WASANII WA MUZIKI WA REGE WAKOSHA NYOYO ZA WATAZAMAJI NDANI YA NGOME KONGWE
Na Andrew Chale, Zanzibar
WASANII wa muziki wa Rege (Reggae) kutoka mataifa tofauti wamewapagawisha Wazanzibar kwa kutoa burudani kemkemu katika siku ya kwanza ya msimu wa tano wa tamasha kubwa la kimataifa la muziki wa Reggae Zanzibar linalofanyika mambo Club ndani ya viunga vya Ngome Kongwe, Unguja, Zanzibar.
Wasanii Wanne akiwemo Mash Marley kutoka Zanzibar alikuwa wa kwanza kufungua msimu huo wa tano ambapo alipagawisha kwa nyimbo zake mbalimbali zilizokonga nyoyo za watu waliofika kushuhudia tamasha hilo, Agosti 11, 2023.
Awali Mash Marley aliwaambia mashabiki zake kuwa kwa sasa amerejea rasmi katika muziki huo baada ya kukaa nje kwa miaka 8, akiendelea ba shughuli za kutayarisha muziki na kusimamia wasanii wanaochipukia.
Msanii huyo ameweza kuimba mwenyewe nyimbo kadhaa na baadae alipanda na wasanii wake walioweza kuimba nyimbo kadhaa na kuamsha shangwe.
Msanii wa Pili kupanda jukwaa hilo alikuwa Maveria Mavo kutoka Afrika Kusini ambapo alipagawisha kwa nyimbo mbalimbali.
Msanii kutoka Uganda na baadae CWyne Nakulala (Uganda) ambapo aliweza kukonga nyoyo kwa nyimbo zake za shangwe za Reggae na mwisho Msanii na mwandaaji wa muziki wa Reggae Afrika na Ulaya, Sugardady aliweza kupagawisha jukwaa hilo pia.
Msanii kutoka Uganda CWyne Nakulala
Muziki wa Reggae umekuwa na ukikua kila mwaka visiwani hapa ambapo tayari wageni wa mataifa wamekuwa wakiweka ratiba kufika kuhushudia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Said Omary Hamad 'Side Rasta' ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuunga mkono uwepo wa tamasha hilo huku akiomba wadau waweze kujitokeza kudhamini kwani linaenda kuwa tamasha la mfano Barani Afrika.
"Mwaka huu ni msimu wa tano wa tamasha. Tunashukuru Serikali kuliunga mkono, hivyo tunaendelea kuomba wadau wajitokeze kudhamini ilikuongeza tija ikiwemo kuvutia wageni wengi zaidi.
Tulianza kidogo kidogo na sasa tunaendelea kukua, Taasisi za Serikali na binafsi hii ni fursa kujitokeza kudhamini matamasha haya ilikusaidiana na Serikali katika kukuza uchumi wa bluu." Amesema Side Rasta.
Tamasha hilo la Zanzibar Reggae Festival 2023, linadhaminiwa na Mgahawa unaoelea baharini eneo la Forodhani Unguja wa Dreamers Island, Dreamers Arusha, Conscious Superstar na wengine wengi.
Post a Comment