TIA KAMPASI YA MWANZA NA MIKAKATI YENYE TIJA KATIKA UTOAJI WA TAALUMA
Na Nashon Kennedy, Ilemela
TAASISI ya Uhasibu Tanzania ( TIA) Kampasi ya Mkoa wa Mwanza imesema katika utoaji wake wa taaluma imejipanga kwenda sambamba na mabadiliko ya uchumi wa kidijitali na sayansi na teknolojia ili kutoa mafunzo ya kitaaluma yanayokwenda na mabadiliko hayo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa TIA Kampasi ya Mwanza Dk Honest Kimario alipokuwa akieleza mipango iliyopo ya Taasisi kwenye maonesho ya wakulima (Nanenane) Kanda ya Ziwa Magharibi inayohusisha mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera yanayoendelea katika viwanja vya Nyamhongolo vilivyopo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Mkuu wa TIA Kampasi ya Mwanza Dk Honest Kimario
Amesema mkoa wa Mwanza ni mkoa wa pili wenye idadi kubwa ya watu na unaochangia kwenye Pato la Taifa baada ya Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba idadi ya watu ni moja kati ya vigezo vinavyoonyesha ukuaji wa uchumi kwa sababu mtaji wa watu(Human Capital) una mchango mkubwa wa kuhuisha maeneo yote ya uzalishaji kwa maana ya ardhi, raslimali muda na fedha.
Amesema raslimali zote hizo mwenye uwezo wa kuzibadilisha(transform) ili viweze kuwa bidhaa za mwisho kwenye uzalishaji( final goods) zitakazosaidia kwenye ukuaji wa uchumi ni raslimali watu.
“Kwahiyo wingi wa watu Mwanza ni mtaji, kama Taasisi kwa kutambua watu wanakua kwa kasi, na tuliangalia mwelekeo (trend) wa taasisi, tukagundua inakua kwa asilimia 342 ndani ya kipindi cha miaka 10 (2012-2022)”, amesema.
Amesema kutokana na ukuaji huo, awali TIA ilikuwa na wanachuo 1466 na kwamba katika kipindi cha miaka 10 ijayo, idadi ya watu inatarajia kuongezeka kutokana na sababu hizo, hivyo TIA ilianza ujenzi wa miundombinu ya Taasisi katika eneo la Nyangomango.
Amesema ujenzi huo umeanza baada ya TIA kuwasilisha andiko likiwa linaonyesha ukuaji wa taasisi(Trend analysis), mchango wa chuo kwenye uchumi wa mkoa wa Mwanza na Taifa kwa ujumla.
“Tunaamini kwa kuwepo kwa wanachuo wengi wanaokuja kujiunga na TIA, wananunua mahitaji yao yote ndani ya mkoa wa Mwanza, hali hiyo ina mchango wa kiuchumi( per capital income) kwa kila mwananchi aliye katika mkoa wa Mwanza”, ameeleza.
Amesema chuo kuhamia eneo la Nyangomango wanategemea jiji la Mwanza litakwenda kuungana na Wilaya ya Misungwi na eneo hilo litazidi kuimarika zaidi kiuchumi baada ya kupata wanachuo wanaohitimu kozi za Ugavi(Procurement) na Uongozi na Ugavi (Logistic and Management).
Dk Kimario akitoa maelezp Kwa mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Muleba Dk Abel Nyamhanga aliyemwakilisha Mkuu wa mkoa wa Kagera( hayupo pichani)
Amesema watakwenda kufanya kazi kwenye sekta za usafirishaji wakisaidia kwenye masuala ya uongozi na ugavi na kuwa sehemu ya kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Mwanza na Taifa kwa ujumla.
TIA pia inawandaa watalaam wake kusaidia kwenye shughuli za kiuchumi kwa madai kuwa mwanachuo anayesoma TIA atapata fursa ya kwenda kufanya uvuvi wa kisasa( Fish cage) katika ziwa Victoria na kufaidi uchumi wa mazao ya aina zote za samaki zinazopatikana katika ziwa hilo.
