HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI KATA YA MISUGUSUGU WAMPONGEZA RAIS SAMIA UJENZI ZAHANATI YA SAENI

>> Wasema uongozi wa Rais Samia umewezesha wananchi kujengewa Zahanati.

>> Zahanati imejengwa kwa Milioni 181, fedha kutoka Serikali kuu, mfuko wa Jimbo na mapato ya ndani ya Halmashauri 

>>Kabla ya ujenzi walitembea km 30 kufuata huduma ya afya Mlandizi, Tumbi

>>Sasa hawatatumia gharama za nauli Sh. 50,000 kufuata huduma ya afya

>> Wanawake wasema kabla ya Zahanati Wajawazito walijifungulia njiani.

Na Gustafu Haule, Pwani

WANANCHI wa Mtaa wa Zogowale ,Saeni na Jonuga iliyopo Kata ya Misugusugu katika Halmashauri ya Kibaha Mjini wamempongeza Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka baada ya kujengewa  zahanati ya kisasa katika eneo lao.

Zahanati hiyo imezinduliwa Agosti 11 mwaka huu na mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ambapo mpaka kukamilika kwake imetumia zaidi ya Tsh. Milioni 181 fedha ambazo zimetoka Serikali Kuu,mfuko wa Jimbo na mapato ya ndani ya Halmashauri .


Wakizungumza katika ufunguzi wa Zahanati hiyo baadhi ya wakazi wa Mitaa hiyo akiwemo Sophia Tebe,amesema kuwa awali walikuwa wanasafiri zaidi ya kilomita 30 kufuata huduma ya matibabu katika Mji wa Mlandizi na katika hospitali ya Tumbi.

Tebe amesema changamoto waliyokuwa wanaipata ni katika usafiri kwani mgonjwa anapotaka kusafirishwa gharama ya usafiri inakuwa zaidi ya elfu hamsini huku akisema wajawazito wakati mwingine walikuwa wakijifungua njiani.

Aidha Tebe amesema kuwa mafanikio ya hupatikanaji wa zahanati hiyo yametokana na juhudi za Serikali ya awamu ya Sita chini Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ambaye amekuwa msimamizi mkubwa katika ujenzi huo.


"Sisi Wananchi wa Mitaa ya Zogowale ,Jonuga na Saeni tunawashukuru sana viongozi wetu hususani Rais Samia pamoja na mbunge wetu Koka maana wamepambana mpaka tumepata zahanati hii ,hakika wanastahili pongezi", amesema Tebe.

Nae Halphan Said ,amesema kuwa hupatikanaji wa zahanati hiyo imekuwa mkombozi kwao kwani walikuwa wanashindwa kufuata huduma za afya katika maeneo mengine kutokana na ukosefu wa fedha.

Said amesema ametambua kuwa viongozi waliokuwa madarakani ni wasikivu kwani walipokwenda kuomba kura waliahidi kutatua changamoto ya zahanati, barabara na maji lakini mpaka sasa vyote vimetekelezeka .

      Wananchi wa Mtaa wa Zogowale, Jonuga na Saeni wakishiriki katika ufunguzi wa zahanati mpya ya kisasa iliyojengwa katika eneo lao

"Eeh Mwenyezi Mungu nakuomba uwalinde viongozi wetu akiwemo Rais wa awamu ya Sita Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wetu Silvestry Koka maana tumeona matokeo ya kazi yao, hapa kwetu tuliomba tujengewe zahanati,tuliomba barabara ya lami na maji lakini kwa usikivu wao vyote tumepata,"amesema said.

Diwani wa Kata ya Misugusugu Upendo Ngonyani(CCM) amesema kuwa Zahanati hiyo imeokoa maisha ya wananchi 14,326 wa Kata hiyo waliokuwa wakifuata huduma za afya katika hospitali zilizokuwa mbali nao.

Nyongani amesema kwa kupata zahanati hiyo imekuwa mkombozi kwa mama wajawazito kujifungua kirahisi pamoja kuokoa maisha ya mama na mtoto ambao walikuwa wanapoteza maisha kwa kukosa huduma kwa haraka.

Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa zahanati hiyo Koka,Mbunge huyo amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita ni sikivu na kwamba wananchi watembee kifua mbele kwakuwa imejipanga kutatua changamoto za wananchi wake.

      Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ,akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Zahanati ya Mtaa wa Saeni katika Kata ya Misugusugu uliofanyika Agosti 11 mwaka huu.

Amesema kuwa wakati anakwenda kuwaomba kura wananchi hao alikutana na changamoto za kupewa maji machafu wanayotumia kunywa wananchi hao, barabara na zahanati lakini ameweza kupambana mpaka sasa mambo yako vizuri.

Amesema kuwa , uzinduzi wa zahanati hiyo sio mwisho kwani malengo yake ni kuendelea kuiboresha ili hiweze kufikia hatua ya kuwa kituo cha afya na kufanya huduma za afya zinazotolewa ziwe za kiwango cha juu.

"Nilikuja hapa kipindi cha kampeni nikawaahidi zahanati na nilianza kwa kutoa milioni tano na baadae nikatoa milioni moja na nusu na ndipo Serikali ikatubeba na leo tunafungua zahanati yetu, kwahiyo niwaombe tuendelee kushirikiana kwa ajili ya kutatua kero nyingine,"amesema Koka.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka, amesema kuwa kazi ya CCM ni kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma zote za kijamii hivyo waendelee kukiamini chama kwakuwa kinaweza.




No comments