WAKERWA BIASHARA YA VYUMA CHAKAVU NA CHUPA ZA PLASTIKI
Na Daniel Limbe, Biharamulo
KATIKA jitihada za kulinda maadili ya vijana pamoja na haki ya watoto kupata elimu bora nchini, Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera limependekeza kupigwa marufuku biashara ya vyuma na plastiki chakavu hasa vijijini.
Mbali na hilo,pia wameshauri kupitiwa upya leseni za michezo ya mabonanza kutokana na kuwa na madhara makubwa kwa wanafunzi ambao hutumia muda wao mwingi kucheza badala ya kwenda shule kujisomea.
Kutodhibitiwa kwa biashara hizo,huenda ikasababisha ongezeko la vitendo vya kiharifu katika jamii, na kwamba ipo haja kubwa ya kukinusuru kizazi cha sasa ili kuwa na taifa imara lenye vijana wasomi na wenye maarifa ukilinganisha na hali ilivyo sasa.
Akichangia hoja ya shughuli za maendeleo zilizotekelezwa na halmashauri ya wilaya ya Biharamulo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 Diwani wa kata ya Runazi, Aniceth Bruno, amesema pamoja na kazi nzuri iliyofanyika ipo hatari kubwa sana ya kupotea maadili mema kwa kundi la vijana na watoto ambao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kucheza mabonanza na kukusanya vyuma na chupa za plastiki kwa lengo la kujipatia pesa.
"Kibaya zaidi watoto na vijana wetu wamekuwa wakiwaibia hadi wazazi wao vifaa kama majembe,Nyundo,sufuria,visu na vyuma vingine kisha kwenda kuuza kwa wanunuzi wa vyuma chakavu, kama haitoshi watoto wengine kutwa nzima wapo mtaani wanakusanya chupa za prastiki na kwenda kuuza hali inayochangia utoro mashuleni"amesema Bruno.
Kutokana na hali hiyo, akashauri hatua za haraka zichukuliwe ili kunusuru kundi la vijana na watoto ambao wapo hatarini kupoteza mwelekeo wa maisha na kwamba ikiwezekana biashara hizo zipigwe marufuku kufanyika vijijini kwa kuwa madhara yake ni makubwa ukilinganisha na mijini.
Kauli hiyo ikaungwa mkono na madiwani wengine huku wakiagiza kitengo cha biashara cha halmashauri hiyo pamoja kitengo cha Utamaduni kufuatilia kwa karibu suala hilo kisha kuja na majibu ya kuridhisha katika kikao cha Baraza la madiwani kijacho.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu,amesisitiza jamii kutofumbia macho mambo yasiyofaa kwa makuzi ya vijana na watoto kwa kuwa madhara ya baadaye ni makubwa na hatari sana kwa mstakabali wa taifa.
Akatumia fursa hiyo kuwaagiza madiwani kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata kuendelea kuwasaka wanafunzi wa sekondari zaidi ya 770 ambao wameacha masomo wilayani humo kwa sababu mbalimbali kisha warejeshwe mashuleni kuendelea na masomo yao.
Diwani wa kata ya Kalenge,Erick Method,akiwasilisha taarifa za maendeleo ya kata yake.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Dk. Sospeter Mashamba,akitoa ufafanuzi wa malalamiko ya wakulima wa tumbaku.
Post a Comment