“Ziwa Victoria ndio ziwa kubwa kuliko maziwa yote katika Bara la Afrika”, alisema na kuongeza ili watu wa mikoa ya Kanda ya ziwa na taifa kwa ujumla waweze kuona mchango wake kwenye uchumi, lazima wanachuo wanaohitimu TIA wazitumie kikamilifu fursa zilizopo katika ziwa katika kujiajiri na kujiimarisha kiuchumi kutokana na elimu waliyoipata chuoni hapo.
Wapokea wanafunzi kutoka nje ya nchi
Amesema chuo pia kinao wanafunzi wanaosoma kutoka mataifa ya nje na kwamba kinaboresha miundombinu ya chuo ili kiweze kufanya udahiri kwa wanachuo wengi zaidi kutoka nje ya nchi.
Amesema chuo hicho kwa muda mrefu kimekuwa kinawandaa wanafunzi pindi watakapohitimu mafunzo yao waweze kuchangia kwenye uzalishaji wa kilimo na waweze kujiajiri.
Amesema tayari chuo kina wanachuo waliojiunga na Kituo Atamizi cha Mawazo ya Biashara ambacho mwanachuo hukitumia katika kuwasilisha wazo lake la kibiashara ambapo huunganishwa na Mwalimu anayehusika na masuala ya ujasiriamali na walimu na wajasiriamali mbalimbali walio ndani ya mkoa wa Mwanza na nje ya Mkoa wa Mwanza.
“Anasikilizwa kuhusiana na wazo lake na hatimaye huliboresha na kumpatia manufaa ya kiuchumi ikiwemo kuongeza thamani za bidhaa mbalimbali za kilimo”, alisema.
Ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa Kampasi ya Mwanza ambazo zitatumika kwa ajili ya kufanya tafiti na ujenzi wa mabweni ikiwa ni moja ya taasisi iliyonufaika na fedha hizo..
“Watalaam wetu wa kampasi mbalimbali zilizopo nchini watatumia fedha hizo kufanya tafiti mbalimbali ambazo majibu yake yatakuwa na mchango mkubwa sana kwenye kukua kwa uchumi wa nchi”, alisema.
Ameongeza pia Taasisi imepata fedha za kupeleka wafanyakazi wa Jinsia ya kike kwenda kusoma Shahada ya Uzamili kupitia mradi atamizi.
Uchumi wa Digital
Kuhusu dunia kuingia kwenye uchumi wa kidigitali kutokana na utandawazi, Dk Kimario amesema TIA kama Taasisi ya Elimu ya Juu, imefanya tafiti mbalimbali zikiwemo zile zinazojikita kwenye mapinduzi ya viwanda vya kati sanjari na ukuaji wa uchumi wa kati, kupitia viwanda.
“Zipo tafiti zilizofanywa ambazo baadhi ya tafiti hizo zimechapishwa na taasisi kwenye majarida makubwa sana duniani”, .kupitia tafiti hizo wamebaini kuwepo kwa maeneo mbalimbali yakiwemo ya usafirishaji, viwanda na eneo la uzalishaji jinsi gani mzalishaji anatakiwa kuunganishwa moja kwa moja na viwanda ambayo yanahitaji kufanyiwa maboresho.
“Wakulima wawe connected ( Waunganishwe) na viwanda, lakini pia watalaam wetu na sehemu mbalimbali kwa ujumla”, amesema.
Kozi zinazotolewa na TIA
Amezitaja kozi zinazotolewa kuwa ni raslimali watu inayotolewa kuanzia ngazi ya cheti hadi Shahada ya kwanza. Nyingine ni Masoko na Uhasibu( Cheti hadi Shahada ya kwanza), Uhasibu(Cheti hadi Shahada ya Kwanza), Ununuzi na Ugavi( Cheti hadi Shahada ya kwanza.
“Lakini pia tumeanzisha Programu mpya ya Shahada ya Ualimu wa Uhasibu na Stadi za biashara, hii itawasaidia walimu wengi waliotoka kazini kujiendeleza”, anaeleza.
Shukrani kwa uongozi
Dk Kimario amemshukuru sana Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA Profesa William Pallangyo kwa jinsi ambavyo anavyoongoza taasisi hiyo kwa hekima, upendo na weledi wa hali ya juu.
