pori la Akiba la Maswa mkoani humo,Lawrence Okode amesema kuwa kwa wanyama hao kuuawa kumeisababishia Serikali hasara ya Shilingi Milioni 38 sambamba na kuwapoteza wanyama hao ambao wanalindwa kisheria.
Amesema wataendelea na operesheni hiyo ya kuwakamata watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kijangili na watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
"Operesheni kali inaendelea katika maeneo yaliyo kandokando ya pori la Akiba la Maswa ilikubaini wanaofanya biashara hizo haramu, hivyo natoa wito kwa wanaojihusisha na biashara hizo kuacha mara Moja na hatutomfunbia macho mtu yeyote anayejihusisha na biashara haramu ya ujangili,"amesema.
Post a Comment