MTOTO WA MIEZI NANE AKATWA KILIMI NA KUTELEKEZWA
Na ASP Richard Minja, Tarime Rorya
JESHI la Polisi Mkoa wa Tarime Rorya linamshikilia mama mmoja kwa tuhuma za kumkata kilimi mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miezi nane na kisha kumtelekeza nyumbani kwa mtu asiyemfahamu mwanzoni mwa Agosti 2023.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime Rorya Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Mark Njera amesema mama huyo mwenye umri wa miaka 25 na mzazi wa watoto watano alitenda kosa hilo 16 Agosti, 2023 baada ya kumpeleka mtoto huyo kwa mganga wa kienyeji kwa lengo la kumtibu kutapika na kuharisha.
Amesema alipatiwa Tiba ya kukatwa kilimi, na baada ya kuona hali ya mtoto inakuwa mbaya alimlaza chini karibu na nyumba ya jirani yake iliyoko mtaa wa Rebu sokoni na kutokomea kusikojulikana.
Majirani zake walimsaka na walipomkamata walimfikisha kituo cha Polisi cha Wilaya ya Tarime na kisha kupelekwa hospitali ya Wilaya.
Katika hali isiyo ya kawaida mama huyo alipofikishwa hospitalini alipewa kitanda katika wodi namba nne na muda mchache aliwaaga manesi kuwa anakwenda kununua maji ya kunywa na kisha kumtorosha mtoto huyo aliyekuwa akipatiwa huduma hospitalini hapo.
Juhudi za kumtafuta mtuhumiwa ziliendelea ambapo Agosti 28, 2023 wasamaria wema walimkamata mama huyo na kumpeleka katika Dawati la Jinsia na Watoto lakini hali ya mtoto ilionekana kuwa mbaya na kupelekwa kupatiwa matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Tarime huku mama yake akishikiliwa kusubiri taratibu za kisheria.
Mnadhimu Mkuu namba moja wa Mkoa wa Polisi Tarime Rorya ACP Ame Anoqie akiambatana na Mkuu wa Uchunguzi wa Kisayansi Mkoa ASP Richard Minja na Mkuu wa Dawati la jinsia na watoto mkaguzi msaidizi Amina Hoza walifika hospitali kuonana na Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime Joshua Makoa.
Taarifa kutoka katika hospiti hiyo zinaeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Julai na Agosti jumla ya watoto saba wenye umri chini miaka miwili waliofanyiwa ukatili wa kukatwa kilimi na kung’olewa meno ya plastiki (meno ya awali) waliofikishwa hospitalini hapo wanne kati yao walifariki.
Hata hivyo, juhudi mbali mbali zilifanyika za kuelimisha jamii kuacha dhana potofu ya kung’oa watoto meno ya plastiki na kutaka kilimi ambapo Kata zote za Wilaya ya Tarime mjini na Vijijini zilifikiwa.
Imeelezwa kuwa wadau walioshiriki kutoa elimu hiyo ni wataalamu wa kinywa na meno toka hospitali ya wilaya ya Tarime, wataalamu wa vituo vya afya vya kila kata, viongozi wa serikali ngazi ya Kata, Polisi Kata na watoa huduma za asili.
Jeshi la Polisi Tarime Rorya linawaonya wananchi wote wenye kufanya matendo hayo ya ukatili kwa watoto kuacha mara moja, na pale watakapobainika watafikishwa katika vyombo vya sheria.
Post a Comment