MBUNGE KOKA AWANYOSHEA KIDOLE WANAOWATUKANA VIONGOZI
Na Gustafu Haule, Pwani
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini (CCM) Silvestry Koka,amewatolea uvivu baadhi ya watu wanaomsema vibaya na kutoa lugha za kejeli kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa waache tabia hiyo.
Koka ,amesema watu kama hao hawatavumilika kwani wakibainika watakiona cha mtemakuni na katika kufanya maamuzi hayo haitaangalia mtu kutoka CCM au upinzani.
Koka, ametoa kauli hiyo Agosti 12 mwaka huu wakati akizungumza na wanachama wa CCM ,wananchi na viongozi wa CCM tawi la Mailimoja lililopo Kata ya Mailimoja wakati akifungua mradi wa choo cha tawi hilo ulioanzishwa kwa ajili ya kuongeza pato la tawi hilo.
Mbunge huyo, amesema kuwa kuna watu ambao hawana nia njema na Serikali ya awamu ya sita na mara nyingi wamekuwa wakitukana viongozi wakuu wa nchi jambo ambalo halitaweza kuvumilika.
Amesema kuwa, hataachwa mtu salama kama anaendelea kufanya mambo yasiyo na maadili kwakuwa hataki kuona mpasuko bali kinachotakiwa ni kuungana kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka akikata utepe kuashiria ufunguzi wa mradi wa choo katika tawi la CCM Mailimoja hafla iliyofanyika Agosti 12 mwaka huu
Amesema kuwa ,Rais Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo na katika kudhihirisha hilo Jimbo la Kibaha mjini ni miongoni mwa majimbo ambayo yamepata miradi mingi ya maendeleo kuliko majimbo mengine hapa nchini.
Amesema , Kibaha mjini imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta ya afya, Elimu,barabara, maji na umeme na itazidi kupiga hatua kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo baina yake na Serikali ya awamu ya Sita.
"Niwaambie jambo, Kibaha mambo mazuri yanakuja na husidanganywe na mtu hakuna wakati kama nina mahusiano mazuri ya chama na Serikali kama awamu hii ya Sita , kwahiyo tumuunge mkono Rais wetu,"amesema Koka
Kuhusu mradi wa Choo cha CCM tawi la Mailimoja Mbunge huyo amewapongeza viongozi wa tawi hilo kwa jitihada walizofanya ambapo ameahidi kuwachangia kiasi cha Sh.720,000 kwa ajili ya kumalizia changamoto ndogondogo za mradi huo.
Katibu wa CCM tawi la Mailimoja Shamimu Masoud, amesema kuwa walianza kujenga mradi huo mwaka 2021 na ilipofika 2023 Juni mradi huo ulikuwa umekamilika kwa asilimia 99 huku ukigharimu zaidi ya milioni 13.
Katibu wa CCM tawi la Mailimoja Shamimu Masoud akimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka risala ya mradi wa choo cha tawi hilo katika ufunguzi uliofanyika Agosti 12 mwaka huu katika ofisi za tawi hilo.
Shamimu, amesema kukamilika kwa mradi huo kumetokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali ikiwemo taasisi ya Allawi Foundation,Kampuni ya Nangara Traders pamoja na Solomon Mtula.
Shamimu, amewashukuru wadau hao huku akisema lengo la kuanzisha mradi huo ni kutaka kuwaongezea kipato ili tawi hilo liweze kujitegemea lenyewe na hivyo kuacha tabia ya kuombaomba.
"Sisi tawi la CCM hapa Mailimoja tulikaa na kubuni mradi wetu wa kujiongezea mapato tukaona bora tujenge mradi wa choo ambao watu watakuwa wanalipia na tumefanya hivi ili tuache tabia ya kila wakati kutembeza bakuli kwa wadau,"amesema Shamimu.
Hatahivyo, mwenyekiti wa CCM Kata ya Mailimoja Mathayo Mkayala,ametumia nafasi hiyo kumshukuru mbunge kwa namna anavyojitoa kusaidia wananchi wake huku akiahidi kumpa ushirikiano kwa kila jambo.
Post a Comment