ULINZI NA USALAMA WA MTOTO NI JUKUMU LA JAMII
Na Samwel Mwanga, Busega
IMEELEZWA kuwa suala la ulinzi na usalama wa mtoto ni jukumu la jamii nzima na siyo kwa wazazi na walezi tu wa watoto hao.
Hayo yameelezwa na Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu, Masuku Kubagwa wakati wa mafunzo ya dawati la ulinzi na usalama wa mtoto ndani na nje ya shule kwa baadhi ya walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Kabita na shule ya msingi Kabita zilizoko wilayani humo.
Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu,Masuku Kubagwa(aliyesimama)akitoa mafunzo ya ulinzi na usalama kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kabita na Shule ya Sekondari Kabita katika mjini wa Lamadi wilayani humo.(Picha Na Samwel Mwanga)
Amesema kwamba kumlinda mtoto dhidi ya aina zote za vitendo vya ukatili kunapaswa kufanywa na jamii nzima kwani vitendo hivyo huweza kuathiri mfumo wa ukuaji na maendeleo ya mtoto kiakili, kimwili na kisaikolojia.
Amesema kuwa vitendo vya kikatili kwa mtoto kama vile ubakaji, ndoa za utotoni, kudhuru mwili, kutelekezwa pamoja na usafirishaji haramu wa watoto vimekithiri katika jamii.
"Suala la ulinzi wa mtoto ni jukumu la jamii nzima, mlezi na mzazi mmoja mmoja kwa nafasi yake katika ngazi ya familia pamoja na serikali kwa ujumla,"alisema.
Amesema kuwa sehemu nyingine ya muhimu ni ushirikiano na mahusiano ya karibu kati ya mwalimu na mzazi ili kuhakikisha mienendo ya mtoto darasani, mtaani hadi nyumbani.
"Ushirikiano katika malezi ya mtoto kati ya wazazi, walezi pamoja na jamii unahitajika kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha usalama wa mtoto,"amesema.
Aidha, amewataka watoto kutoa taarifa mara moja wanapofanyiwa vitendo vya ukatili ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Walimu na wanafunzi wa shule ya Sekondari Kabita na Shule ya Msingi Kabita wilaya ya Busega kwa ajili mafunzo ya Usalama na ulinzi wa mtoto.
Naye Mwalimu, Felister Gatawa wa shule ya Msingi Kabita amesema kuwa jamii na serikali ikishirikiana hatuwezi hata siku moja kuwaona watoto wakiwa mitaani wanazurura muda ambao wanatakiwa kuwa shuleni nasi tubaki kimya.
" Sheria ya Mtoto Tanzania bara inazipa serikali za mitaa mamlaka ya kulea, kulinda na kutunza watoto walioko katika halmashauri zao hivyo tukishirikiana kwa umoja wetu tutakomesha vitendo vya ukatili wa aina yoyote kwa Watoto wetu,"amesema.
Awali Mkurugenzi wa Shirika la Mass Media Bariadi,Frank Kasamwa amesema kuwa wanatoa mafunzo hayo ikiwa ni utekekezaji wa Kampeni ya kuimarisha usawa wa kijinsia mkoa wa Simiyu kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari katika wilaya za Bariadi na Busega mkoani humo.
Amesema kuwa mafunzo hayo watayatoa kwa shule 13 zikiwemo shule 10 za Msingi na shule tatu kwa wanafunzi 183 na Walimu wa Malezi na Unasihi wapatao 47.
Mafunzo hayo yameandaliwa chini ya Shirika lisilo la kiserikali la Foundation For Civil Society Tanzania.
Post a Comment