“Hakika amekuwa ni baba, kiongozi na mlezi wetu, amekuwa mshauri wetu katika masuala ya taaluma, utendaji kazi wetu na umoja na mshikamano, mambo ambayo yameendelea kuongeza tija kubwa katika utendaji wa taasisi yetu.
" Amesema na kuushukuru pia uongozi wa Mkoa wa Mwanza chini ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wa sasa Amos Makalla na wakuu wengine waliotangulia ambao wametoa mchango mkubwa kwa taasisi ikiwemo hata eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikubwa.
“Nawashukuru pia wafanyakazi wenzangu kwa kuendelea kuwa na mshikamano wa pamoja na hivyo kuwezesha utendaji kazi wa kila siku wa taasisi yetu kuwa wa mafanikio”, alisema na kuwashukuru wananchi wa mkoa wa Mwanza kwa kuendelea kukiunga mkono chuo hicho na kuwaomba wakitumie chuo katika kuwasomesha vijana wao ambacho kina walimu wenye ubobevu wa hali ya juu.
TIA yamshukuru Rais Samia kwa utoaji fedha
Dk Kimario amesema TIA Kampasi ya Mwanza inamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Taasisi hiyo kiasi cha Sh bilioni 7.8 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la taaluma.
Amesema fedha hizo zilizotolewa katika mwaka wa fedha 2021/22 kupitia Wizara ya Fedha zimeiwezesha Taasisi hiyo kujenga jengo lenye vyumba vya madarasa vyenye uwezo wa kuhudumia wanachuo 1,100 kwa wakati mmoja.
“Lakini pia tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa sababu jengo hilo lina maktaba ya kisasa yenye uwezo wa kuhudumia wanachuo 250 ambayo ndani yake kuna majarida ya aina mbalimbali ya uchumi”, amefafanua.
Amesema jengo hilo pia lina maabara ya kisasa ya kompyuta yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 200 kwa wakati mmoja na kufafanua kuwa ni jengo litakaloiwezesha taasisi hiyo kuwa na uwezo wa kusajiri wanachuo 1550.
Amesema ujenzi wa jengo hilo umefanywa kwa njia za kisasa zaidi ambao utasaidia kuwapata wanachuo wengi kutoka nchi za nje kwenda kusoma katika taasisi hiyo.
“Wanafunzi hao watakuja na fedha za kigeni ambazo zina mchango mkubwa sana wa kukua kwa uchumi katika taifa letu”, amesema.
Amesema fedha ambayo sasa ingewekezwa kwenye mataifa mengine itakuja kuwekeza nchini Tanzania kupitia wanafunzi wanatoka nje kwenda kusoma TIA.
“Watalipa ada, ambapo wanachuo wanaotoka ndani ya Afrika Mashariki na nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara wanaweza kulipa ada inayolingana sawa na ada yetu”, ..
Amesema kuwa wanafunzi hao wanaotoka nje ya nchi kwenda kusoma TIA watasaidia katika kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini Tanzania kama vile za utalii, elimu na fursa zingine za kiuchumi
Maoni ya Wadau
Baadhi ya wadau wanasema TIA ni miongoni mwa Taasisi bora inayotoa elimu ya uhasibu hapa nchini kupitia kampasi zingine zilizoko mikoani.
Godfrey John mkazi wa jijini Mwanza anasema TIA imekuwa ni taasisi kinara inayotoa wahitimu bora katika fani za uhasibu, ugavi na masoko.
“Ukitembelea karibu ofisi zinazotoa huduma za masoko, ugavi na uhasibu huwezi kukosa product ( mhitimu) kutoka TIA”, anasema na kuiomba TIA iendelea kutoa mafunzo ya kitaluma kwa kuendelea na maono yake ya kwenda na mabadiliko ya kidunia hususani kwenye uchumi wa kidigitali.
Pili Mwita Mkazi wa Buswelu anaipongeza TIA kwa kazi kubwa ya kuielimisha vijana hususani kwenye fani za uhasibu na ugavi na kusaidia katika kujenga uchumi wa taifa.
Wankuru Chacha mkazi wa Bugarika anasema binafsi anaipenda taasisi ya TIA ambayo imekuwa kinara katika utoaji wa taaluma ya uhasibu na ugavi mkoani Mwanza na Tanzania Kwa ujumla.
Post a Comment